Polisi imethibitisha kuwa mwanamke mmoja aliyepigwa risasi wakati wa vurugu zilizotokea baada ya wafuasi wa Trump kuvamia bunge, amefariki dunia kwasababu ya majeraha aliyopata.
Bado maafisa hawajataja jina la mwanamke huyo lakini polisi wanasema alikuwa raia wa kawaida.
Aidha, mtu mwingine amepigwa risasi wakati wa vurugu zilizotokea ndani ya bunge la Marekani, kulingana na shirika la habari la Associated Press.
Lindsay Watts, mwanahabari wa shirika lenye kuhusishwa na Fox News, ameandika ujumbe kwenye Twitter kuwa wahudumu wa afya wa Washington DC walisema juhudi za kumuokoa mwanamke mmoja aliye kwenye hali mahututi zinaendelea baada ya kupigwa risasi kifuani.
Wafuasi wa Trump waliokuwa na hasira waliandamana huku wakiimba, "Tunamtaka Trump" huku mmoja wao akipigwa picha akiwa ameketi kwenye kiti cha rais wa bunge la Seneti.
Polisi Washington imesema kuwa ni wazi waandamanji hao walikuwa tayari kutumia nguvu yoyote ile kuingia katika majengo ya bunge.
Inasemekana hadi kufikia sasa watu 13 na silaha tano zimenaswa na polisi wakati ghasia zinaendelea bungeni.
Maafisa polisi wa Washington DC wamesema wamepata bunduki tano ikiwemo za mkononi na ndefu.
Mkuu wa polisi Robert Contee amewaambia wanahabari kuwa waliokamatwa sio wakazi wa eneo la DC.
Baada ya uvamizi huo uliochukua saa kadhaa, afisa anayesimamia mipangilio ya bungeni alitangaza kuwa sasa jengo hilo limenusuriwa na vikosi vya usalama.
Wakati mmoja Bwana Trump alilazimika kurekodi ujumbe kwenye video na kuutuma katika mtandao wa Twitter akitoa wito kwa wafuasi wake kuondoka katika majengo ya bunge lakini naye akawa anaendelea madai yasiokuwa na ushahidi wowote kuwa Democrats waliiba kura.
Lakini kukawa na ishara kidogo zinazoonesha kwamba waandamanaji hao wanatii wito wa Trump unaowataka warejee nyumbani licha ya kwamba mji huo wote unatekeleza hatua ya kutoka nje kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi kumi na mbili asubuhi.
"Najua machungu yenu, najua mumevunjika moyo," Trump alisema. "Lakini lazima sasa murejee nyumbani, lazima tuwe na amani ... hatutaki yeyote ajeruhiwe."
Bwana Biden kwa upande wake amesema maandamano hayo "yamesababishwa na uchochezi na ni lazima hilo likome sasa", amesema.
Wanajeshi na maafisa wa polisi pia wamepelekwa katika majimbo jirani huku maafisa wa shirika la ujasusi FBI wakipelekwa katika majengo ya bunge kusaidiana na maafisa wa polisi.
Pia amethbitisha kuwa baadhi ya maafisa wanapata matibabu baada ya kujeruhiwa.
Wafuasi wa Donald Trump wenye hasira wamevuka mipaka ya usalama iliyowekwa na kusimama kandokando ya bunge huko Washington, wakati wabunge wanakutana kumuidhinisha rais mteule Joe Biden kama mshindi wa uchaguzi uliofanyika Novemba mwaka jana.
Katika matukio ya kutatanisha, waandamanaji walizunguka jengo la bunge huku wabunge nao wakisindikizwa kutoka bungeni humo na polisi.
Bwana Biden alisema huo ni "uasi", huku Bwana Trump kwa upande wake akatoa ujumbe kwa njia ya video akiwataka wafuasi wake kutoka bungeni na kurejea nyumbani.
Kikao cha pamoja cha bunge kuidhinisha ushindi wa Bwana Biden kimeahirishwa na bunge limelazimika kwenda mapumzikoni.
Kuna taarifa kuwa watu walitumia bunduki kwenye jengo hilo .Pia mabomu ya kutoa machozi yametumika kutawanya waandamanaji.
Waandamanaji walikuwa wanalenga nini?
