Thursday, March 11, 2021

WAZIRI MPANGO AWASILISHA MPANGO NA UKOMO WA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2021/22 JIJINI DODOMA

Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai (kulia) akizungumza na Waheshimiwa Wabunge wakati wa uwasilishwaji wa Mapendekezo ya Serikali ya  Mpango, Kiwango  na Ukomo wa Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2021/22 katika Ukumbi wa  Pius Msekwa Jijini Dodoma. Katikati ni Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa na kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango  akiwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya  Mpango, Kiwango  na Ukomo wa Bajeti  kwa mwaka wa Fedha 2021/22 katika Ukumbi wa  Pius Msekwa Jijini Dodoma.

Waheshimiwa Mawaziri, Wabunge na Watendaji wa Serikali wakifuatilia uwasilishwaji wa Mapendekezo ya Serikali ya  Mpango, Kiwango  na Ukomo wa Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2021/22 katika Ukumbi wa  Pius Msekwa Jijini Dodoma.

PICHA NA BUNGE

…………………………………………………………………………………..

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA 

WIZARA YA FEDHA NA MPANGO 

MAELEZO YA MHE. DKT. PHILIP I. MPANGO (MB), WAZIRI WA FEDHA NA  MIPANGO, AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA SERIKALI YA  MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA NA KIWANGO CHA UKOMO WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2021/22 

DODOMA 

11 MACHI, 2021 

UTANGULIZI

  1. Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kutumia fursa hii kumshukuru  Mwenyezi Mungu, kwa kuendelea kutujalia uhai na afya njema na kutuwezesha wote  kukutana tena hapa Jijini Dodoma kupokea Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa  Maendeleo wa Taifa na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/22.  Aidha, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuijalia nchi yetu umoja, amani na  utulivu. 
  2. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua fursa hii kutoa pole kwa Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, ndugu, jamaa na marafiki kwa vifo  vilivyotokea wakati wa mkutano uliopita: Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla  aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Manyara; na Mheshimiwa Atashasta  Justus Nditiye aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Muhambwe (CCM). Tunamwomba Mwenyezi Mungu azipumzishe roho zao kwa amani. Aidha napenda kuchukua fursa hii  kumpongeza Mheshimiwa Yustina Arcadius Rahhi (Mb.), kwa kuteuliwa kwake kuwa  Mbunge, Viti Maalum CCM, Manyara.  
  3. Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii inawasilisha Mapendekezo ya Serikali ya  Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa  Mwaka 2021/22. Wasilisho hili ni kwa mujibu wa Kanuni ya 116 fasili ya (1) na (2) ya  Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Juni 2020. Aidha, taarifa hii imegawanyika katika  sehemu kuu tatu: Sehemu ya Kwanza ni Tathmini ya Mwenendo wa Hali ya Uchumi;  Sehemu ya Pili ni Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka  2020/21 na Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka  2021/22; na Sehemu ya Tatu ni Tathmini ya Utekelezaji wa Bajeti kwa Kipindi cha Julai  2020 hadi Januari 2021 na Mapendekezo ya Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali  kwa Mwaka 2021/22. 

SEHEMU YA KWANZA 

TATHMINI YA MWENENDO WA HALI YA UCHUMI 

  1. Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto mbalimbali zilizoikumba  dunia ikiwemo mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu, uchumi wa Tanzania  umeendelea kuwa imara. Kuendelea kukua kwa uchumi kumetokana na utekelezaji  madhubuti wa sera za bajeti na fedha chini ya uongozi thabiti wa jemedari wetu,  Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania. 
  2. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2020, Pato  la Taifa lilikua kwa asilimia 4.7. Aidha, mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 3.5  Januari 2021 ikilinganishwa na asilimia 3.7 Januari 2020. Riba za amana kwa kipindi cha  mwaka mmoja zilipungua kufikia asilimia 8.41 Desemba 2020 kutoka asilimia 8.90  Desemba 2019 na riba za mikopo ya kipindi cha mwaka mmoja imepungua na kufikia  wastani wa asilimia 15.72 Desemba 2020 kutoka asilimia 16.28 Desemba 2019. Thamani  ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani na sarafu nyingine duniani imeendelea  kuwa tulivu kutokana na utekelezaji wa sera thabiti za fedha na bajeti pamoja na  kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho wa mali nje  ya nchi. 

  1. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka  2020/21, urari wa malipo ya kawaida unaojumuisha biashara ya bidhaa, huduma,  mapato ya vitega uchumi na uhamisho mali wa kawaida uliimarika kufikia nakisi ya dola  za Marekani milioni 331.3 kutoka nakisi ya dola za Marekani milioni 344.3 katika kipindi  kama hicho mwaka 2019/20. Hii ilitokana na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa nje kwa  asilimia 17.6 na kupungua kwa uagizaji wa bidhaa kutoka nje kwa asilimia 14.1. Aidha,  mapato na malipo ya huduma yalipungua kutokana na kupungua kwa huduma za usafiri  ikijumuisha utalii na safari za nje. Hadi Desemba 2020, akiba ya fedha za kigeni ilifikia  dola za Marekani bilioni 4.8 inayokidhi uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi kwa  kipindi cha miezi 5.6.  
  2. Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi Desemba 2020, deni la Serikali lilikuwa shilingi  trilioni 59.0, sawa na ongezeko la asilimia 7.6 ikilinganishwa na shilingi trilioni 54.8  kipindi kama hicho mwaka 2019. Kati ya kiasi hicho, deni la nje ni shilingi trilioni 42.8 na  deni la ndani ni shilingi trilioni 16.2. Ongezeko hilo limetokana na: kupokelewa kwa  fedha za mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi  wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme na maji; na malimbikizo  ya riba ya deni la nje, hususan nchi zisizo wanachama wa kundi la Paris Club ambazo  Serikali inaendelea kujadiliana nazo. Aidha, matokeo ya tathmini ya uhimilivu wa deni  iliyofanyika Desemba 2020 yanaonesha kuwa deni ni himilivu kwa muda mfupi, wa kati  na mrefu. 

SEHEMU YA PILI 

TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA 2020/21 NA  MAPENDEKEZO YA SERIKALI YA MPANGO WA MAENDELEO  

WA TAIFA KWA MWAKA 2021/22 

  1. TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA  WA MWAKA 2020/21 
  2. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2020/21, Serikali ilitenga jumla ya  shilingi trilioni 12.8, sawa na asilimia 37 ya bajeti ya Serikali kwa ajili ya kugharamia  miradi ya maendeleo. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 10.0, sawa na asilimia 78.6, ni  fedha za ndani na shilingi trilioni 2.7, sawa na asilimia 21.4, ni fedha za nje. Hadi  Januari 2021, ridhaa ya matumizi ya fedha za kugharamia miradi ya maendeleo ilikuwa  shilingi trilioni 4.7, ikijumuisha shilingi trilioni 3.4 fedha za ndani na shilingi trilioni 1.2  fedha za nje.  
  3. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021,  Serikali iliendelea kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21,  ambao pia ni mpango wa mwisho wa utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa  Taifa 2016/17-2020/21 . Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: 

