WIZARA
ya Madini kupitia Tume ya Madini inatarajia kukusanya shilingi bilioni
650 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021-2022 na kuendelea kuboresha
shughuli za uchimbaji na madini ili Sekta ya Madini iwe na mchango
mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi
Hayo
yameelezwa leo tarehe 30 Machi, 2021 mjini Morogoro na Mhasibu Mkuu wa
Wizara ya Madini, Anthony Tarimo alipokuwa akifungua kikao kazi
kilichokutanisha wahasibu kutoka Tume ya Madini Makao Makuu na Ofisi za
Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa chenye lengo la kujenga uelewa wa pamoja
kwenye usimamizi wa mifumo ya fedha pamoja na kutatua changamoto
mbalimbali zinazowakabili katika utendaji kazi.
Alisema
kuwa, ili kuhakikisha lengo la ukusanyaji wa maduhuli katika mwaka wa
fedha 2021-2022 linafikiwa kwa wakati, Tume ya Madini imeweka mikakati
mbalimbali kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na
kuongeza mikakati kwenye udhibiti wa utoroshaji wa madini, usimamizi
zaidi kwenye masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini
vilivyoanzishwa na kuboresha mazingira ya kazi kwa kuhakikisha vitendea
kazi vya kutosha vinakuwepo kwenye ofisi za maafisa madini wakazi wa
mikoa na masoko ya madini.
Akielezea
hali ya ukusanyaji wa maduhuli katika mwaka wa fedha 2020-2021, Tarimo
alisema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 2020 hadi Februari, 2021
Tume ya Madini ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 399
ikiwa ni sawa na asilimia 113.7 ya lengo la kipindi husika ambalo
lilikuwa ni kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 351.
Katika
hatua nyingine, Tarimo aliwataka wahasibu kuendelea kuwa wabunifu
kwenye utendaji kazi na kusisitiza kuwa Wizara ya Madini itaendelea
kutatua changamoto mbalimbali katika ukusanyaji wa maduhuli ili
kuhakikisha kuwa Sekta inazidi kukua na kufikia mwaka 2025 inakuwa na
mchango wa asilimia 10 kwenye pato la Taifa.
Wakati
huohuo, Mkurugenzi wa Huduma za Tume ya Madini, William Mtinya alisema
kuwa lengo la kikao hicho lilikuwa ni kuwapa wahasibu uelewa wa pamoja
kuhusu usimamizi wa Sekta ya Madini hususan kwenye ukusanyaji wa
maduhuli kwa kutumia mifumo mbalimbali.
Mtinya
alieleza maeneo mengine yanayoangaziwa katika kikao hicho kuwa ni
pamoja na kujadili taarifa za utekelezaji wa ofisi za maafisa madini
wakazi wa mikoa, usimamizi wa fedha za umma, sheria ya fedha za umma,
uandaaji wa taarifa mbalimbali za kifedha na kuweka maazimio
yatakayosaidia kutoa taarifa sahihi na kuwezesha menejimenti kufanya
maamuzi yenye tija.
No comments :
Post a Comment