*************************************************
NA SULEIMAN MSUYA SONGEA
WAZIRI wa Maliasili
na Utalii Dk.Damas Ndumbaro amesema serikali inaendelea kuhamasisha
miradi ya kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu kwa kuwa ina
mchango mkubwa kwenye ukuaji wa pato la taifa.
Dk.Ndumbaro amesema
hayo wakati wa uzinduzi wa mashine ya kuchakata mazao ya misitu
iliyotolewa Shirika la Mpingo na Maendeleo (MCDI), chini ya ufadhili wa
Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC).
Program ya FORVAC inatekelezwa chini ya Idara ya Nyuki na Misitu na kufafhiliwa na Serikali ya Tanzania na Finland.
Amesema kinachofanywa
na FORVAC na MCDI ni sehemu utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Ibara ya 69 kigungu F ambayo inasema kuwepo mashine za kuongeza
thamani mazao ya misitu ili kuleta ajira na kusaidia wananchi.
“Misitu ni sekta
muhimu sana katika nchi kimazingira, kiuchumi, ajira na ukuaji wa
viwanda. Leo tumezindua mashine hii inayochakata tani 5,000 kwa mwaka,
mbao 400 kwa siku ni kiwanda kabisa ambacho kinaongeza ajira, kodi na
pato la taifa kwa ujumla.,” amesema.
Amesema misitu nchini
Tanzania inachukua asilimia 54 ya eneo lote hivyo ikitumiwa kwa
matumizi bora itabadilisha maisha ya wananchi.
Dk.Ndumbaro amesema
ili sekta hiyo kuendelea kuongoza katika uchangiaji wa pato la taifa ni
vema wadau wote kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha taratibu
zinafuatwa kwenye kila hatua muhimu kama FORVAC na MCDI wanafanya.
Amesema kwa sasa
sekta hiyo inachangia pato la taifa kwa asilimia 21 ambapo Utalii
inachangia asilimia 17.5 na misitu asilimia 3.5 hivyo dhana ya mnyororo
wa mazao ya misitu itumike kuongeza mchango zaidi.
Waziri Ndumbaro
amesema miti na misitu ikivunwa kwa mfumo endelevu itachochea maendeleo
hivyo rai yake ni kuona kila wilaya yenye miti inayoweza kuvunwa
kiundelevu ikawa na mashine ya kisasa ya kuchakat mazao ya misitu.
Amesema Serikali
itahakikisha kila mahali kwenye fursa za misitu inatumiwa kuchochea
maendeleo na huduma za kijamii na kuvitaka vijiji kununua mashine za
kuchakata.
Waziri amesema wao kama wizara hawatalala kuhakikisha mchango wao kwa pato la taifa unaongezeka.
“Niwaombe wadau wote
sekta ya misitu tafuteni Sera ya Misitu ya 1998 na Sheria ya Misitu ya
2002 kuhakikisha lengo la sekta hii kuchangia pato la taifa inatimia
bila kuathiri mazingira na maliasili zingine” amesema.
Kwa upande wake
Mratibu wa FORVAC Kitaifa, Emmanuel Msoffe amesema wamesukumwa kutoa
fedha za ununuzi wa mashine hiyo ili usimamizi wa misitu kuwa endelevu
huku ukuaji wa uchumi ukiwepo.
Amesema mashine hiyo
ambayo imegharimu zaidi ya shilingi milioni 100 itatumika katika vijiji
vya Longosi, Lipagalo Liweta, Litoa, Litumbati vya wilaya ya Songea na
vijiji vitano vya wilaya ya namtumbo.
Amesema program hiyo
imekuwa na mafanikio kwa kiwango kikubwa katika hatua zote ila kuna
changamoto ya masoko na kuahidi kuziifanyia kazi.
Mkurugenzi Mkuu wa
MCDI, Makala Gasper amesema wamekuwa wakijishughulisha na uhifadhi wa
misitu kwa kushirikiana na Serikali katika kila ngazi jambo ambalo
linachangia mafanikio.
Amesema mashine hizo
zina mchango mkubwa kwenye kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya
misitu ambapo hadi sasa vijiji 61 vimenufaika na kukusanya zaidi ya
shilingi bilioni 2 zinazotumika kwa miradi yaayaaendeleo.
“Tupo katika vijiji
61 wilaya 9 na mikoa 4 ambapo kuna mabadiliko makubwa katika kukuza
kipato cha wanavijiji, kuboresha na kujenga huduma za jamii, ajira
kupatikana na manufaa mengine mengi,” amesema.
Anasema maratajio yao
ni kuhakikisha jamii inayojihusisha na Usimamizi Shirikishi wa Misitu
ya Jamii (USMJ) inanufaika pamoja na Serikali.
No comments :
Post a Comment