***********************************************
Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amefanya ziara ya kushtukiza leo
katika ofisi za ardhi za Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino jijini
Dodoma ambapo ameagiza kubadilishwa vituo vya kazi Mkuu wa Idara ya
Ardhi Bwana Letare Sinda na Afisa Mipango Miji Bwana David Msemo.
Waziri Lukuvi amefikia uamuzi
huo baada kukagua utunzaji wa nyaraka pamoja na maombi ya vibali vya
ujenzi yaliyowasilishwa kwenye ofisi ya Mipangomiji kwenye Halmashauri
hiyo ambapo, alikerwa na ukiukwaji wa sheria na miongozo ya kutoa
vibali vya ujenzi na umilikishaji ardhi ambao umechangia malalamiko ya
wananchi kuongezeka.
Lukuvi ameagiza Kamishna wa
Ardhi na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi kutoka Makao makuu ya Wizara
watume wataalam wengine haraka iwezekanavyo ili wakasimamie uandaaji wa
nyaraka za umiliki pamoja na utoaji vibali vya ujenzi katika Halmashauri
ya Wilaya hiyo.
Ameongeza kwamba, Wilaya ya
Chamwino ndiyo Wilaya pekee ambayo ilipewa upendeleo na Wizara wa
kupatiwa vifaa vya Upimaji, gari la Idara ya ardhi na vifa vya Kompyuta
lakini ndiyo Wilaya inayolalamikiwa zaidi katika mkoa wa Dodoma.
‘Jiji la Dodoma linakua kwa
haraka sana, Wilaya ya Chamwino ndiyo Wilaya namba moja na Ikulu ipo
ndani yake. Ni lazima iwe wilaya ya mfano kwenye utoaji huduma za sekta
ya ardhi. Muda wa kufanya kazi kwa mazoea hakuna tena, kila mtaalam
afuate miongozo iliyowekwa na Serikali ya kutolea huduma, Alisema
Lukuvi’
Lukuvi Alisema, Wilaya ya
Chamwino imekuwa na tamaa ya kuuza viwanja kwa gharama kubwa, kiasi cha
kuwakatisha tamaa wananchi masikini na wanyonge ambao ndio wazawa wa
Chamwino. Hali hii inapelekea wananchi kuyakimbia maeneo yao na kwenda
kutafuta maeneo sehemu nyingine na kuanzisha Makazi holela.
Aliongeza kwamba, wananchi
wachache wanaoweza kununua viwanja ndani ya Wilaya hiyo, bado wanakutana
na changamoto nyingine ya gharama kubwa za vibali vya ujenzi ambapo
hata kumbukumbu tuu za jumla ya maombi yaliyopokelewa na yaliyotolewa
hakuna.
Mbali na sheria na miongozo
kutokufuatwa, Waziri Lukuvi amesema maombi mengi ya vibali vya ujenzi
hayajatolewa na hakuna nyaraka yeyote inaoonesha sababu zilizokwamisha
maombi hayo.
“Haiwezekani mwananchi alete
maombi ya kibali cha ujenzi yeye mwenye na asikifuatilie kama taratibu
za utoaji huduma ni rafiki na ziko wazi, Alisema waziri Lukuvi”.
Aidha, Mhe.Waziri amesema
kufanya kazi kwa mazoea na kutokuzingatia sheria, taratibu na kanuni
katika utoaji wa huduma kunatengeneza mianya ya rushwa na kuzalisha
malalamiko ya wananchi.
Katika muongozo wa utoaji vibali
vya ujenzi uliotolewa hivi karibuni na Ofisi ya Rais TAMISEMI uliwataka
wataalam wote wanaohusika kupitia maombi kuweka utaratibu wa kukutana
wote kwa pamoja na kupitia maombi yaliyowasilishwa ili kutoa mwanya kwa
kila mtaalam kujiridhisha na kipengele kinachomuhusu. Aidha muongozo huo
uliwataka wataalam hao kuhakikisha kibali cha ujenzi kinatolewa ndani
ya siku saba tangia maombi yalipowasilishwa.
No comments :
Post a Comment