Kikao maalum cha bunge kilikuwa kinaendelea kuidhinisha ushindi wa Bwana Biden katika uchaguzi wa Novemba 3.
Kawaida vikao kama hivyo huwa vinachukua muda mfupi sana na vyenye kufurahiwa lakini wabunge wa Republican wamekuwa wakipinga baadhi ya matokeo ya uchaguzi.
Kwa siku kadhaa sasa Bwana Trump amekuwa akimshinikiza Bwana Pence, ambaye anaongoza kikao hicho, kuzuia uidhinishaji wa matokeo hayo.
Lakini katika barua iliyoandikiwa bunge Jumatano, Bwana Pence alisema hana "mamlaka ya moja kwa moja ya kuamua ni kura gani za wajumbe zitahesabiwa".
Waandamanaji walifika katika majengo ya bunge kutoka kwa mkutano uliopewa jina la "Save America Rally", ambapo Bwana Trump aliwataka wafuasi wake kuunga mkono wabunge wanaopinga kuidhinishwa kwa Biden kama mshindi.
Bwana Trump alikataa ukubali kuwa ameshindwa katika uchaguzi wa Novemba 3 na kudai mara kadhaa kwamba uchaguzi huo ulikumbwa na wizi wa kura bila kutoa ushahidi wowote.
Jumatano Trump alisema tena: "Hatutachoka. Hatutakubali kuwa tumeshindwa."
Pia ameonesha kutilia shaka uchaguzi wa marudio uliofanyika Jumanne katika jimbo la Georgia.
Katika ubashiri wa jinsi matokeo yalivyo kwenye uchaguzi huo wa marudio kulingana na vyombo vya habari vya Marekani, inaonekana chama cha Democrats kimeshinda kiti kimoja huku washindani wakikaribiana mno katika kiti kilichosalia.
Ikiwa Democrats itashinda viti vyote, Bwana Biden atakuwa na udhibiti wa bunge la Seneti na hilo litasaidia kupitisha ajenda zake baada ya kuapishwa rasmi kama rais wa Marekani Januari 20.
Viongozi duniani walaani uvamizi wa bunge Marekani
Kitendo hicho kimelazimisha kuahirishwa kwa muda kikao maalum cha kumuidhinisha Biden mshindi.
Viongozi wengi wametoa wito wa amani na ubadilishanaji wa madaraka kwa njia ya utulivu, wakielezea uvamizi uliotokea kama wenye "kuogofya na uvamizi wa demokrasia".
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, amelaani kitendo hicho na kusema ni "aibu".
"Marekani inasimamia demokrasia kote duniani na ni muhimu sana kuwa na ubadilishanaji wa madaraka kwa njia ya amani na wenye mpangilio," ameandika kwenye mtandao wa Twitter.
Viongozi wengine wa kisiasa Marekani wamekosoa ghasia hizo huku kiongozi wa upinzani Sir Keir Starmer akitaja kitendo hicho kama "uvamizi wa moja kwa moja wa demokrasia".
Wazriri wa kwanza wa Scotland Nicola Sturgeon ameandika kuwa kinachotokea bungeni "kinatia hofu mno".
Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sánchez amesema: "Nina imani na demokrasia ya Marekani. Uongozi wa rais mpya Joe Biden utakabiliana na kipindi hiki kigumu, kuunganisha watu wa Marekani."
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amelaani kitendo hicho na kusema ni "uvamizi mbaya dhidi ya demokrasia", huku mwenzake wa Ujerumani, Heiko Maas, akisema bwana Trump na wafuasi wake "lazima wakubali uamuzi wa wapiga kura wa Marekani na waache kutatiza demokrasia".
Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel amesema kuwa aliamini sana Marekani "katika kuhakikisha ubadilishanaji wa madaraka kwa njia ya amani" kwa Bwana Biden, na Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema ana matarajio makubwa ya ushirikiano na chama cha Democrat.
Katibu Mkuu wa Nato Jens Stoltenberg aliungana na wale waliosema matokeo ya uchaguzi ni lazima yaheshimiwe.
Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau amesema raia wake "wamehuzunishwa sana na kitendo hicho cha uvamizi wa demokrasia".
No comments :
Post a Comment