Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba akikabidhi ripoti ya utekelezaji wa miradi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote aliyoisoma ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, akipokea ripoti hiyo ni Mkuu wa Mkoa Brigedia Jenerali Marco Gaguti, Mkoani Kagera.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba akiwasikiliza baadhi ya wananchi waliokuwa wakimwelezea baadhi ya changamoto za kimawasiliano wanazokutana nazo katika Kata ya Kakunyu, Kijiji cha Bungango mpakani mwa Tanzania na Uganda, Mkoani Kagera.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia
Jenerali Marco Gaguti akiwa katika picha ya pamoja na Afisa Mtendaji
Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba pamoja na
baadhi ya wajumbe wa bodi ya Mfuko huo baada ya kupokelewa ofisini
kwake, Mkoani Kagera.
…………………………………………………………………………………..
Na Celina Mwakabwale- UCSAF
Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) umesema utahakikisha unaboresha huduma za
mawasiliano ya simu pamoja na usikivu wa radio na televisheni katika maeneo ya mipakani ili wananchi wa maeneo hayo wapate huduma hiyo muhimu lakini pia kuhakikisha salama wa nchi kwa kudhibiti vitendo vya kihalifu vinavyoweza kuwafanywa kwa kutumia mawasiliano na taarifa za nchi nyingine kama uvamizi, uporaji na uhamiaji haramu.Hayo yamebainishwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba akiwa Mkoani Kagera katika ziara aliyoambatana na wajumbe wa bodi ya Mfuko huo kwa lengo la kukagua huduma za mawasiliano katika wilaya za Mkoa huo zinazopakana na nchi nyingine.
Akiwa katika Kata ya Kakunyu, Kijiji cha Bungango mpakani mwa Tanzania na Uganda, Bi Mashiba amesema wananchi wengi katika eneo hilo hawapati huduma za mawasiliano ya mitandao ya simu kutoka Tanzania, hali ambayo kwa namna moja ama nyingine inaweza kuhatarisha usalama wa wananchi hao na nchi kwa ujumla kwa kuwa mitandao ya simu, pamoja na taarifa nyingne katika vyombo vya habari hususani radio na televisheni katika maeneo hayo hupatikana kutoka nchi nyingine.
“Mkoa wa Kagera umepakana na nchi jirani nne, kwa hiyo ni Mkoa ambao unahitaji kuwa katika hali ya usalama na tutakuwa na ziara katika wilaya zote ambazo zimepakana na nchi nyingine ili kubaini ukubwa wa changamoto ya mawasiliano katika maeneo hayo ya mipakani” aliongeza Bi Mashiba.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti ameipongeza UCSAF kwa hatua hiyo huku akiongeza kuwa ni muhimu Mkoa wa Kagera ukapewa kipaumbele kutokana Mkoa huo kupakana na nchi nyingi ukilinganisha na mikoa mingine ya Tanzania.
“Mkoa wa Kagera unapakana na nchi nne kati ya nane ambazo Tanzania tunapakana nazo, tunapakana na Rwanda, Burundi na Uganda na kupitia ziwa Victoria tunapakana na Kenya, kwa hiyo unaweza kuona utofauti”
Kwa upande mwingine Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa mawasiliano ya uhakika yanaweza pia kuboresha hali ya uchumi wa Mkoa na wananchi wa maeneo hayo kwa ujumla.
“Asilimia 50 ya kahawa ya Tanzania inatoka Kagera, na asilimia 80 ya kahawa katika Mkoa huu inatoka katika Wilaya za Mipakani, tumekuwa na changamoto kubwa ya kufikia huduma za kifedha kwa sababu huduma hii inahitaji mitandao ya simu, kwa hiyo kama hakuna mawasiliano ya simu katika maeneo hayo,uwezekano wa wananchi kupata huduma hizo haupo” anasema Brigedia Jenerali Gaguti
Ameongeza kuwa kutokana na changamoto hiyo wakulima wengi Mkoani humo wamekuwa wakiuza kahawa nchi jirani na imekuwa ngumu kuwabana kutokana na kuwepo kwa changamoto ya mawasiliano ya simu na huduma za kifedha kutoka wa watoa huduma nchini Tanzania katika maeneo yao.
Ziara ya Mtendaji Mkuu na wajumbe wa bodi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote inafanyika Mkoa wa Kagera katika Wilaya ya Misenyi, Karagwe, Kyerwa pamoja na Ngara.
No comments :
Post a Comment