Wednesday, March 31, 2021

Soma zaidi...... SHAMIMU MWASHA NA MUMEWE GEREZANI MAISHA, GARI LAO KUTAIFISHWA

Mmiliki wa Blog ya 8020 Fashion, Shamimu Mwasha akitoka katika chumba cha Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mara baada ya kuhukumiwa kifungo cha misha Jela leo Machi 31.
Mfanyabiashara Abdul Nsembo (45) akiwa katika Mahabusu ya Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu kama mahakama ya mafisadi leo mara baada ya Kuhukumiwa Kifungo cha Maisha jela.

Gari aina ya Land Rover Discover, T 817 DQN walilokutwa nalo washtakiwa na Shamimu na Mumewe limeamuliwa litaifishwe na kuwa mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii
MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu kama mahakama ya mafisadi, imemuhukumu Shamim Mwasha (41), na mume wake, Abdul Nsembo (45), kutumikia kifungo cha maisha gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha na kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya aina ya Heroine zenye uzito wa gramu 232.70.

Aidha, Mahakama hiyo imeamuru kutaifishwa kwa gari aina ya Land Rover Discover, T 817 DQN kuwa mali ya serikali na pia dawa za kulevya walizokutwa nazo Mwasha na Nsembo kuteketezwa.

Hukumu hiyo imesomwa leo Machi 31, 2021 na Jaji Elinaza Luvanda baada ya kuridhika na ushahidi wa mashahidi sita wa upande wa mashtaka walioweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka Shamimu na mume wake walitenda makosa hayo.

Akisoma hukumu hiyo Jaji Luvanda amesema, amepitia ushahidi wote wa upande wa mashtaka na ule wa utetezi pamoja na hoja mbalimbali zilizowasilishwa na imeonyesha kuwa, hakuna shaka kuwa vielelezo vyote vilikutwa nyumbani kwa washtakiwa hivyo washtakiwa wote mmekutwa na hatia, mahakama inawatia hatiani.

Hata hivyo kabla ya kuwasomea adhabu, Jaji Luvanda aliuliza upande wa mashtaka kama walikuwa na lolote la kusema waliomba mahakama itoe adhabu kali kulingana na sheria inavyoagiza kwa sababu kosa walilofanya washtakiwa hao linaleta madhara makubwa kwa jamii ikiwemo utegemezi na upungufu wa afya ya akili.

Katika utetezi wao, washtakiwa kupitia mawakili wao, Juma Nassoro na Hajra Mungula waliomba mahakama kuwapunguzia wateja wao adhabu kwani ni wakosaji wa kwanza na pia ni wanandoa, ni wazazi wa watoto watatu wanaohitaji malezi ya wazazi hivyo mahakama itoe hukumu kwa kuangalia huruma hiyo.

Hata hivyo Jaji Luvanda amesema anatoa hukumu kulingana na matakwa ya sheria, na kwamba kifungu cha sheria cha 15 (1)a cha sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya sura ya 95 walichoshtakiwa nacho washtakiwa hakitoi mwanya wa kutoa adhabu mbadala zaidi ya kutoa kifungo cha maisha tu.

"Ni kweli washtakiwa ni wakosaji wa kwanza lakini sheria inatoa adhabu kwa makosa haya na kwa kuwa sheria haijatoa mwanya kwa mahakama kutoa huruma, ninawahukumu kifungo cha maisha gerezani na pia vielelezo ikiwemo gari aina ya discover waliyokutwa nayo washtakiwa inataifishwa na kuwa mali ya serikali." Amesema Jaji Luvanda.

Aidha upande wa utetezi umeeleza nia yao ya kukata rufaa huku wakiomba wapatiwe nakala ya hukumu haraka kwa ajili ya kuanza maombi ya rufaa hiyo.

Katika kesi hiyo Shamimu ambaye ni mmiliki wa blogu ya 8020 fashion na mumewe mfanyabiashara Abdu Nsembo wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mawili ya kusafirisha na kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya aina ya Heroine zenye uzito wa gramu 232.70 kosa walilolitenda Mei 1, 2020 katika eneo la Mbezi Beach Mkoani Dar es Salaam.

 

No comments :

Post a Comment