Monday, January 4, 2021

WAKAZI WA NYASA WASHUKURU UKAMILISHWAJI WA UJENZI WA BARABARA

*******************************************

Na Muhidin Amri,
Nyasa

WAKAZI wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, wameshukuru kukamilika kwa ujenzi wa

barabara ya lami kutoka Nyasa hadi Mbinga yenye urefu wa km 66 inayojengwa na kampuni ya Chico ya nchini China.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema, kukamilika kwa barabara hiyo kunakwenda kumaliza  changamoto ya mawasiliano kati ya wilaya hizo mbili na kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi  kwa kwao.

Wamesema, uthubutu uliofanywa na serikali ya awamu ya tano kujenga barabara hiyo ni kati ya mambo mengi mazuri yaliyofanyika  katika kipindi cha pili cha serikali ya awamu ya tano na sehemu ya kufungua fursa kiuchumi na ukuaji wa wilaya ya Nyasa ambapo Serikali  imeweka alama  ya kihistoria kwa vizazi vijavyo.

Wamesema, barabara hiyo ni kama zawadi kutoka kwa Serikali ya Rais Dkt John Magufuli kwa wananchi wa wilaya hiyo, ambao kwa muda mrefu walikuwa katika mateso makubwa kwa kukosa mawasiliano ya barabara ya uhakika.

Mbunge wa jimbo la Nyasa Stella Manyanya alisema, kabla ya ujenzi wa barabara ya lami walikuwa wanatumia kati ya saa 12 hadi 16 kwenda Mbinga, lakini baada ya kukamilika kwa sasa wanatumia  saa 1 hadi 1.30 kufika wilaya jirani ya Mbinga na masaa matatu kufika makao makuu ya mkoa  Songea.

“kwa kweli namshukuru sana Rais Dkt John Magufuli kujenga barabara hii,kwa niaba ya wananchi wa wilaya ya Nyasa nasema asante sana,hakika ametutendea jambo kubwa katika historia ya wilaya yetu”alisema.

Aidha Manyanya,  ameipongeza wizara ya ujenzi kwa kuipa kazi  kampuni ya China Henan International Cooperation  Group Co Ltd (Chico)kujenga barabara hiyo  kwa viwango vya hali ya juu,kukamilisha  ujenzi kwa wakati na kuwataka wananchi kuitunza ili ilete manufaa na kuharakisha maendeleo kwa kizazi cha sasa  na baadaye.

Alisema, ujenzi wa barabara hiyo kunaifanya wilaya ya Nyasa kuwa kitovu cha mawasiliano kwa wilaya na mikoa mingine hapa nchini na kutoa fursa  kwa wananchi kufanya shughuli mbalimbali  ikiwemo kusafirisa mazao ya kilimo,samaki na dagaa  ambao wanapatikana kwa wingi katika ziwa nyasa.

Amewataka wananchi wa Nyasa kuitumia barabara hiyo  kama kichocheo cha kukuza kipato na kuondokana na umaskini, hasa ikizingatia  bado kuna fursa nyingi ambazo kama zitatumika vizuri wilaya hiyo itakuwa  mfano wa kuigwa kimaendeleo hapa nchini.

Amewaomba wadau mbalimbali kwenda Nyasa kwa ajili ya kuwekeza  miradi mbalimbali ya kiuchumi, kufuatia wilaya hiyo kuanza kufunguka kwa kuwepo miundombinu ya uhakika kama meli na barabara ya lami.

Fidelix Duwe alisema, barabara hiyo ni ukombozi mkubwa kiuchumi  na itafungua fursa  mbalimbali kwa wananchi  na fahari kubwa kuona  ujenzi wa barabara hiyo umekamilika kwa wakati  sambamba na kuanza kwa safari za meli tatu katika ziwa Nyasa.

Kwa mujibu wake, barabara hiyo ina faida lukuki  ikiwemo jamii ya wavuvi  ambao watauza samaki moja kwa moja kutoka Nyasa kwenda  katika  masoko mbalimbali ya Mbinga na makao makuu ya mkoa mjini Songea.

Hivyo, watazidi kupanua wigo  wa biashara ikilinganisha na siku za nyuma ambapo walishindwa kufikisha  samaki,dagaa na mazao mbalimbali  kwa wakati muafaka na wakati mwingine kuharibika njiani kabla ya kuwafikia walaji.

Duwe ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Nyasa,ameipongeza kampuni ya Chico kutokana na uwezo mkubwa kujenga barabara kwa ubora wa hali ya juu na ameiomba Serikali kuhakikisha inashirikiana na kampuni ya Chico  kwa kuipa  kazi ya ujenzi wa miradi  katika mikoa mbalimbali ambayo bado haijaunganishwa kwa barabara za lami.
MWISHO.

 

No comments :

Post a Comment