Thursday, February 11, 2021

SERIKALI YAANZISHA KITENGO CHA MILIKI KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI

…………………………………………………………………………….

Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Serikali imeendelea  kutambua maeneo yote yenye migogoro ya ardhi ili kuitatua kwa lengo la kuondoa changamoto hiyo kwa wananchi.

Akijibu swali jana Bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias Kwandikwa  alisema kuwa mgogoro wa ardhi kati ya Kambi ya Jeshi ya Itaka na  vijiji vya

Itewe  na Sasenga vilivyopo jimbo la Mbozi, pamoja na mgogoro wa ardhi wa Kasulu imesababishwa na sababu mbalimbali  ikiwemo hali ya uzalendo iliyokuwa ikifanywa na jeshi hilo ya kuruhusu wananchi kufanya shughuli zao katika maeneo ya jeshi ambapo baadae wananchi wamehamia katika maeneo hayo.

“Nafahamu katika kambi ya Itaka kuna mgogoro wa ardhi na tayari Serikali  imetambua maeneo yote yenye migogoro ya  ardhi na tumejipanga kwa ajili ya kuitatua.  Tayari tumeanzisha kitengo maalumu cha Miliki ili kiweze kutatua maeneo yote yenye mgogoro ya ardhi nchini”, alisema Waziri Kwandikwa. 

Aliongeza kuwa zoezi hilo litafanyika kwa kufuata utaratibu ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka na wananchi wanapata  haki zao na jeshi linaendelea na shughuli zake kama kawaida.

Waziri Kwandika alisisitiza, “Zaidi ya asilimia 50 ya migogoro ya ardhi iliyopo kati ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini na Jeshi la Kujenga Taifa imetatuliwa na maeneo mengi ambayo yalihitaji fidia wananchi wameshalipwa fedha zao, na hii inaonesha kuwa tunao mwendelezo mzuri wa kuendelea kulipa na hivyo tunatafuta fedha ili tuweze kulipa maeneo mengine yanayohitaji fidia”.

 

No comments :

Post a Comment