(i) Reli: Serikali inaendelea na ujenzi wa reli ya kati ya kiwango cha Kimataifa  (Standard Gauge Railway – SGR) ambapo ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) umefikia asilimia 90 na kipande cha Morogoro – Makutupora 

(km 422) umefikia asilimia 52.2, kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa kipande  cha Mwanza – Isaka (km 341) utakaogharimu shilingi trilioni 3.07; na kuendelea  kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa vipande vya Makutupora – Tabora (km 294)  na Tabora – Isaka (km 133). Jumla ya shilingi bilioni 596.8 zimetumika katika  kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021. Aidha, ukarabati wa miundombinu ya  reli ya kati kutoka Dar es Salaam – Isaka (km 970) umekamilika na huduma za  usafirishaji wa abiria na mizigo katika reli ya Tanga hadi Arusha (km 439)  zimerejeshwa baada ya ukarabati kukamilika; 

(ii) Uboreshaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL): kupokelewa kwa ndege  mpya mbili aina ya Bombadier Dash 8-Q400 na Boeing 787-8 Dreamliner;  kukamilika kwa malipo ya awali ya ununuzi wa ndege tatu (3), ambapo ndege  mbili (2) ni aina ya Airbus A220-300 na moja (1) ni Dash 8-Q400 De-Havilland na  hivyo kuwezesha Serikali kuwa na ndege mpya 11 kutoka ndege moja (1)  iliyokuwepo mwaka 2015 na kuifanya ATCL kuwa na jumla ya ndege 12 ambapo  ndege tatu (3) zinatarajiwa kuwasili mwaka 2021/22. Katika kipindi cha Julai 2020  hadi Januari 2021 jumla ya shilingi bilioni 31.6 zimetolewa; 

(iii) Viwanja vya Ndege na Rada: kuendelea na ujenzi wa viwanja vya ndege vya  Geita (asilimia 98), Songea (asilimia 95) na Mtwara (asilimia 53.2); kukamilika  kwa maandalizi ya mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha  Msalato ambao utagharimu dola za Marekani milioni 330, sawa na shilingi bilioni  759; uzinduzi wa ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege vya Shinyanga,  Kigoma, Tabora na Sumbawanga (Rukwa) vinavyogharimu Euro milioni 50, sawa  na shilingi bilioni 136.85. Jumla ya shilingi bilioni 5.0 zimetumika katika kipindi  cha Julai 2020 hadi Januari 2021; 

(iv) Mradi wa Kufua Umeme wa Maji – Julius Nyerere MW 2,115: kuendelea  na ujenzi wa tuta kuu la bwawa; kukamilika kwa handaki la kuchepushia maji;  kuendelea na ujenzi wa mgodi wa kuzalisha umeme, ujenzi wa njia za kupeleka  maji kwenye mitambo na ununuzi wa vifaa mbalimbali vya mradi. Shilingi bilioni  249.3 zimetumika katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021; 

(v) Miradi ya Umeme: kukamilika kwa ujenzi na upanuzi wa vituo vya kupoza  umeme pamoja na njia za kusafirisha umeme katika Mradi wa Njia ya Kusafirisha  Umeme wa Msongo wa KV 220 Bulyanhulu – Geita; kuendelea na ujenzi wa njia  ya kusafirisha umeme wa msongo wa KV 400 Singida – Arusha – Namanga  ambapo utekelezaji umefikia asilimia 86; kukamilika kwa asilimia 73.3 ya mradi  wa Kufua Umeme – Rusumo MW 80; kuendelea na mradi wa Kinyerezi I Extension  MW 185 ambapo utekelezaji umefikia asilimia 84; kukamilika kwa usanifu wa  miradi ya Kakono MW 87 na Malagarasi MW 45; kuendelea kuhuisha upembuzi  yakinifu na usanifu wa miradi ya kufua umeme wa maji ya Ruhudji MW 358 na  Rumakali MW 222; na kukamilika kwa upembuzi yakinifu na kuendelea na  uthamini wa mali za wananchi watakaopisha mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme  wa Msongo wa kV 400 Rufiji – Chalinze – Dodoma na Chalinze – Kinyerezi. Hadi  Januari 2020, jumla ya vijiji 10,018 kati ya vijiji 12,317 viliunganishiwa umeme,  sawa na asilimia 81.3 ya vijiji vyote. Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari  2021 shilingi bilioni 323.7 zimetumika; 

(vi) Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda)  hadi Tanga (Tanzania): kukamilika kwa tathmini ya athari za mazingira;  kuendelea na utoaji wa elimu kwa umma kwa maeneo ya pembezoni mwa eneo  la mradi; kukamilika kwa majadiliano ya maeneo mawili (2) kati ya matatu (3) ya  mikataba ikiwemo ya nchi hodhi na wawekezaji, mkataba wa ubia, mkataba wa  bandari na mkataba wa pango la ardhi; 

(vii) Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia – Lindi: kukamilika kwa  ulipaji wa fidia kwa wananchi watakaopisha mradi; na kuendelea na majadiliano  baina ya Serikali na kampuni za uwekezaji kuhusu mikataba hodhi ya utafutaji wa  gesi na uendelezaji wa mradi. Hadi Desemba 2020, shilingi bilioni 6.0 zimetumika  katika maandalizi ya mradi, ikijumuisha kulipa fidia kwa wananchi watakaopisha  mradi; 

(viii) Ujenzi wa Barabara na Madaraja Makubwa: kujengwa kwa mtandao wa  barabara kwa kiwango cha lami wenye urefu wa kilomita 3,537 (barabara kuu na  za mikoa kilomita 2,208.6 na barabara za halmashauri kilomita 1,328) na hivyo  kufanya mtandao wa barabara uliojengwa kwa kiwango cha lami hadi mwaka  2020/21 kufikia kilomita 13,044 ambapo kilomita 10,939 ni barabara kuu na  kilomita 2,105 ni barabara za mikoa. Miradi iliyotekelezwa ni pamoja na:  kuzinduliwa na kuanza kutumika kwa barabara ya juu (Interchange) ya Kijazi;  kuendelea na ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza) lenye urefu wa  kilomita 3.2 na upana wa mita 28.45 ambapo utekelezaji umefikia asilimia 14.5;  na daraja la Tanzanite lenye km 1.03 (Dar es Salaam) na barabara unganishi  zenye jumla ya urefu wa km 5.2 ambapo ujenzi umefikia asilimia 62. Shilingi  bilioni 623.2 zimetumika katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021;  

(ix) Uendelezaji wa Bandari: katika Bandari ya Dar es Salaam shughuli  zilizofanyika ni pamoja na kuboreshwa kwa gati namba 1 – 4; kukamilika kwa  ujenzi wa gati la kupakia na kushushia magari (RoRo); na kuendelea na  uboreshaji wa gati na 5 hadi 7. Shilingi bilioni 42.6 zimetumika katika kipindi cha  Julai 2020 hadi Januari 2021. Aidha, katika Bandari ya Mtwara, ujenzi wa gati  jipya lenye urefu wa mita 300 na yadi ya kuhudumia makasha umekamilika.  Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021 shilingi bilioni 45.0 zimetumika. 

