Ofisa madini Mkazi
Mkoa wa kimadini wa Mirerani, Fabian Mshai akizungumza kwenye sala na
dua ya kumuombea apumzike kwa amani Rais wa awamu ya tano hayati Dokta
John Magufuli, kwenye maombolezo yaliyofanyika nje ya ukuta unaozunguka
migodi ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro
Mkoani Manyara.
Wadau wa madini ya
Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara,
wakifuatilia sala na dua ya kumuombea apumzike kwa amani Rais wa awamu
ya tano hayati Dokta John Magufuli iliyofanyika pembeni ya ukuta
unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite.
…………………………………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu, Mirerani
UKUTA unaozunguka
migodi ya madini ya Tanzanite uliopo Mji mdogo wa Mirerani Wilayani
Simanjiro Mkoani Manyara, uliojengwa na Rais wa awamu ya tano hayati
John Magufuli, umesababisha kuongeza makusanyo na kukomesha wizi na
utoroshaji wa madini hayo.
Ofisa madini mkazi wa
mkoa wa kimadini wa Mirerani, Fabian Mshai ameyasema hayo Mji mdogo wa
Mirerani kwenye sala na dua ya kumuombea hayati Magufuli kwenye
maombolezo yaliyofanyika kwenye lango la ukuta unaozunguka migodi hiyo.
Mshai amesema awali
kabla ya ukuta huo kujengwa mapato ya madini ya Tanzanite yalikuwa chini
kwani walikuwa wanakusanya shilingi milioni 238 kwa miaka miwili ya
2016 na 2017.
Amesema baada ya
kujengwa ukuta huo na kukamilika mwaka 2018 mapato yakiongezeka na
kufikia shilingi bilioni 1.4 na mwaka 2019 ikafikia shilingi bilioni
2.1.
Amesema hayati
Magufuli atakumbukwa kwa mambo mengi ya maendeleo kwenye sekta ya madini
ndiyo sababu wameungana na wadau wa madini kufanya sala na dua pembeni
ya ukuta huo ili kumuombea apumzike kwa amani.
Ukuta unaozunguka
migodi ya madini ya Tanzanite wenye urefu wa kilomita 24 ulianza
kujengwa mwaka 2017 na kukamilika mwaka 2018 na kugharimu shilingi
bilioni 5.
Ukuta huo uliojengwa
kwa muda wa miezi mitatu na askari wa JKT ulikamilika na kufunguliwa
baada ya miezi sita ya tamko la hayati Magufuli.
Diwani wa Kata ya
Mirerani, Salome Mnyawi amesema hayati Dkt Magufuli alipojenga ukuta huo
amesababisha wanawake wadau wa madini kufanya kazi zao kwa usalama
tofauti na awali.
Katibu wa chama cha
wachimbaji madini Mkoani Manyara MAREMA Tawi la Mirerani, Rachel Njau
amesema hayati Dkt Magufuli ndiye amesababisha mchimbaji mdogo
akatambulika kuwa naye ni mdau wa maendeleo kupitia sekta binafsi.
Diwani wa kata ya
Endiamtu, Lucas Zacharia amesema hayati Dkt Magufuli ndiye amesababisha
yeye akaingia kwenye siasa kipindi akiwa Waziri wa uvuvi.



No comments :
Post a Comment