Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,
Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla amesema Tangazo la Elimu Bila Malipo
lililotolewa mara tu baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka
1964 lilikuwa na maana ya kuongeza fursa za kupata elimu iliyo bora kwa
wote,
Mheshimiwa
Hemed Suleiman Abdulla amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Skuli ya
Sekondari ya Donge Mkoa Kaskazini Unguja ikiwa ni shamrashamra za
Maadhimisho ya kusherehekea Miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar
ya Mwaka 1964.
Amesema,
elimu bora na ya kiwango ndio inayomuwezesha mwanaadamu hasa watoto wa
Taifa hili kukabiliana vyema na changamoto mbalimbali watakazokuwa
wakipambana nazo katika maisha yao, wazazi na hata Taifa kwa ujumla. Hemed
ameeleza kwamba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane chini
ya usimamizi wa Rais wake Dkt. Hussein Ali Mwinyi itaendelea kutoa elimu
bila ya malipo kwa taaluma ya msingi hadi sekondari ili kuwawezesha
wananfunzi wenye sifa kupata elimu bila ya vikwazo.
“Rais
wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Aman Karume aliyeongoza
Mapinduzi ya Zanzibar kwa lengo la kuwakomboa Wazanzibari alitangaza
Elimu bure kwa wote bila ya ubaguzi wowote mnamo Tarehe 23 Septemba
1964,"amesisitiza Mheshimiwa Hemed Suleiman.
“Rais
Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Saba, Dkt. Ali Mohamed Shein naye
alitoa Tamko katika Sherehe za Miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar pale
Uwanja wa Aman Tarehe 12/01/2015 kwa kufuta kabisa ile michango midogo
midogo ya Skuli, kwa nganzi ya Elimu ya Msingi na baadae Sekondari,”
amekumbusha Mheshimiwa Hemed.
Amewapongeza
wananchi wa Donge kwa jitihada, mshikamano,ushirikiano na ustahamilivu
wao wa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kujiletea maendeleo hasa
katika sekta muhimu ya elimu ambapo sasa jamii inashuhudia matunda
hayo.
Makamu
wa Pili wa Rais amesema kwamba Donge imekuwa mfano mzuri wa kuigwa na
Jamii nyengine hapa Nchini kwa kujenga Skuli kubwa na ya Kisasa ya
Ghorofa jambo ambalo limesaidia kupunguza changamoto za ufinyu wa nafasi
katika Elimu ndani ya Wilaya ya Kaskazini B.
Amesema
ujenzi wa Skuli hiyo ni kielelezo cha juhudi za Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar katika kuwaletea Maendeleo Wananchi wake ikiwa ni Mkakati wa
kuhakikisha nafasi za masomo kwa Watoto wa Visiwa vya Unguja na Pemba
zinapatikana katika maeneo yote.
“Fursa
sawa za kupata Elimu ni miongoni mwa malengo ya Mapinduzi yetu ya Mwaka
1964 ambapo hivi sasa tumo katika kuadhimisha Miaka 57,”ameeleza Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Mheshimiwa
Hemed amesema, historia inaeleza kwamba Wilaya ya Kaskazini B haikuwa
na hata Skuli Moja ya Sekondari kabla ya Mapinduzi na wakati huo Elimu
ilikuwa ikitolewa kwa ubaguzi katika maeneo na watu maalum.
Amebainisha
kwamba hivi sasa Wilaya ya Kaskazini B ina jumla ya Skuli 11 za
Sekondari pekee ikiwa ni maendeleo makubwa na ni Matunda ya Mapinduzi ya
Mwaka 1964 ambapo Wananchi wanapaswa kujivunia kwa vile Elimu imekuwa
ikiwafikia Wananchi pale walipo.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesisitiza umuhimu wa Wazazi, Walezi,
Walimu na Kamati za Maskuli Nchini kuendelea kushirikiana hatua
itakayorahisisha upatikanaji wa Maendeleo ya haraka ya Watoto wao.
Aidha
Mheshimiwa Hemed Suleiman amewakumbusha Wanafunzi kuyatumia mazingira
bora wanayowekewa na Serikali kwa kuzidisha juhudi za masomo
zitakazozalisha matokeo mapya ya viwango vya juu katika Mitihani yao ya
Taifa.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameridhika na gharama zilizotumiwa za
Ujenzi wa Mradi wa Skuli ya Sekondari ya Donge jambo ambalo wasimamizi
wa Mradi huo wanastahiki kupongezwa kutokana na Uzalendo wao
waliyouonyesha.
Amesema
alikuwa akifuatilia muenendo wa watangulizi wake katika hafla hiyo na
kama asingeridhika na Mradi huo aliweka wazi kwamba asingeufungua Mradi
huo na angelazimika kuiagiza Mamlaka ya kupamba na Rushwa na kuzuia
Uhujumu Uchumi Zanzibar {Zaeca} kufanya uchunguzi.
Amewatahadharisha
Walimu Wakuu wa Maskuli ya Sekondari kusimamia majukumu yao katika
kuona kiwango cha Ufaulu kinaongezeka mara dufu kuanzia sasa vyenginevyo
Wizara ya Elimu italazimika kumuwajibisha Mwalimu Mkuu husika.