Vile vile, katika Bandari ya Tanga kina cha lango la kuingia meli kimeongezwa  kutoka mita nne (4) hadi mita 13 na ujenzi wa gati mbili (2) kwenye kina kirefu umekamilika. Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021 shilingi bilioni 20.4  zimetumika; 

(x) Kuboresha Usafiri wa Abiria na Mizigo katika Maziwa Makuu: Kukamilika  kwa ukarabati wa meli mbili (2) za New Butiama Hapa Kazi Tu na New Victoria  Hapa Kazi Tu; kuendelea na ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu  yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo; kukamilika kwa  ujenzi wa Chelezo cha kujengea na kukarabati meli katika Bandari ya Mwanza 

chenye uwezo wa kubeba meli yenye uzito wa kuanzia tani 1 hadi 4,000, kikiwa  na reli na mfumo unaowezesha kupandisha meli zaidi ya moja kulingana na  ukubwa; kukamilika kwa ujenzi wa matishari mawili (2) yenye uwezo wa kubeba  tani 1,000 kila moja; na ujenzi wa meli moja mpya ya MV Mbeya II yenye uwezo 

wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200 umekamilika na kuanza kufanya kazi.  Shilingi bilioni 20.2 zimetumika katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021; 

(xi) Uendelezaji wa Viwanda: Baadhi ya viwanda vilivyojengwa ni: Kilimanjaro  International Leather Industries Co Ltd (awamu ya kwanza) katika mkoa wa  Kilimanjaro; Taifa Leather Company Ltd, Murzar Wilmar Rice Mills Ltd na  Mahashree Agro-processing Tanzania Ltd vilivyopo Morogoro; majengo ya  viwanda (Industrial Sheds) kwa ajili ya wajasiriamali katika mikoa ya Kagera,  Kigoma, Geita, Mtwara na Ruvuma; kiwanda cha chai cha Kabambe (Njombe);  kiwanda cha Yalin Cashewnut Company Ltd kinachobangua korosho (Mikindani – 

Mtwara); na jengo la kiwanda kipya cha kuunganisha matrekta TAMCO – Kibaha.  Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021 shilingi bilioni 6.0 zimetumika; 

(xii) Kilimo: Kuendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya umwagiliaji ambayo  imeongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 461,376 mwaka 2015 hadi  hekta 694,715 mwaka 2020; kuongezeka kwa uzalishaji wa mbegu bora kutoka  tani 36,614 mwaka 2015 hadi tani 76,726 mwaka 2020; kuongezeka kwa  upatikanaji wa mbolea kutoka tani 302,450 mwaka 2015 hadi tani 727,719  mwaka 2020; kusambazwa kwa tani 40,592.6 za salfa na lita 1,314,465 za  viuatilifu maji kwa wakulima wa korosho; na kuendeshwa kwa minada nane (8)  ya kahawa katika mikoa ya Kilimanjaro (2), Songwe (4) na Ruvuma (2). Shilingi  bilioni 29.5 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21; 

(xiii) Mifugo: kukarabatiwa kwa minada ya mifugo ya upili ambapo utekelezaji  umefikia asilimia 95 katika mnada wa Ipuli – Tabora, Igunga – Tabora (asilimia  90) na Nata – Tabora (asilimia 70); kuimarishwa kwa kituo cha Taifa cha  Uhimilishaji (National Artificial Insemination Centre – NAIC) kilichopo USA River,  Arusha kwa kununua madume nane (8) ya mbegu; kuzalishwa na kusambazwa  kwa mitamba 2,224 katika Mashamba ya Serikali; kuzalishwa na kusambazwa  kwa dozi 84,801,750 za chanjo za mifugo katika halmashauri 184; kuendelea na  ujenzi wa jengo la kuzalisha chanjo za bakteria katika Kituo cha Kuzalisha Chanjo  cha Kibaha (Tanzania Vacccine Institute – TVI) ambapo ujenzi umefikia asilimia  87. Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021 shilingi bilioni 2.3 zimetumika; 

(xiv) Uvuvi: kukamilika kwa upembuzi yakinifu wa awali (pre – feasibility study) kwa  ajili ya ujenzi wa bandari ya uvuvi; kuimarishwa kwa mialo sita (6) ya kupokelea  samaki katika Ukanda wa Ziwa Victoria, minne (4) Ukanda wa Ziwa Tanganyika; na mitatu (3) katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi; kuendelea na  ukarabati wa kituo cha ukuzaji viumbe maji cha Kingolwira – Morogoro;  kuanzishwa kwa vituo vya ubora na uthibiti wa mazao ya uvuvi Singida, Kisesya  na Murusagamba; kusambazwa kwa matenki 22 ya kukuzia vifaranga vya  samaki; na kukarabatiwa kwa mabwawa nane (8) katika vituo vinne (4) vya  kuendeleza ukuzaji viumbe maji vya Kingolwira – Morogoro, Mwamapuli – Tabora,  Ruhila – Ruvuma na Nyengedi – Lindi. Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari  2021 shilingi bilioni 1.0 zimetumika;  

(xv) Madini: kupitia na kutunga Sheria, Sera na mikataba ya madini; kuanzishwa kwa  Kampuni mpya ya Twiga Minerals Corporation inayomilikiwa kwa ubia kati ya 

Tanzania (hisa asilimia 16) na Kampuni ya Barrick (hisa asilimia 84) ambapo  imetoa gawio la shilingi bilioni 100; kuanzishwa kwa kampuni ya Tembo Nickel  Corporation ambayo ni ubia kati ya Serikali ya Tanzania (hisa asilimia 16) na  kampuni ya LZ Nickel Mining Ltd (hisa asilimia 84) kwa ajili ya uchimbaji wa  madini ya nickel Kabanga; kujengwa kwa masoko 39 ya madini na vituo 41 vya  kuuzia madini; kukamilika kwa ujenzi wa vituo vinne (4) vya umahiri katika  maeneo ya Bariadi, Musoma, Bukoba na Handeni na kuendelea na ujenzi wa vituo  vya Songea, Mpanda na Chunya. Aidha, ukusanyaji wa maduhuli katika sekta ya  madini umeongezeka hadi shilingi bilioni 360.7, sawa na asilimia 117.4 ya lengo la  kukusanya shilingi bilioni 307.3 katika kipindi Julai 2020 hadi Januari 2021.  Shilingi bilioni 3.3 zimetumika katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021; 

(xvi) Miradi ya Afya: kuendelea kutoa huduma za kupandikiza uloto; kukamilika kwa  ujenzi wa jengo la huduma za dharura na ukarabati wa jengo la X-ray katika  Hospitali ya Rufaa Dodoma; kukamilika kwa asilimia 98.2 ya ujenzi wa Hospitali  ya Uhuru – Dodoma; ununuzi wa mashine ya Positron Emmission Tomography  (PET Scan) kwa ajili ya Hospitali ya Ocean Road; kujenga na kuboresha  miundombinu ya hospitali za rufaa za Mara, Geita, Songwe, Katavi, Sekou Toure  (Mwanza), na hospitali za rufaa za kanda ya kusini Mtwara na kanda ya nyanda  za juu kusini Mbeya na Hospitali ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) na Hospitali ya  Kanda ya Ziwa ya Burigi (Geita). Aidha, mafanikio mengine ni: kuongezeka kwa  idadi ya zahanati kutoka 4,922 mwaka 2015 hadi 6,120 mwaka 2020; vituo vya  afya kutoka 535 mwaka 2015 hadi vituo 710 mwaka 2020; na Hospitali za  Halmashauri za Wilaya kutoka 77 mwaka 2015 hadi 179 mwaka 2020. Shilingi  bilioni 69.4 zimetumika katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021; 

