Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi wakati akitoa tamko la wiki ya Elimu ya Afya kwa Umma kwenye mwaka wa 2021 mahususi kwa ajili ya kuimarisha udhibiti wa magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza.
Picha mbalimbali zikionesha wataalamu wa afya wakiwa katika mkutano huo.
Na.WAMJW – Dodoma
Wananchi wametakiwa kuzingatia usafi binafsi wa mwili na mikono kwa kutumia maji safi
tiririka na sabuni mara kwa mara katika maeneo yote ikiwemo maeneo ya kazini, mashuleni, vyuoni, nyumba za ibada pamoja na kunywa maji yaliyochemshwa kuanzia nyumbani na mahala pa kazi na baada ya kutoka maliwatoni na mazingira yenye uchafu.Rai hiyo imetolewa leo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi wakati akitoa tamko la wiki ya Elimu ya Afya kwa Umma kwenye mwaka wa 2021 mahususi kwa ajili ya kuimarisha udhibiti wa magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza.
Prof. Makubi amesema kuwa wananchi wanapaswa kufahamu kuwa kinga ni bora kuliko tiba kwani tiba ni gharama na siyo lazima upone maana inaweza kusababisha kifo au ulemavu wa kudumu pamoja na uwingi wa maradhi mengi ikiwemo ya kuambukiza na yasiyoambukiza ambayo yanazuilika iwapo kila mmoja atapata elimu juu ya magonjwa haya na jinsi ya kuzuia”. Alisema Mganga Mkuu huyo.
Amesema mkakati wa utekelezaji wa usafi umeleta matokeo chanya kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita hadi sasa ambapo nchi haijapata visa vya kipindupindu.
“Sasa ni vema kuhamasisha jamii iendelee na hii tabia ya kuhakikisha vifaa vya kunawia na sabuni vinakuwepo katika maeneo yote kuanzia nyumbani hadi mahala pa kazi na ambapo watu hukusanyika ili tuzidi kujikinga na magonjwa yote ya kuambukiza kupitia uchafu ikiwemo magonjwa ya kuhara na mafua”. Alisisitiza Prof. Makubi.
Kuhusu usafi wa mazingira Prof. Makubi amesema wananchi wahakikishe nyumba zinakuwa safi na mizunguko ya hewa inakuwepo ili kukinga dhidi ya magonjwa ya mafua, homa ya mapafu, malaria, kifua kikuu na ili kulinda kinga za mwili zisishambuliwe na maradhi mara kwa mara wananchi wanatakiwa kula lishe bora ili kuimarisha kinga za mwili kwa kula vyakula vya mboga za majani, vyakula visivyo na sukari nyingi, kula matunda na kunywa maji kadri ya mahitaji ya mwili.
Hata hivyo Prof. Makubi alihimiza kuwa ufanyaji wa mazoezi ya mwili na viungo ni nguzo muhimu katika kujenga nguvu za mwili ili kuimarisha mifumo ya hewa, mapafu, moyo na mzunguko wa damu na endapo mwananchi atakapoona dalili za kuugua kwa namna yoyote mfano kuchoka, homa, kukosa hamu ya kula, kichwa na mwili kuuma mwananchi anatakiwa kuwahi katika kituo cha kutolea huduma za afya mara tu anapoona dalili hizo kabla mwili haujachoka hivyo kuwa kwenye nafasi nzuri ya kupona.
Vilevile Prof. Makubi alisisitiza matumizi ya tiba asili katika kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ikiwa ni pamoja na kujifukiza na kunywa dawa za bidhaa za tiba asili kama ambavyo Tanzania imekua na jadi ya asili na kama ilivyo mataifa mengine kwani tiba asili zimesaidia kwenye matibabu ya magonjwa.
No comments :
Post a Comment