Thursday, January 21, 2021

WAZIRI MKUU AAGIZA KODI NA TOZO ZA MKONGE ZIFANYIWE MAPITIO

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo ifanye mapitio ya kodi na tozo zote zilizopo katika zao la mkonge kwa lengo la kubaini ni zipi zenye manufaa kwa wadau na

Taifa na kuainisha zisizokuwa na tija ili zifanyiwe mchakato wa kuondolewa.

Pia, Waziri Mkuu alizitaka taasisi za kifedha nchini ziendelee kuangalia kiasi cha riba kinachotozwa kwa wakulima wanaokopeshwa ili zisisababishe wahusika kushindwa kukopa kutokana na ukubwa wa riba.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo jana (Jumatano, Januari 20, 2021) wakati wa kikao chake na wadau wa mkonge kwenye ukumbi wa Regal Naivera jijini Tanga, ambapo alitumia fursa hiyo kuiagiza Wizara ya Kilimo iendelee kufuatilia mwenendo wa mazao yote ya biashara.

Alisema Serikali imejipanga ipasavyo kuhakikisha zao la mkonge linarudi katika nafasi yake, hivyo aliiagiza Wizara ya Kilimo iendelee kuratibu maendeleo yake kuanzia hatua za utayarishaji mashamba hadi mwenendo wa masoko.

“Mkonge unafaida nyingi lakini sisi tumejikita katika utengenezaji wa nyuzi tu, tutumie wataalamu wa vyuo vikuu na taasisi za utafiti kwa ajili ya kutumia fursa nyingine zinazopatikana katika zao hili kwa kutengeneza sukari, mbolea na vinywaji.”

Waziri Mkuu alisema Wizara ya Kilimo iendelee kukiboresha Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Mlingano na ijiridhishe kama kina vifaa vya kutosha katika uzalishaji wa miche ya mkonge. Pia aliiagiza Bodi ya Mkonge Tanzania ishirikiane kikamilifu na kituo hicho ili kuendelea kuboresha zao hilo.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliziagiza halmashauri zote zinazolima mkonge nchini pamoja na uongozi wa Bodi ya Mkonge kuanzisha kanzi data kwa ajili ya kuwa na takwimu za wakulima wadogo, wakati na wakubwa pamoja na ukubwa wa mashamba yao.

Alisema kanzi data hiyo itawasaidia kuwafikia wakulima kwa urahisi pale wanapotaka kutoa elimu kuhusu namna bora ya kulima zao hilo kuanzia hatua za uandaaji wa shamba, matumizi ya pembejeo pamoja na upatikanaji wa masoko.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema mwaka 2020 uzalishaji wa mkonge nchini ulikua tani 36,298, malengo yalikuwa ni kuzalisha tani 42,286. Katika kipindi cha 2020-2025 Bodi ya Mkonge inampango wa kuongeza uzalishaji na kufikia tani 120,000 kwa mwaka.

Alisema Wizara ya Kilimo itahakikisha nchi inapunguza uagizaji wa magunia ya katani kutoka nje ya nchi ili kuliongezea tija zao. “Kwa kuanzia katika zao la korosho msimu huu wakati wa kutangaza ‘tender’ ya vifungashio tumeeleza kwamba tunatoa ‘priority’ kwa vivungashio vya katani vinavyozalishwa nchini.”

Kufuatia hatua hiyo, alivitaka viwanda vyote vya Serikali vya kutengeneza vifungashio kwa kutumia katani vilivyopewa wawekezaji binafsi kuhakikisha vinafanya kazi kwani Wizara ya Kilimo haitasita kushauri Serikali kuvirudisha Serikalini vile ambavyo havitafanya kazi kufikia mwishoni mwa mwaka fedha wa 2020/21.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge Tanzania, Saady Kambona alisema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2020 kampuni ya mkonge ya Amboni Plantation iliongoza kwa upande wa wakulima wakubwa kwa kuzalisha tani 8,277 katika shamba la hekta 14,000 ikifuatiwa na kampuni ya Melt iliyozalisha tani 4,922.53 katika shamba lenye ukubwa wa hekta 33,000 huku wakulima wadogo nchini wakiongoza kwa kuzalisha tani 9,728.63.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imejipanga ipasavyo kuhakikisha zao hilo linafufuliwa na tayari imefanya utafiti wa kutosha ambapo inatarajia kuongeza uzalishaji na kufikia tani 150,000 ifikapo mwaka 2025.

No comments :

Post a Comment