(xvii) Miradi ya Maji Mijini na Vijijini: katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari  2021, Serikali imekamilisha miradi 422 ya maji mijini na vijijini, ambapo miradi  355 ni ya vijijini na 67 ni ya mijini. Aidha, miradi 924 ipo katika hatua mbalimbali  za utekelezaji. Shilingi bilioni 241.3 zimetumika katika kipindi cha Julai 2020 hadi  Januari 2021;  

(xviii) Elimu: kujengwa kwa miundombinu muhimu katika shule 3,904 (Msingi 3,021 na  Sekondari 883), mabweni 547, nyumba za walimu 101, majengo ya utawala 25  na maktaba 43; kukamilika kwa ujenzi wa maboma 2,815 katika shule za msingi  2,133; kuendelea kugharamia elimumsingi bila ada; kukarabatiwa shule kongwe  86 kati ya 89, sawa na asilimia 97 ya lengo; na kuboreshwa kwa miundombinu ya  vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi. Shilingi bilioni 178.0 zimetumika katika  kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021; 

(xix) Mawasiliano na Teknolojia ya Habari: kukamilika kwa mradi wa Mkongo wa  Taifa wa Mawasiliano awamu ya tatu ambayo inajumuisha ujenzi wa Kituo cha  Taifa cha Data cha Dar es Salaam na uunganishwaji wa Zanzibar kwenye Mkongo  wa Taifa; kuendelea na utekelezaji wa Mradi wa Mfumo wa Anuani za Makazi na  Postikodi ambapo uwekaji wa miundombinu ya Mfumo umefanyika katika kata  110 za mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na wadi 8 za Zanzibar; na kuanza  kwa Programu ya kuendeleza wajasiriamali wadogo wanaotengeneza bidhaa za 

TEHAMA nchini. Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021 shilingi bilioni 2.2  zimetumika; 

(xx) Maliasili na Utalii: kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Burigi ambapo jumla  watalii 1,171 walitembelea hifadhi hii kati yao 996 ni wa ndani na 175 ni wa nje  ambapo jumla ya shilingi milioni 492.7 zimekusanywa kuanzia Novemba, mwaka  2019 hadi Desemba, 2020; kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ambapo  jumla ya watalii 9,938 (6,189 wa nje na 3,749 wa ndani) walitembelea hifadhi  hiyo tangu mwezi Novemba, 2019 hadi Desemba, 2020 ambapo jumla ya shilingi  bilioni 1.6 zimekusanywa; kutangazwa kwa vivutio vya utalii katika nchi  mbalimbali duniani; kulinda rasilimali za misitu na kutunza mazingira ambapo  jumla ya Tani 4.9 za aina mbalimbali za mbegu bora za miti na miche ya miti  milioni 24 zimezalishwa; na kuongeza rasilimali za mazao ya misitu na uoto wa  asili ambapo jumla ya hekta 1,876.5 zimepandwa miti. Aidha katika hatua za  kufanya maboresho ya mandhari ya Jiji la Dodoma, jumla ya miche 21,678  ilipandwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji. Shilingi bilioni 183.4 zimetumika  katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021; 

(xxi) Ajira: katika kipindi cha kuanzia Julai, 2020 hadi Januari, 2021 jumla ya ajira  450,416 zimezalishwa katika sekta mbalimbali. Kati ya ajira hizo, ajira 169,475  zimetokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya Serikali na ajira  280,941 zimezalishwa katika sekta binafsi. Aidha, ajira 16,067 zimezalishwa katika  sekta ya umma, ikijumuisha ajira 13,529 za walimu, 1,000 za madaktari na 1,538  katika taasisi mbalimbali za Serikali; na 

(xxii) Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi: kuandaliwa kwa taarifa za mipango  ya matumizi ya ardhi kwa vijiji 59; kuandaliwa kwa Hati za Hakimiliki za Kimila  20,841 katika wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi; kukamilika kwa ujenzi wa  ofisi za ardhi za halmashauri za wilaya za Kilombero na Ulanga; kupimwa kwa  viwanja 95,329 kwenye maeneo ya mradi katika mikoa 19; kurasimisha jumla ya  makazi 1,496,357 katika halmashauri mbalimbali nchini; kuboreshwa kwa Mfumo  Unganishi wa Taarifa za Ardhi; na kununuliwa kwa vifaa vya kisasa vya upimaji.  Shilingi bilioni 5.1 zimetumika katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021. 

  1. MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2021/22 
  2. Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22  ni wa kwanza katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka  Mitano 2021/22 – 2025/26 wenye dhima ya “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda  kwa Maendeleo ya Watu”. Uandaaji wa Mapendekezo ya Serikali ya Mpango  umezingatia: Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Ilani ya CCM kwa Ajili ya Uchaguzi Mkuu  wa Mwaka 2020; Hotuba za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John  Pombe Joseph Magufuli wakati akizindua Bunge la 11 na 12 la Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania; Sera na Mikakati mbalimbali ya kisekta, kikanda na kimataifa zikiwemo Dira ya  Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) 2050; Dira ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa  Afrika (SADC) 2050; Ajenda 2063 ya Maendeleo ya Afrika; na Malengo ya Maendeleo  Endelevu 2030.

  1. Mheshimiwa Mwenyekiti, vipaumbele vitakavyozingatiwa katika Mpango wa  Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22 ni pamoja na:  

(i) Miradi ya Kielelezo: Mradi wa Kufua Umeme wa Maji – Julius Nyerere MW  2,115; Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL); Ujenzi wa Reli ya Kati kwa  kiwango cha kimataifa (Standard Gauge); Makaa ya Mawe – Mchuchuma na  Chuma – Liganga ikijumuisha ujenzi wa reli ya kiwango cha Kimataifa (Standard  Gauge Railway – SGR) kutoka Mtwara hadi Mbambabay na matawi ya  Mchuchuma na Liganga; Bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi  Tanga (Tanzania); Mradi wa Kuchakata Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) – Lindi;  Mradi wa Kufua Umeme wa Maji – Ruhudji MW 358; Mradi wa Kufua Umeme wa  Maji – Rumakali MW 222; Uchimbaji wa madini ya Nickel; Ujenzi wa Madaraja  Makubwa na Barabara za Juu za Daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza), Tanzanite  (Dar es Salaam) na Interchange ya Kamata (Dar es Salaam); Bandari ya Uvuvi  (Mbegani) na Ununuzi wa Meli za Uvuvi; Kiwanda cha Sukari Mkulazi; Utafutaji wa  mafuta katika vitalu vya Eyasi Wembere na Mnazi Bay North; Mradi wa Magadi  Soda – Engaruka; Kuongeza Rasilimali Watu yenye Ujuzi Adimu na Maalum (Ujuzi  wa Kati na Wabobezi) kwa Maendeleo ya Viwanda na Ustawi wa Jamii; Kanda  Maalum za Kiuchumi; 

