Saturday, February 13, 2021

Makamu wa Rais atembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa maji Pugu-Gongo la Mboto


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Pugu alipotembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa maji Pugu-Gongo la mboto ulioanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi na kuzindua maji kwenye nyumba ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

 Na Zainab Nyamka, Michuzi Tv

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa maji Pugu-Gongo la mboto ulioanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi.

Makamu wa Rais amefanya ziara ya kutembelea miradi inayotekelezwa na DAWASA na kuzindua maji kwenye nyumba ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Samia amesema Dawasa wamefanya kazi kubwa sana ya kupeleka maji katika maeneo muhimu hususani ya Dar es Salaam ya kusini 

 Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja kuhusu amesema, mradi huo una thamani ya Bilioni 6.9 ukitekelezwa kwa fedha za ndani.

Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema kufikishwa kwa  maji ndani ya Shule ya Sekondari Pugu ni jambo kubwa sana kutokana na shule hiyo kukosa huduma hiyo kabla ya uhuru na hata kipindi ambacho baba wa Taifa anaishi hapo.

Amesema, wakati anasoma Pugu Sekondari hawakuwa na huduma ya maji na zaidi walikuwa wanakaa hata wiki nzima bila kuoga.

Hata hivyo, ameupongeza uongozi wa Dawasa chini ya Mwenyekiti wa Bodi Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange na Afisa Mtendaji Mkuu Mhandisi Cyprian Luhemeja kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kumtua mama ndoo kichwani.

Akielezea kwa ufupi,Luhemeja amesema mradi huo umekamilika na leo Makamu wa Rais atazindua maji katika nyumba aliyoishi Hayati Baba wa Taifa katika shule ya Sekondari Pugu 

Amesema, huu ni moja ya mradi wa kimkakati na kwa sasa Dawasa inatekeleza miradi mikubwa 7 na midogo yenye thamani ya Bilion 62 wakitumia fedha za ndani.

 Luhemeja amesema mradi ni wa Km 50  hadi sasa tayari wameshalaza  Km  18 kutoka Pugu hadi Chanika na utawanufaisha wakazi wa Gongo la Mboto, Chanika, Majohe, Ukonga na baadhi ya maeneo ya Jimbo la Segerea na ujenzi wa tanki la ujazo wa lita Milioni 2 umekamilika.

Naye Mwenyekiti wa Bodi wa Dawasa Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange amesema Dawasa bado wana mikakati ya kumaliza tatizo la maji ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na Miji ya Pwani.

Ameeleza kuwa kwa sasa hivi wanafikiria kuchukua maji kutoka Mto Rufiji ili kila mwananchi apate huduma ya maji.

Mbali na hilo, amesema kazi kubwa inayofanywa na Dawasa ni kuhakikisha inafikia lengo la asilimia 95 ya upatikanaji wa maji kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

No comments :

Post a Comment