Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akizungumza na wananchi wa Namanga (hawapo pichani) wakati wa kupokea mabomba ya mradi wa maji wa Longido-Namanga
Shehena ya mabomba kwa ajili ya mradi wa Longido-Namanga ikipakuliwa kutoka kwenye moja ya lori lililowasili Namanga
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akijadiliana jambo na Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Mhandisi Clement Kivegalo wakati wa ziara yao kwenye mradi wa maji wa Longido-Namanga
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Kimokouwa katika mji wa Namanga wakishuhudia upakuaji wa shehena ya mabomba kwa jili ya mradi wa maji wa Longido-Namanga
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kulia) akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira AUWSA wakati wa upakuaji wa shehena ya mabomba ya mradi wa maji wa Longido-Namanga.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Kimokouwa katika mji wa Namanga waliofika kushuhudia upakuaji wa shehena ya mabomba kwa jili ya mradi wa maji wa Longido-Namanga.
*************************************
Na Mohamed Saif- Arusha
Wananchi wa Kata ya Kimokouwa katika Mji wa Namanga, Mkoani Arusha wameipongeza
Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Maji kwa kuwapelekea mradi wa maji.Wametoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti Machi 14, 2021 mbele ya katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga wakati wa kupokea shehena ya mabomba kwa ajili ya mradi wa maji wa Longido-Namanga.
Mhandisi Sanga alisema ujenzi wa mradi ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwaondolea kero ya maji wananchi wa Namanga.
“Rais Magufuli aliahidi na alituelekeza kuhakikisha wananchi wake wa Namanga wanapata huduma ya maji, nipo hapa kukagua utekelezaji wa maelekezo hayo pamoja na kuona hatua iliyofikiwa,” alisema Mhandisi Sanga.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mwenyekiti wa kitongoji cha Kimokouwa, Losieti Laiser aliipongeza Serikali kwa kuanza kutekeleza ahadi ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
“Serikali ya Awamu ya Tano inafanya kazi kubwa, nimeona inawafanyia mambo makubwa wananchi wake; tunaona kweli sasa hivi Serikali inatekeleza na maji tutapata,” alisema Laiser.
Akielezea adha walionayo, Laiser alisema inawalazimu kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 20 kufuata maji kutoka kwenye chemchem ya Mlima Longido na hivyo aliwasihi wataalam kuhakikisha wanaukamilisha mapema.
Aidha, wananchi hao walimhakikishia Katibu Mkuu Sanga ushirikiano wa kutosha ikiwemo kulinda miundombinu ya mradi pamoja na kuchangamkia fursa zitokanazo na mradi.
Na pia walisisitiza matoleo ya mabomba kwa ajili ya mifugo yao kama walivyoahidiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA), Mhandisi Justine Rujomba wakati akiwasilisha taarifa ya mradi kwa Katibu Mkuu Sanga.
Kwa mujibu wa Mhandisi Rujomba, mradi wa Longido-Namanga unahusisha ulazaji wa mabomba umbali wa kilomita 43 kutoka Longido hadi Namanga na kwamba unatekelezwa na wataalam wa ndani kwa gharama ya shilingi bilioni 4.58 ambayo inalipwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maji.
Alisema mradi unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi 13,000 na kwamba utakuwa na matoleo kwa ajili ya mifugo na wanyamapori na kwamba tayari wamefanya mazungumzo na wataalam wa wanyamapori kuona namna ya kufikisha maji.
Mhandisi Rujomba alisema chanzo cha maji cha mradi huo ni Mto Simba uliopo Wilayani Siha Mkoani Kilimanjaro kwa umbali wa zaidi ya kilomita 100.
Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Sanga aliambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Clement Kivegalo ambaye alibainisha kwamba mradi wa Longido-Namanga unajengwa kwa ushirikiano kati ya AUWSA na RUWASA.
No comments :
Post a Comment