*********************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
WADAU wa madini ya
Tanzanite wa kikundi cha Muungano na Mara Group wa Mji mdogo wa Mirerani
Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wameiomba Serikali kuwapiga picha na
kuwazuia kuingia watu watakaokamatwa wakitorosha madini ndani ya ukuta
unaozunguka migodi ya madini hayo.
Wadau hao waliyasema
hayo kwenye mkutano wa kutoa elimu kwa jamii juu ya kupiga vita
utoroshaji wa madini kilichofanyika Mji mdogo wa Mirerani.
Mwenyekiti wa Mara
Group, Godwin Kosodo amesema kila mmoja atimize wajibu wake na mtu
akikamatwa na madini achukuliwe hatua kwa kuzuiwa kuingia tena ndani ya
ukuta unaozunguka migodi ya Tanzanite.
“Watu wa Mara ni
jamii kubwa akichafuka mmoja tunachafuka wote, hata wakikamatwa wengine
hawatajwi kama tunavyotajwa sisi, hivyo hata mmoja akikamatwa anatorosha
tunachanganywa wote, tuepuke hayo,” amesema Kosodo.
Askofu wa kanisa la
Roho Mtakatifu, Boaz Ambonya ambaye pia ni Mwenyekiti wa mtaa wa
Manyara, amesema upekuzi wa kuvuliwa nguo unafanyika kutokana na watu
wachache kushiriki wizi huo.
“Watu wanakuwa na
watoto wao, kaka zao, baba zao, kisha wanapekuliwa uchi kwa sababu ya
watu wachache, elimu inatolewa ila izidi kutolewa ili watu wawe
waaminifu,” amesema Ambonya.
Mchuuzi wa madini
hayo, Gerald Orinyo alisema mtu mmoja akikamatwa kutorosha asisababishe
kuchafua jamii nzima ya Mara na kuonekana wote wanahusika na utoroshaji
wa madini.
“Ni bora akapigwa
picha na kuzuiliwa kuingia ndani ya ukuta kwani kuna baadhi ya watu
wanawarubuni vijana wanatorosha madini badala ya kulipa kodi,” amesema
Orinyo.
Hata hivyo, kaimu
ofisa madini mkazi wa Mirerani, Ezra Gregory alisema amepokea
mapendekezo hayo na atayafikisha kwa kiongozi wao Fabian Mshai.
“Sheria ipo wazi kuwa
anayekamatwa akitorosha madini haruhusiwi kuingia ndani ya ukuta ila
hawa waliokamatwa wanaomba msamaha Kisha wanaruhusiwa ila tutalifikisha
kwa uongozi lifanyiwe kazi,” amesema Ezra.
No comments :
Post a Comment