(ii) Kuchochea Uchumi Shindani na Shirikishi: ukarabati wa njia kuu ya reli ya  kati; ununuzi wa injini na mabehewa; ujenzi wa barabara za kufungua fursa za  kiuchumi, kuunganisha nchi jirani, kuondoa msongamano mijini na kuboresha  barabara za vijijini; ujenzi wa madaraja makubwa ikiwemo madaraja ya New  Wami (Pwani), Kitengule (Kagera), Kirumi (Mara) na Mkenda (Ruvuma); ujenzi na  ukarabati wa meli kwenye maziwa makuu ikijumuisha MV Mwanza Hapa Kazi Tu,  MV Liemba na MV Umoja; uboreshaji wa bandari za Dar es Salaam, Tanga,  Mtwara na bandari za maziwa makuu; miradi ya uzalishaji, usafirishaji na  usambazaji umeme mijini na vijijini; mapinduzi ya TEHAMA ikijumuisha mradi wa  mkongo wa Taifa wa mawasiliano na kutekeleza mradi wa Tanzania ya Kidigitali; 

(iii) Kuimarisha Uwezo wa Uzalishaji Viwandani na Utoaji Huduma:  Kuendeleza viwanda vinavyolenga kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao ya  kilimo, mifugo, uvuvi na madini pamoja na kuzalisha bidhaa zitakazotumia  malighafi na rasilimali zinazopatikana nchini. Miradi hiyo ni pamoja na: miradi ya  kuongeza tija kwenye kilimo ikiwemo tafiti za mbegu bora, miundombinu ya  umwagiliaji, masoko ya bidhaa za kilimo, huduma za ugani, zana za kilimo, tiba  na udhibiti wa magonjwa ya mifugo; viwanda vya kuongeza thamani ya madini  ikiwemo kiwanda cha kuchenjua dhahabu – Mwanza; na kufufua Shirika la Uvuvi  (TAFICO). Aidha, eneo hili linajumuisha pia miradi na programu inayolenga  kuboresha sekta ya utalii, huduma za fedha na bima;  

(iv) Kukuza Biashara na Uwekezaji: Eneo hili linajumuisha miradi ya kuboresha  mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji ikiwemo kuendelea kutekeleza  Mpango wa Kuboresha Biashara na Uwekezaji (Blueprint) kwa: kutekeleza miradi  ya kuimarisha mifumo ya kitaasisi ili kuchochea biashara na uwekezaji; kuanzisha  vituo vya kutoa huduma pamoja kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa;  kurekebisha sheria na kanuni zinazokinzana; na kuboresha na kuunganisha 

mifumo ya TEHAMA katika mamlaka za udhibiti. Kwa upande wa uboreshaji wa  masoko, miradi itakayotekelezwa inajumuisha: uendelezaji wa masoko ya bidhaa;  kuboresha mifumo ya taarifa za Soko la ajira ili kuwezesha ukusanyaji, uchambuzi  na utoaji wa taarifa; na kuimarisha udhibiti wa viwango vya ubora wa bidhaa; 

(v) Kuchochea Maendeleo ya Watu: miradi itakayotekelezwa inajumuisha:  kuimarisha miundombinu ya Hospitali ya Taifa Muhimbili; uboreshaji wa hosptitali  za rufaa za kanda na za mikoa, halmashauri, vituo vya afya na zanahati; ununuzi  na usambazaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi; kuimarisha huduma za  tiba asili na tiba mbadala; kuendelea na udhibiti wa magonjwa yasiyoambukizwa;  kuendelea na utoaji wa elimumsingi bila ada; kuendelea na utoaji wa mikopo kwa  wanafunzi wa elimu ya juu; kuendelea na uboreshaji wa miundombinu ya  kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote za elimu ikijumuisha vyuo vya mafunzo  ya ualimu; kuendelea kuboresha miundombinu na huduma za maji safi na maji  taka mijini na vijijini; kuendelea na kupanga, kipima na kumilikisha ardhi mijini na  vijijini; kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji; na kuendelea na utekelezaji  wa programu za kulinda mazingira na kuhimili mabadiliko ya tabianchi; na 

(vi) Kuendeleza Rasilimali Watu: Eneo hili linajumuisha programu na mikakati  inayolenga kuendeleza maarifa na ujuzi wa rasimali watu nchini. Miradi  itakayotekelezwa ni pamoja na: kuboresha miundombinu ya kufundishia na  kujifunzia katika taasisi za mafunzo ya ufundi na vyuo vya mafunzo ya ufundi  stadi; kufanya mapitio ya mitaala inayotumika katika taasisi za mafunzo ya ufundi  na vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira; kukuza  ujuzi na uhawilishaji wa teknolojia; kuendeleza wabunifu ili kuongeza matumizi ya  ubunifu katika mifumo rasmi ya uchumi na viwanda kwa maendeleo na ushindani  wa kibiashara; kujenga uwezo wa vikundi na kampuni za ndani ili ziweze kufaidika  na fursa za zabuni za ndani; na kutambua na kuainisha teknolojia mbalimbali. 

SEHEMU YA TATU 

TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI KATIKA KIPINDI CHA JULAI 2020  HADI JANUARI 2021 NA MAPENDEKEZO YA KIWANGO CHA UKOMO  WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2021/22 

  1. TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI KATIKA KIPINDI CHA JULAI  2020 HADI JANUARI 2021 
  2. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2020/21, Serikali ilipanga kukusanya  jumla ya shilingi trilioni 34.9 ikijumuisha: mapato ya ndani ya shilingi trilioni 24.1;  misaada na mikopo nafuu shilingi trilioni 2.9; mikopo ya ndani shilingi trilioni 4.9; na  mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara shilingi trilioni 3.0. Aidha, Serikali ilipanga  kutumia shilingi trilioni 34.9 ambapo shilingi trilioni 22.1 ni kwa ajili ya matumizi ya  kawaida na shilingi trilioni 12.8 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.  
  3. Mheshimiwa Mwenyekiti, makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa  mwaka 2020/21, yaliandaliwa kwa kuzingatia misingi (assumptions) pamoja na shabaha  mahususi za uchumi ujumla. Mafanikio yaliyopatikana katika shabaha za uchumi jumla ni 

10 

kama ifuatavyo: Pato la Taifa lilikuwa kwa wastani wa asilimia 4.7 kati ya Januari hadi  Septemba 2020, ikilinganishwa na lengo la mwaka la asilimia 5.5; mfumuko wa bei  ulikuwa asilimia 3.3. mwaka 2020 ikiwa ni ndani ya lengo la kutozidi asilimia 5; akiba ya  fedha za kigeni ilitosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi  kisichopungua miezi 5.6 ikiwa ni zaidi ya lengo la miezi minne (4); na nakisi ya bajeti  inatarajiwa kutozidi asilimia 3 ya Pato la Taifa kwa mwaka 2020/21. 

