Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Geoffrey Mwambe (Mb) amewataka watumishi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Wakala wa Vipimo (WMA) kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na kuwafikiria wafanya biashara wakati wakitoa huduma kwa wafanyabiashara ili kuendelea kutengeneza taswira nzuri ya bidhaa za Tanzania katika soko la ndani nan je ya nchi.
Waziri Mwambe aliyasema hayo alipokuwa akiongea na menejimenti na wafanyakazi wa TBS na WMA alipofanya ziara katika taasisi hizo akiambatana na Naibu Waziri wa Viwanda Mhe. Exaud Kigahe (Mb) pamoja na baadhi ya wakurugenzi wa Wizara ya Viwanda na Biashara leo tarehe 11 Januari 2021 katika taasisi husika.
Akiwa TBS, Waziri Mwambe ameiagiza TBS kufanya ukaguzi wa bidhaa kwa kushirikiana na taasisi nyingine zinazohusika na ukaguzi wa mizigo bandarini na mipakani ili kupunguza muda unatumika kugagua bidhaa hizo,kupunguza mianya ya rushwa na kurahisisha utoaji wa mizigo hiyo kwa haraka.
Aidha, Mhe. Waziri aliitaka TBS kupunguza muda wa kuandaa viwango kutoka miezi 9 hadi miezi 3 na muda wa usajili wa bidhaa na kutoa alama ya ubora kutoka miezi 3 hadi mwezi mmoja ili kuwarahisishia wajasiliamali kuwezakufanya na kukuguza biashara zao kwa urahisi.
Vilevile Mhe. Waziri ameielekeza TBS kufanya kazi kwa pamoja na Shirika la Kuhudumia Viwand Vidogo (SIDO) na Balaza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC katika kuandaa Viwango na miongozo yenye vigezo rahisi vitakavyowawezesha wajasiliamali kuanzisha viwanda vidogo majumbani ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa,kukuza biashara kuongeza ajira nakuongeza pato la taifa.
Mhe. Mwambe pia ameihimiza TBS kufanya kazi kwa karibu na Maafisa Biashara wa Halmashauri ili kurahisisha utoaji wa elimu na usimamizi wa viwango kwa wajasiliamali ili kupanua uwigo wa utoaji huduma na kuwafikia wajasiliamali wengi walioko katika halmashauri hizo.
Naye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe amezitaka TBS na WMA kuhakikisha zinasimamia viwango na ubora pamoja na vipimo sahihi vya bidhaa za Tanzania ili kuziwezesha bidhaa hizo kuingia katika soko la ushindani ndani na nje ya nchi kwa ufanisi.
Aidha naibu Waziri aliziagiza taasisi hizo kuendelea kuimarisha ukaguzi wa bidhaa zinazotoka nje ya nchi zinakuwa na viwango navipimo sahihi ili kuiepusha Tanzania kuwa dampo la bidhaa hafifu.
No comments :
Post a Comment