Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu yakamilisha ziara ya siku mbili kukagua Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa Dar es Salaam - Makutupora na
Karakana ya reli mkoani Morogoro, ziara hiyo imefanyika kuanzia Machi 12 - 13, 2021.
Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kufanya tathmini ya
utekelezaji wa bajeti ya miundombinu pamoja na kuweka mikakati ya
kutetea bajeti ya miundombinu katika bunge la bajeti linalotarajiwa
kuanza hivi karibuni.
Aidha, kamati imeridhishwa na utendaji wa
Shirika hususani katika usimamizi wa miradi ukiwemo mradi wa SGR kutoka
Dar es Salaam hadi Makutupora ambapo kwa kipande cha Dar es Salaam -
Morogoro ujenzi wake umefika zaidi ya 90% ukitarajiwa kukamilika Agosti
2021 na kipande cha Morogoro - Makutupora ambacho ujenzi wake umefika
56%, halikadhalika mradi wa ukarabati wa vichwa sogeza 7 ambavyo
vimekamilika tayari kwa ajili ya kuanza kazi.
Aidha, Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kadogosa amesema kuwa
lengo la ziara hiyo ni kwa ajili ya kuona maendeleo ya mradi sambamba na
matumizi ya pesa ambazo zilipitishwa na bunge ili kutekeleza mradi huo.
“Wizara
yetu inahusika kiutendaji na bajeti ya miundombinu, leo tumepata ugeni
huu tunashukuru kwa sababu hiki ni kipindi cha bajeti hivyo wanapokuja
wanapata fursa ya kuona matumizi ya pesa walizopitisha katika bunge la
bajeti lililopita na kuendelea kutetea bajeti ili kuendelea kutekeleza
mradi huu” alisema Kadogosa
Mkurugenzi ameongeza kuwa bado
Shirika linaendelea kusisitiza ushiriki wa wazawa katika mradi ambapo
kwa hivi sasa katika kazi nyingi zinazoendelea wanaofanya na kusimamia
kazi hizo ni wazawa, mfano mzuri ni katika kiwanda cha Mataruma ambacho
wajumbe wameweza kujionea kuwa wafanyakazi wote wanaosimamia kiwanda
hiko ni watanzania.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Miundombinu Mhe. Selemani Kakoso ametoa Shukurani zake kwa Mhe. Rais
Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali kwa kazi kubwa kwa kuwa kazi katika
kipande cha Dodoma – Morogoro kinakwenda vizuri na kuongeza kuwa
wanakamati wana imani kuwa fedha wanazoidhinisha Bungeni zinafanya kazi
kwa ajili ya manufaa ya taifa.
Mhandisi Mwanaisha Ulenge, Mbunge
wa Viti Maalumu mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya
Miundombinu amepongeza Shirika la Reli kwa usimamizi mzuri wa mradi huo
kwa kuzingatia viwango pamoja na utendaji wa kazi za ujenzi katika mradi
huo
No comments :
Post a Comment