Thursday, February 11, 2021

SERIKALI NA KIWANDA CHA SUKARI KILOMBERO KUONGEZA UZALISHAJI


 

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (Mb.)

 


Na. Peter Haule na Farida Ramadhani, WFM, Dodoma

SERIKALI pamoja na mbia mwenza wa kiwanda cha sukari Kilombero (Kilombero Holding

Limited) wapo kwenye majidiliano ya kuongeza uzalishaji kwa kufanya upanuzi wa kiwanda hicho.

Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (Mb) alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kilombero, Mhe. Abubakar Damian Asenga, aliyeuliza ni lini Serikali itaongeza uwekezaji wa Kiwanda cha Sukari Kilombero ili kunusuru miwa ambayo haijavunwa kwa zaidi ya mwaka mmoja.

“Serikali inaona kuna umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa sukari nchini ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa sukari ambao umekuwa ukijitokeza mara kwa mara hivyo hoja ya kuongeza uwekezaji katika Kiwanda cha Sukari cha Kilombero ni ya msingi”, alieleza Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis.

Mheshimiwa, Mwanaidi Ali Khamis, alisema kuwa wamekubaliana kuangalia gharama za upanuzi, upembuzi yakinifu na ugharamiaji wa mradi, jambo linakalo sababisha uwekezaji katika kiwanda hicho kufanyika kwa haraka.

Alisema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imekuwa ikisimamia utendaji kazi wa kiwanda hicho cha Sukari kwa ukaribu kama inavyosimamia Kampuni nyingine ambazo Serikali ina hisa chache kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina, Sura 370.

 

No comments :

Post a Comment