Wednesday, February 24, 2021

DKT. GWAJIMA AELEKEZA KUTOLEWA KWA ELIMU YA KUTENGENEZA VIPUKUSI NCHINI.



 Na Rayson Mwaisemba, WAMJW- DOM

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amemwagiza Mfamasia Mkuu wa Serikali kuendelea kutoa elimu ya namna ya kutengeneza vipukusi kupitia taasisi mbalimbali nchini ili kusaidia wananchi kupata huduma hiyo kwa gharama nafuu zaidi ili kuweza kujikinga dhidi ya magonjwa yakuambukiza na yasiyoambikiza.

Dkt. Gwajima ametoa maelekezo hayo leo wakati akitoa tamko la kuongeza kasi ya utekelezaji wa hatua za kujikinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza katika Kongamano la Mkutano Mkuu wa Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii nchini.

"Namuelekeza Mfamasia Mkuu wa Serikali kuendelea kutoa elimu ya jinsi gani tunaweza kutengeneza vipukusi vyetu vya ndani ya nchi kupitia taasisi zetu, zilizo karibu zaidi na wananchi ili kuwezesha wananchi kupata huduma hii ya vipukusi kwa bei rahisi zaidi hali itakayosaidia kujikinga dhidi ya magonjwa" amesema Dkt. Gwajima.

Ameendelea kusema kuwa, tuendeleze tabia ya kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi yanayo tiririka na sabuni. Iwapo maji tiririka na sabuni hakuna, tumia vipukusi (sanitizer).

Hata hivyo, amewataka wananchi kuvaa barakoa safi na salama ambayo wametengeneza wao mwenyewe au wamenunua kwa watengenezaji wa ndani waliothibitishwa na Wizara ya Afya mfano Bohari ya Dawa, taasisi  za afya na watengenezaji wengine ambao wamethibitishwa.

Vile vile amemwelekeza Mfamasia Mkuu wa Serikali kutoa elimu ya jinsi ya kutengeneza barakoa binafsi na kuwataka wananchi kuvaa barakoa kwa kuzingatia muongozo uliotolewa na Wizara hususan katika maeneo ya msongamano, huku akimwagiza Mfamasia Mkuu wa Serikali kutangaza orodha ya watengenezaji wa barakoa ambao wamesha thibitishwa.

Pia, Dkt. Gwajima ameendelea kutoa wito kwa wananchi kufanya mazoezi mara kwa mara, baadhi ya mazoezi rahisi kama vile kutembea kwa kasi siyo chini ya dakika 30 au zaidi walau utoke jasho, kuruka kamba, kukimbia mwendo unaoona unakufaa na kufanya zoezi la kusimama na kukaa.

Hata hivyo ameendelea kusisitiza matumizi ya tiba asili kwa dawa za kunywa na kujifukiza zilizosajiliwa na Baraza la Tiba Asili kama inavyoelimishwa na wataalamu husika, na kuwaagiza waratibu wa tiba asili ngazi zote za mkoa na halmashauri kuendelea kutoa elimu kwenye redio za maeneo yao.

Amewataka wananchi, kuepuka misongamano isiyo ya lazima ikiwemo kwenye vyombo vya usafiri, huku akiwataka wananchi kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za afya mara waonapo dalili za maradhi ili watoa huduma wapate nafasi nzuri zaidi ya kutoa matibabu.

No comments :

Post a Comment