Tuesday, February 9, 2021

Waziri Jafo aziagiza Halmashauri zote nchini Kutenga Maeneo ya Michezo


Na Shamimu Nyaki – WHUSM, DODOMA
Waziri wa Nchi Ofisi  ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo ametoa agizo kwa Halmashauri zote  nchini kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za michezo, huku akiagiza Wakurugenzi katika halmashauri hizo kusimamia vyema miundombinu ya michezo na kuhakikisha maeneo ya michezo hayavamiwi.


Mhe. Jafo ameyasema hayo leo Februari 08, 2021 jijini Dodoma katika kikao kati ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kilichoandaliwa na Wizara ya Habari ambacho kilijadili namna ya kuboresha Michezo katika shule za msingi na Sekondari.


“Nawaagiza walimu wakuu wa shule zote nchini, kusimamia vyema vipindi vya michezo kwa kuhakikisha vinafundishwa katika muda sahihi na wanafunzi wanashiriki vyema vipindi hivyo. Na sisi upande wa Serikali tutasimamia vyema ajenda hiyo na tutahakikisha maafisa elimu Mkoa na Wilaya wanafuatilia michezo katika maeneo yao kwakua tunataka Tanzania iwe na wanamichezo wazuri wa kuisaidia nchi yetu” alisema Mhe. Jafo


Kwa upande wake Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako   amesema kuwa Wizara yake itahakikisha inaandaaa na kuhuisha Mitaala iliyopo kuhusu somo la michezo ili somo hilo lilete tija kwa Taifa kwa kuzalisha wataalamu wengi wa fani hiyo.


“Kwakua tunafahamu Michezo ni ajira na inajenga afya, ni jukumu letu kuhakikisha  tunaisimamia vyema na tayari katika shule za msingi kuna somo linaitwa Haiba na Michezo na katika shule za sekondari kuna somo linaitwa Elimu kwa njia ya Michezo (Physical Education), masomo hayo yanatengeneza wataalamu katika  sekta hiyo” alisema Mhe. Joyce.


Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa mbali na kuzishukuru Wizara hizo kushiriki na kutoa mawazo chanya yanayolenga kuboresha maendeleo ya michezo nchini, amesema dhamira ya Serikali ni kuleta uhai katika timu za Taifa na uhai huo unatokana na kuwepo kwa vipaji vinavyozalishwa kuanzia shule za msingi na sekondari.


“Sera ya Michezo ya mwaka 1995 ilikua imekosa Mpango Mkakati wa kuitekeleza vyema, na tayari rasimu ya mpango huo ipo, lengo la kikao hiki ni muendelezo wa  utekelezaji wa vikao mbalimbali vya  kuboresha sekta hii kwa kushirikiana na wizara hizi tatu” alisema Mhe. Bashungwa.


Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Habari Mhe. Abdallah Ulega ametoa wito kwa vyuo na shule zinazofundisha michezo kusimamia vyema ufundishaji wa masomo hayo kwakua ndio yanayosaidia kuzalisha wataalam wa kuendeleza michezo nchini.


Kikao hicho kimeazimia mambo mengi ikiwemo kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya shughuli za michezo ya UMISETA na UMITASHUM

 

No comments :

Post a Comment