Tuesday, February 9, 2021

MIFUKO YA UWEZESHAJI UCHUMI KWA WANANCHI KUUNGANISHWA - MAJALIWA

Waziri mkuu akiangalia baadhi ya bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali waliopo kwenye maonyesho ya nne ya mifuko ya programu za  uwezeshaji wananchi kiuchumi yanayofanyika Katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid  jijini Arusha. (picha na Woinde Shizza , ARUSHA)

 
Na Woinde Shizza, Michuzi TV ARUSHA

WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali imeamua kufuta na

kuunganisha baadhi  mifuko ya uwezeshaji 54 iliyopo na kubakiza  michache yenye uwezo ya kuwafikia wananchi wengi vijijini

Ameeleza hayo leo wakati akifungua maonyesho ya nne  ya mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi yanayoendelea Mkoani Arusha, ambapo amesema kuna mifuko mingi ambayo haijulikani nini  inafanya na wapi inapatikana, hivyo Serikali haina budi kuifuta na kuunganisha baadhi ili lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi liweze kutumia.

Aidha amewaagiza wakuu wa mikoa kupitia mifuko hiyo   kuangalia aina ya mikopo wanayotoa Ili kuweza kuwasaidia wananchi  kutapata uwezeshwaji kwa gharama nafuu.

Pia ameiagiza mifuko hiyo kufanya uwezeshaji kwa kuwa wabunifu zaidi ili kuweza kupanua wigo wa kukuza uchumi wa wananchi na kwenda sambamba na  malengo ya Serikali yanayolenga  kukuza uchumi taifa na mtu mmojammoja.

Vilevile amesema kuwa, tathimini zilizofanywa zinaonyesha mifuko hiyo imesaidia kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kupata mikopo ambapo hadi sasa mifuko hiyo imeshatoa mikopo ya shilingi trilioni 2.22 iliyowanufaisha watu milioni 4.9.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa baraza la taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi, Festus Limbu amesema kuwa, maonesho hayo yamekuja katika kipindi kizuri ambacho serikali imeingia Katika kipindi chake cha awamu ya pili ya uongozi ambao bado wanaendelea  na dhamira yake kutekeleza kauli mbiu  yao ya  kuwezesha wananchi kiuchumi.

"Dhamira ya nchi katika ujenzi wa taifa imara inatekelezwa kwa nguvu zaidi na ndio maana kauli mbiu  ya maonyesho hayo inayosema "Mifuko na Programu ya Uwezeshaji Wananchi  Kiuchumi kwa Maendeleo ya Taifa." Amesema.

Amesema kuwa Serikali ilianzisha mifuko hiyo kwa ajili ya kusaidia wananchi kujenga uchumi wa nchi na kuteketeza umaskini .

Pia Katibu mtendaji wa baraza la taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi  Beng'i Issa alisema kuwa Katika maonyesho hayo watatoa mafunzo mbalimbali ikiwemo namna ya kuandaa  maandiko ya biashara, ujasiriamali, mikopo, Jinsi ya kuanzisha biashara, jinsi ya kuongeza thamani ya biashara pamoja na namna ya kutunza maandiko ya biashara.

Amesema wanategemea maonesho haya yatakuwa na manufaa makubwa katika kuelekea uchumi wa viwanda hususani katika kipindi hiki ambacho taifa  limefikia mefika katika uchumi wa kati.

No comments :

Post a Comment