  1. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021,  Serikali ilikusanya jumla ya shilingi trilioni 17.1 kutoka vyanzo vyote vya ndani na nje,  sawa na asilimia 87.7 ya makadirio ya shilingi trilioni 19.5. Mapato ya ndani yakijumuisha  mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa yalifikia shilingi trilioni 12.0, sawa na asilimia  87.9 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 13.7. Kati ya mapato hayo: mapato  yaliyokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yalikuwa shilingi trilioni 10.4,  sawa na asilimia 88.3 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 11.7; mapato yasiyo ya kodi  kutoka Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala na Taasisi za Serikali yalikuwa shilingi  trilioni 1.2, sawa na asilimia 83.2 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 1.5; na mapato ya  Mamlaka ya Serikali za Mitaa yalifikia shilingi bilioni 462.5, ikiwa ni asilimia 93.1 ya  lengo la kukusanya shilingi bilioni 496.7. Aidha, Desemba 2020, Mamlaka ya Mapato  iliweza kukusanya kiasi cha juu ambacho hakijawahi kufikiwa katika historia cha shilingi  trilioni 2.1. 
  2. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2020/21, Bunge liliidhinisha  mapendekezo ya Serikali ya kuboresha sera za mapato kwa lengo la kupanua wigo wa  kodi pamoja na kuendeleza na kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara.  Marekebisho hayo ya mfumo wa kodi yalitarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa  shilingi milioni 3,504.2. Katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2020, mapato halisi  yaliyotokana na vyanzo hivyo vipya yalifika shilingi milioni 1,440.1, ikiwa ni ufanisi wa  asilimia 82.2 ya lengo la kukusanya shilingi milioni 1,752.1 kwa kipindi hicho. Hatua  nyingine zilizochukuliwa zililenga kuboresha mazingira ya Biashara na uwekezaji kwa  kufuta ama kupunguza kodi na tozo mbalimbali, pamoja na kuwa hatua hizo zilipunguza  mapato kwa ujumla wake. 
  3. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha malengo ya ukusanyaji wa  mapato yanafikiwa, Serikali itaendelea kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa sheria,  kanuni na taratibu za kodi; Kuboresha mifumo ya TEHAMA ya kukusanya kodi na  maduhuli, ikiwemo Electronic Fiscal Device Management System (EFDMS) ambao  hupokea na kutunza kumbukumbu za utoaji wa risiti za mauzo. kuimarisha mifumo ya  usimamizi na ufuatiliaji wa makusanyo ya mapato kwa kutoa elimu ya kodi na umuhimu  wa kutoa na kudai risiti ili kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari; kuimarisha ushirikiano  miongoni mwa mamlaka zinazokusanya mapato ya Serikali na vyombo vya ulinzi na  usalama ili kudhibiti biashara za magendo; kukasimisha jukumu la kukusanya kodi ya  majengo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa; kufanya mapitio ya mfumo wa mapato na  matumizi ya Serikali ili kuwa na bajeti endelevu; na kukamilisha uanzishwaji wa ofisi ya  msuluhishi wa masuala ya kikodi (Tax Ombudsman) ili kushughulikia malalamiko ya  walipakodi nje ya Mahakama.

11 

  1. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inakamilisha utafiti kuhusu visababishi  muhimu vya kiwango cha chini cha uhiari wa walipakodi kusajili biashara zao, ulipaji wa  kodi kwa wakati na uwazi katika utoaji wa taarifa sahihi kuhusu biashara wanazofanya,  hususan kwa wafanyabiashara wadogo. Utafiti huu unahusisha kuchunguza changamoto  za kitaasisi, tabia sababishi na hatua zinazopaswa kuchukuliwa. Aidha, Mamlaka ya  Mapato Tanzania inatekeleza mradi wa kujirejeshea kutoka kwa mawakala jukumu la  kusimamia EFD ili kuongeza ufanisi katika usambazaji wa mashine za EFD pamoja na  utoaji wa huduma za kiufundi pindi mashine hizo zinapopata hitilafu. Vile vile, Serikali  inafanya mapitio ya mfumo wa mapato na matumizi kwa lengo la kuwezesha upatikanaji  wa mapato yatakayokidhi ugharamiaji wa mahitaji ya Serikali na hivyo kuwa na bajeti  endelevu. 
  2. Mheshimiwa Mwenyekiti, Washirika wa Maendeleo walitoa jumla ya shilingi  trilioni 1.4 sawa na asilimia 82.4 ya makadirio ya shilingi trilioni 1.7. Kati ya kiasi  kilichotolewa, mikopo nafuu ya kibajeti ilikuwa shilingi bilioni 150.9, miradi ya maendeleo  ilikuwa shilingi trilioni 1.1 sawa na asilimia 75.1 ya makadirio kwa kipindi hicho na mifuko  ya kisekta ilipokea shilingi bilioni 149.0 sawa na asilimia 62.9 ya makadirio. 
  3. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021,  Serikali ilipanga kukopa katika soko la ndani jumla ya shilingi trilioni 3.0. Katika kipindi  hicho, shilingi trilioni 2.7 zilipatikana, sawa na asilimia 88.7 ya lengo. Kati ya kiasi  kilichokopwa, shilingi trilioni 1.7 zimetumika kulipia mikopo ya ndani iliyoiva na shilingi  bilioni 988.9 zimetumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo. Serikali  inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali kuhakikisha kuwa kiasi kilichopangwa  kukopwa katika soko la ndani kinapatikana. Mikakati hiyo ni pamoja na kutoa elimu zaidi  kwa wananchi na wadau wengine ili waweze kuwekeza katika hatifungani na dhamana  za Serikali. 
  4. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilipanga kukopa kiasi cha shilingi trilioni 3.0  kutoka vyanzo vyenye masharti ya kibiashara. Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari  2021, Serikali imefanikiwa kukopa kiasi cha shilingi trilioni 1.1 sawa na dola za Marekani  milioni 463.8 kutoka Standard Chartered Bank (SCB) kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa  reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa. Aidha, Serikali inaendelea na majadiliano ili  kukamilisha upatikanaji wa mkopo kutoka Benki ya Credit Suisse AG (Dola za Marekani  milioni 200) kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa miundombinu mbalimbali. Vilevile,  majadiliano na benki mbalimbali yanaendelea ili kukopa kiasi chote kilichopangwa  kwenye bajeti ya mwaka 2020/21. Mikopo hii inachelewa kupatikana kutokana na  majadiliano kuchukua muda mrefu hususan kutokana na masharti magumu ya mikopo  hiyo. 
  5. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa matumizi, ridhaa ya matumizi  iliyotolewa katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021, ilikuwa shilingi trilioni 16.7,  sawa na asilimia 86.7 ya lengo. Kati ya kiasi kilichotolewa, shilingi trilioni 12.1 ni fedha za  matumizi ya kawaida, sawa na asilimia 93.7 ya lengo na shilingi trilioni 4.7 ni fedha za  maendeleo, sawa na asilimia 74.1 ya lengo. Fedha za matumizi ya kawaida zilizotolewa  zinajumuisha: shilingi trilioni 4.4 kwa ajili ya mishahara, sawa na asilimia 97.6 ya lengo;  shilingi trilioni 4.5 kwa ajili ya kugharamia deni la Serikali, sawa na asilimia 89.4 ya 

12 

lengo; na shilingi trilioni 3.2 kwa ajili ya matumizi mengineyo, sawa na asilimia 96.3 ya  lengo. Aidha, fedha za maendeleo zilizotolewa zinajumuisha shilingi trilioni 3.4 fedha za  ndani na shilingi trilioni 1.2 fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Vile vile, kiasi  cha shilingi bilioni 402.2 ni fedha ambazo zimetengwa mahsusi kwa ajili ya kugharamia  utekelezaji wa miradi mikubwa baada ya kukamilishwa kwa uhakiki wa hati za madai  pamoja na hati mpya za madai zitakazowasilishwa. 