Uongozi
wa Serikali Mkoa wa Kaskazini Unguja unapaswa kuweka mkakati maalum
katika kuhakikisha Wilaya zilizomo ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja
zinaondoa au kupunguza kabisa Zero zinazotokea katika Skuli mbali mbali
za Mkoa huo.
Akitoa
Taarifa za Kitaalamu kuhusiana na Ujenzi wa Jengo la Skuli ya Sekondari
ya Donge, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Zanzibar Mhandisi Dr. Idriss
Muslim Hijja alisema Jamii ya Kijiji hicho ilifikia hatua ya kuanzisha
Mradi huo ili kukidhi mahitaji halisi.
Dr.
Muslim amesema ujenzi rasmi wa Jengo hilo la Ghorofa Mbili ulianza
mnamo Mwaka 1992 kwa kutumia nguvu za Wananchi wenyewe licha ya ujenzi
wake kusua sua kwa kipindi kirefu kilichopelekea Mradi huo kuachiwa
Serikali Kuu kwa hatua zinazoendelea.
Amesema,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Amali ilitafuta wafadhili na wahisani kwa ajili ya kukamilisha ujenzi
huo uliomalizika rasmi Mwishoni mwa Mwaka 2020.
Katibu
Mkuu huyo wa Wizara ya Elimu amesema kwamba Mradi wa Ujenzi huo wa
Skuli ya Sekondari ya Donge uliogharimu Jumla ya Shilingi Bilioni 1.3
utakidhi mahitaji halisi kwa vile msongamano wa Wanafunzi wa Sekondari
na Msingi kwa sasa umeondoka kwa vile watakuwa wakipata elimu kwa
kutumia mkondo Mmoja tu wa Asubuhi.
Kwa
upande wao Mwakilishi wa Jimbo la Donge Dr. Khalid Salum Mohamed na
Mbunge wa Jimbo hilo Mheshimiwa Soud walisema ndani ya Miaka Mitano
ijayo watahakikisha Skuli ya Sekondari ya Donge inaanza kutoa Wanafunzi
wa Kidato cha Tano na kuendelea na cha Sita.
Walisema
mpango huo unawezekana kabisa kwa vile wamekusudia na kinachohitajika
zaidi ni nguvu za pamoja kati ya Uongozi, Wazazi, Wananchi pamoja na
Kamati ya Skuli.
Viongozi
hao wa Jimbo la Donge wameikumbusha Serikali kufikiria Utekelezaji wa
ahadi ya Rais wa Zanzibar katika ujenzi wa Bara bara ya Donge hadi
Chaani kwa kiwango cha Lami wazo ambalo tayari Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar alithibitisha kwamba halina mjadala wakati ni ahadi ya
Serikali.
Dr.
Khalid na Mheshimiwa Soud waliomba katika kuimarisha Elimu ya Sekondani
Serikali iangalie pia uwezekano wa Kujenga Dakhalia pamoja na Ukumbi wa
Mikutano kwenye Skuli hiyo ili kukidhi mahitaji halisi ya Wataalamu wa
Skuli hiyo.
Akitoa
salamu za Mkoa wa Kaskazini Unguja. Mkuu wa Mkoa huo Mheshimiwa Ayoub
Mohamed Mahmoud alisema Mkoa huo utaendelea kusimamia Elimu ili kuongeza
matokeo ya ufaulu wa Wanancfunzi katika Mitihani yao ya Kitaifa na
hatimae kubakia kuwa Historia kwa mikakati itakayowekwa ya kuondosha
changamoto ya matokeo mabaya.
Mh.
Ayoub alisema Serikali ya Mkoa imethibitisha kuendelea kuliona Jengo
hilo la Skuli ya Sekondari ya Donge linatunzwa kutokana na Historia yake
iliyotokana na Wananchi wa eneo hilo kubeba dhima ya kuwajengea
mazingira bora ya Elimu Watoto wao.
Alisema
Jengo hilo lina Historia Maalum likiingia katika Tunu ya Mapinduzi
kutokana na kujengwa katika misingi ya nguvu za Wananchi wenyewe
waliokuwa chini ya Waasisi wa Afro Shirazy Party wa eneo hilo.
Akimkaribisha
Mgeni rasmi kuzungumz na Wananchi hao wa Kijiji cha Donge na Vitongoji
vyake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mheshimiwa Simai Mohamed Said
alisema Wizara hiyo inakusudia kufanya mapitio ya Mitaala ya Elimu kwa
lengo la kuwajengea mazingira bora zaidi ya Taaluma Wanafunzi wake.
Mh.
Simai alisema hatua hii ndio itakayosaidia ufaulu mkubwa wa Wanafunzi
jambo ambalo Serikali Kuu kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
katika kuimarisha Sekta hiyo imekusudia kujenga Majengo mengine Matatu
ya Sekondari katika maeneo ya Gamba na Mfenesini kwa Unguja na Micheweni
kwa Pemba.
Skuli
ya Sekondari ya Donge inakusudia kuchukuwa wanafunzi 800 wakati ile ya
msingi iliyopo jirani ina wanafunzi wasiopungua 1,000.
No comments :
Post a Comment