Wednesday, February 3, 2021

Mheshimiwa Rais, wafanyakazi tunakuomba msamaha

KIPANYA MONEYmsamahapic
By Mwandishi Wetu

Mheshimiwa Rais, nakusalimia kwa heshima na taadhima, Mimi kijana wako naendelea kulitumikia

taifa nikiwa kituo changu cha kazi hapa Mlimani, kuna jamaa wengine wanapaita Jalalani, ingawa silipendi kabisa hili jina.

Kilichonisukuma kukuandikia ni baada ya kukutana na Profesa mmoja akinunua mihogo kwa ajili ya chakula cha mchana, mitaa ya jirani na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Profesa huyo kapandishwa cheo mwaka jana, lakini bado hajaanza kulipwa mshahara wa uprofesa hadi sasa.

Nilipomuuliza kwanini ananunua mihogo ya Sh2,000 akadai kuwa ‘purchasing power’ yake ni kidogo na haijaongezeka tangu uingie madarakani. Nilimkemea kwa niaba yako kwa sababu anakuonea; umekuwa ukipambana kukuza uchumi wa nchi.

Ingawa kiukweli wako wafanyakazi wengi wa kundi lake ambao hadi sasa wanalilia kulipwa mishahara stahiki kwa muda mrefu, lakini hawaoni dalili zozote. Na wengine bado wanasubiri malimbikizo.

Ukiacha maprofesa, wapo manesi, walimu, waganga, mabwana na bibi shamba na mifugo, askari polisi, magereza, uhamiaji, makarani, makatibu muhtasi, wakunga, waganga wa maabara, mafundi umeme, wakufunzi na wahadhiri, na wengine wengine. Orodha ni ndefu, nao kilio chao ni hicho hicho.

Nimekusanya sahihi zao kutoka maeneo mbalimbali ya Tandahimba, Newala, Namtumbo, Madaba, Ludewa, Makete hadi Ileje, Nkasi, Mlele, Buhigwe, Kakonko, Karagwe, Ngara, Busega, Itilima, Mkalama, hadi Rorya. Nilitaka niwakatae jamaa wa kutoka Runzewe, Katoro na Bwanga nikiamini wanaweza kukufikishia wao wenyewe, lakini nikaona si vibaya ngoja niwawakilishe.

Ila mawaziri, makatibu wakuu, majaji, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya hawahusiki na msamaha.

Wafanyakazi wengi uwezo wao wa kufanya manunuzi ni mdogo. Kiasi kilichokuwa kinaingia mwaka 2016 ndo hicho hicho hadi mwaka 2021, wanatamani waone nafuu fulani kwenye uwezo wao wa kuhimili manunuzi kwa ajili ya kuhudumia familia.

Naona kama wenzetu wa Bodi ya Mikopo walinusa hilo mapema . Wao wakaweka kipengele cha ‘value retention fee’ toka 2016 kulinda thamani yao ya hela. Walijua kila mwaka thamani ya hela inashuka kwa asilimia sita na ikifika 2021 hela waliyoweza kumpatia mwanafunzi 2016 itakuwa haitoshi 2021, hivyo wakapachika hicho kijamii kinaitwa ‘value retention fee’.

Ukiacha Bodi ya Mkopo kutukata asilimia 15 ya mkopo, kuna hawa jamaa wa TRA nao naona wameamua kutukomalia zaidi wafanyakazi tuwe na TIN. Wamesema bila TIN mwezi huu wa Januari tunatoka bila bila kwenye akaunti zetu.

Mheshimiwa Rais, naomba nichukue nafasi hii kuzishukuru benki tunazopitishia mishahara yetu. Ingawa wanatengeneza faida, lakini huwa wanatuokoa. Baada ya mshahara kuingia wakakata hela yao waliyonikopesha mwezi uliopita. Nilipochungulia kilichosalia kikawa hakitoshi kunifikisha wiki moja mbele, basi siku hiyo hiyo nikakopa tena ‘salary advance’. Sasa hivi ndo ‘salary advance’ ndio mkombozi wetu.

Mheshimiwa, siyo kwamba tunapenda kuishi hivi, ila majukumu ya kifamilia ni mengi na uwezo wa kuyamudu kwa hiki tunachopokea ni mdogo, maana wakataji ni wengi.

Sitaki kuingia nao ugomvi lakini mishahara yetu inachukuliwa na TRA, HESLB, NHIF, PSSF/NSSF kwa sehemu kubwa.

Mheshimiwa Rais, nisikuchoshe na maneno mengi. Wafanyakazi wenzangu walioko Serikalini wameniomba nije kukuomba radhi, kama wakati wowote tangu ukiwa waziri hadi Rais kuna mahali tulikukosea, tunaomba msamaha. Maisha yetu huku mtaani ni magumu, hatuna furaha, baadhi yetu tuna sura za uzee kumbe bado vijana.

Ndoa zetu sasa hivi ziko hatarini, wake zetu wanatudhania wote tuna tabia za wangoni kumbe shida yetu ni hela. Tuna changamoto nyingi za kifamilia, kijamii na binafsi.

Sasa hivi hata viongozi wa dini tunawaona kama wapiga dili kwa sababu nao hawajui tumesahauliwa kwenye ‘value retention’ ya mishahara yetu, utawasikia wakisema, ‘safari hii tegemeza jimbo ongezeko ni asilimia 40 ya mwaka jana’.

Wakiangalia vitambi vyetu wanajua tuna hela kumbe thamani ya mifuko yetu bado ni ile ile ya mwaka 2016.

Tuonee huruma Mheshimiwa Rais, usishangae asilimia kubwa ya wafanyakazi wa Serikali tukianza kukusanya chupa tupu mtaani na kuzigombania kwenda kuuza. Natumaini wewe ni baba mwenye huruma utasikiliza maombi yetu ya msamaha.


Imeandikwa na Faraja Kristomus, mwandishi anafundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na anapatikana kwa simu ya mkononi 0787525396

 

No comments :

Post a Comment