  1. Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji  wa sera za matumizi katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021 ni kuelekeza  rasilimali fedha kwenye maeneo yaliyolindwa, yasiyoepukika pamoja na vipaumbele  vinavyochochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi. Maeneo hayo ni pamoja na: kulipa Deni  la Serikali, ambapo jumla ya shilingi trilioni 4.5 zilitolewa; kulipa mishahara ya watumishi  kwa wakati, ambapo shilingi trilioni 4.4 zilitolewa; kugharamia shughuli za uendeshaji wa  Serikali, ambapo jumla ya shilingi trilioni 3.2 zilitolewa; kugharamia kwa mara ya kwanza  Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kwa kutumia fedha za ndani, ambapo jumla ya shilingi  bilioni 268.5 zilitumika; ulipaji wa madeni yaliyohakikiwa ya shilingi bilioni 340.0, ambapo  kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 52.1 ni madai ya watumishi ya kimshahara na yasiyo ya  kimshahara, shilingi bilioni 21.7 ni madai ya wazabuni, shilingi bilioni 201.3 makandarasi,  shilingi bilioni 32.0 watoa huduma na shilingi bilioni 32.9 ni madai mengineyo;  kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, uimarishaji wa vyuo vya ufundi stadi  (VETA) na kukuza ujuzi kwa vijana ambapo shilingi bilioni 248.5 zilitolewa; na  kugharamia elimumsingi bila ada ambapo shilingi bilioni 145.6 zilitolewa. Aidha, Serikali  imeendelea kusimamia nidhamu ya matumizi, kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima na kuongeza kasi ya matumizi ya TEHAMA katika usimamizi wa matumizi ya Serikali. 
  2. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Februari hadi Juni 2021, mapato  ya ndani yanatarajiwa kufikia lengo la mwaka kwa kutekeleza mikakati mbalimbali ya  kuimarisha usimamizi na kuhimiza matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji  wa mapato. Misaada na mikopo nafuu kutoka nje inatarajiwa kufikia lengo kwa  kuimarisha ushirikiano na Washirika wa Maendeleo kwa kutekeleza Mpango Kazi wa  Mwongozo wa Ushirikiano (Development Cooperation Framework – DCF); na Mikopo ya  ndani na nje yenye masharti ya kibiashara inategemewa kufikia lengo la bajeti. Aidha,  katika kipindi cha Februari hadi Juni 2021, Serikali itaendelea kupeleka fedha kwenye  Mafungu kwa kuwianisha mapato na matumizi ikiwa ni pamoja na kutoa kipaumbele kwa  mahitaji yasiyoepukika kama vile ugharamiaji wa deni la Serikali, ulipaji wa mishahara ya  watumishi, uendeshaji wa ofisi na utekelezaji wa miradi muhimu yenye maslahi mapana  kwa Taifa. 
  3. MAPENDEKEZO YA KIWANGO CHA UKOMO WA BAJETI YA SERIKALI  KWA MWAKA 2021/22 

Sera za Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2021/22 

  1. Mheshimiwa Mwenyekiti, sera za mapato na hatua za kiutawala kwa mwaka  2021/22 zitalenga: kutoa kipaumbele katika utekelezaji wa mikakati na miradi ya  kuongeza mapato; kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa  kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA; kuimarisha usimamizi wa sheria za 

13 

kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato;  kuboresha mazingira ya ulipaji kodi kwa hiari na upanuzi wa wigo wa kodi; kuendelea  kutekeleza Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo Tanzania; na kuendelea kukopa  kutoka katika vyanzo vyenye masharti nafuu, hususan kwa utaratibu wa Export Credit  Agency (ECA). 

  1. Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika mwaka 2021/22, Serikali itaendelea  kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma ili kupunguza matumizi yasiyo ya  lazima, kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuelekeza rasilimali fedha  kwenye miradi ya kielelezo na kimkakati. Aidha, Serikali itaendelea kuhakiki, kulipa na  kuzuia ongezeko la malimbikizo ya madai kwa Serikali. Hivyo, Sera za matumizi kwa  mwaka 2021/22 zitajumuisha yafuatayo: kuelekeza fedha kwenye maeneo ya  kipaumbele yatakayochochea ukuaji wa uchumi na kuhakikisha kuwa miradi  inayoendelea inapewa kipaumbele kabla ya miradi mipya; kuhakikisha kuwa nakisi ya  bajeti haizidi asilimia 3.0 ya Pato la Taifa; kudhibiti ulimbikizaji wa madai; kuendeleza  nidhamu ya matumizi ya fedha za umma; na kuongeza matumizi ya TEHAMA katika  shughuli za Serikali ili kuongeza ufanisi ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo wa wataalamu  wa ndani kwenye eneo la usalama wa mifumo. 

Kiwango cha Ukomo wa Bajeti kwa Mwaka 2021/22 

  1. Mheshimiwa Mwenyekiti, uandaaji wa Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya  Serikali katika kipindi cha mwaka 2021/22 umejengwa katika misingi (assumptions)  ifuatayo:  

(i) Kuendelea kuwepo kwa amani, usalama, umoja, utulivu wa ndani na nchi  jirani;  

(ii) Kuhimili athari za majanga ya asili;  

(iii) Ushiriki mpana wa sekta binafsi;  

(iv) Hali nzuri ya hewa itakayowezesha uzalishaji wa chakula cha ziada; na  (v) Kuimarika kwa uchumi wa dunia na utulivu wa bei katika masoko ya  kimataifa. 

  1. Mheshimiwa Mwenyekiti, malengo na shabha za uchumi jumla ni kama  ifuatavyo: 

(i) Ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 6.0 mwaka 2021 na asilimia 6.3  ifikapo mwaka 2023; 

(ii) Kuhakikisha kuwa mfumuko wa bei unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja  ya wastani wa asilimia kati ya 3.0 – 5.0 katika muda wa kati; 

(iii) Mapato ya ndani kufikia asilimia 15.9 ya Pato la Taifa mwaka 2021/22 na  asilimia 16.3 ya Pato la Taifa mwaka 2023/24; 

(iv) Mapato ya kodi kufikia asilimia 13.5 ya Pato la Taifa mwaka 2021/22 kutoka  matarajio ya asilimia 12.9 mwaka 2020/21; 

(v) Kuhakikisha nakisi ya bajeti haizidi asilimia 3.0; na 

(vi) Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya  uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi  minne (4).

14 

  1. Mheshimiwa Mwenyekiti, shabaha za uchumi jumla zimeandaliwa kwa  kuzingatia hali halisi ya uchumi wa Tanzania na ulinganisho wa chumi nyingine duniani,  hususan kusini mwa Jangwa la Sahara. Wastani wa mapato ya ndani kwa nchi za kusini  mwa Jangwa la Sahara ni asilimia 14.5 ya Pato la Taifa, nakisi ya bajeti ni wastani wa  asilimia 7.6 na wastani wa mfumuko wa bei ni asilimia 10.5.  
  2. Mheshimiwa Mwenyekiti, vigezo vilivyotumika katika uandaaji wa kiwango cha ukomo wa bajeti za matumizi za Mafungu ni pamoja na: miradi inayoendelea; matumizi  yaliyolindwa; vibali vya miradi mipya; miradi yenye vyanzo maalumu; vibali vya ajira  mpya na upandishwaji wa madaraja kwa watumishi; matumizi yasiyojirudia; na mahitaji  ya Mamlaka za Uhifadhi zilizoathiriwa na kushuka kwa biashara katika sekta ya utalii. 
  3. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwa, yapo mafungu yenye  vyanzo maalum yenye mahitaji makubwa ikilinganishwa na uwezo wa kibajeti kwa sasa  kama vile barabara na maji vijijini (TARURA NA RUWASA). Ili kukabiliana na upungufu  uliopo, Serikali inafanya tathmini ya utendaji wa taasisi zinazosimamia maeneo hayo ili  kuongeza tija na kuangalia uwezekano wa kuwa na bajeti endelevu ya maeneo hayo.  Aidha, Serikali ipo katika majadiliano na Benki ya Dunia ili kuwezesha upatikanaji wa  mkopo nafuu wa dola za Marekani milioni 300 kwa ajili ya kugharamia ujenzi na  matengenezo ya miradi ya barabara za TANROADS na TARURA.  
  4. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia sera, misingi na vigezo vya ukomo,  jumla ya shilingi trilioni 36.3 zinatarajiwa kukusanywa kwa mwaka 2021/22, ikiwa ni  sawa na ongezeko la asilimia 4.0 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2020/21. Kati ya  mapato hayo: mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 26.0, sawa na asilimia  71.8 ya bajeti yote; misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo  shilingi trilioni 2.9; mikopo ya ndani shilingi trilioni 5.0; na mikopo ya nje yenye masharti  ya kibiashara shilingi trilioni 2.4. 
  5. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2020/21, Serikali inapanga kutumia  jumla ya shilingi trilioni 36.3 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo,  shilingi trilioni 23.0 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikiwa ni asilimia 63 ya  bajeti yote na shilingi trilioni 13.3 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo, sawa na  asilimia 37 ya bajeti yote. Bajeti ya maendeleo inajumuisha shilingi trilioni 10.4 fedha za  ndani, sawa na asilimia 78.2 ya bajeti ya maendeleo na shilingi trilioni 2.9 fedha za nje,  sawa na asilimia 21.8 ya bajeti ya maendeleo. Aidha, shilingi, trilioni 10.7 sawa na  asilimia 29.5 ya Bajeti yote zimetengwa kwa ajili ya kulipa fedha zilizokopwa kugharamia  utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo imekamilika na inayoendelea. Fedha hizo  zilitengwa kwenye kasma za Matumizi ya Kawaida lakini kimsingi sio za kulipa mishahara  wala posho. 
  6. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia maelezo hayo, kiwango cha ukomo  wa bajeti kwa mwaka 2021/22 ni kama ilivyo katika Jedwali lifuatalo:

15 

Mapendekezo ya Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka  2021/22 

Shilingi Milioni 

Mapato 2021/22 A. Mapato ya Ndani-Serikali Kuu 25,168,718 (i) Mapato ya Kodi (TRA) 22,097,676 (ii) Mapato yasiyo ya kodi 3,071,042 B. Mapato ya Halmashauri 863,858 C. Misaada na Mikopo nafuu kutoka Washirika wa Maendeleo 2,884,990 (i) Misaada na Mikopo nafuu – GBS * 0 (ii)Misaada na Mikopo nafuu ya Miradi 2,602,684 (iii)Misaada na Mikopo nafuu ya Kisekta 282,306 D. Mikopo ya Ndani na Nje 7,341,240 (i) Mikopo ya Nje 2,352,107 (ii) Mikopo ya Ndani 1,838,796 (iii)Mikopo ya Ndani- Rollover 3,150,337 JUMLA YA MAPATO YOTE (A+B+C+D) 36,258,806 

Matumizi 

  1. Matumizi ya Kawaida 23,002,951 

o/w (i) Mfuko Mkuu wa Serikali 10,663,278  -Malipo ya Riba Ndani 1,561,637  -Malipo ya Mtaji Ndani (Rollover) 3,150,337  -Malipo ya Mtaji Nje 3,015,070  – Malipo ya Riba Nje 1,151,376  – Michango ya Serikali kwenye Mifuko ya Hifadhi za Jamii 1,247,149  -Matumizi Mengine ya Mfuko Mkuu 537,710  (ii) Mishahara 8,150,509  (iii)Matumizi Mengineyo (OC) 3,944,164  – Malipo ya Madeni yaliyohakikiwa 200,000  – Matumizi ya Halmashauri (own source) 532,768  – Matumizi mengineyo 3,211,396  (iv) Mahitaji ya TANAPA, NCAA na TAWA 0 245,000 

  1. Matumizi ya Maendeleo 13,255,855 (i) Fedha za Ndani 10,370,865  o/w Malipo ya Madeni yaliyohakikiwa 400,000  o/w Ugharamiaji wa SGR 1,174,246  o/w Ugharamiaji wa Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere 1,440,000  o/w Matumizi ya Halmashauri 331,090  o/w Miradi mingine 7,025,529 (ii) Fedha za Nje 2,884,990 JUMLA YA MATUMIZI YOTE (E+F) 36,258,806 NAKISI YA BAJETI (ASILIMIA YA PATO LA TAIFA) 1.8% Chanzo: Wizara ya Fedha na Mipango

16 

HITIMISHO 

  1. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutekeleza hatua mbalimbali za  kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi, kugharamia  mahitaji yasiyoepukika kama vile ugharamiaji wa miradi ya kipaumbele na kimkakati,  deni la Serikali, mishahara ya watumishi, mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu,  elimumsingi bila ada na uendeshaji wa ofisi. Aidha, Serikali itaendelea kusimamia  nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti, SURA 439,  Sheria ya Fedha za Umma, SURA 348, Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, SURA 290 na  Sheria ya Ununuzi wa Umma, SURA 410. Lengo ni kupunguza matumizi yasiyo ya lazima  na kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma. Vile vile, Serikali itaendelea kuhakiki,  kulipa na kuzuia ongezeko la malimbikizo ya madai kwa Serikali. 
  2. Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa  Mwaka 2021/22 pamoja na Bajeti ya mwaka 2021/22, unatarajiwa kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi, upatikanaji wa huduma za kijamii, kuongeza fursa za ajira na  maendeleo ya watu na nchi kwa ujumla. 
  3. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.

 

No comments :

Post a Comment