Thursday, January 14, 2021

WADAU WA TANZANITE WAMFAGILIA WAZIRI BITEKO

Waziri wa Madini Dotto Biteko (kushoto) akizungumza na Mkurugenzi wa kampuni ya Franone Mining and Gems Ltd Onesmo Mbise alipofanya ziara kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.

Mdau wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Ambrose Ndege akizungumza kwenye mkutano na Waziri wa Madini Dotto Biteko.
*******************************************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
Wadau wa madini yaq Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wanaojihusisha na uchimbaji madini (WanaApolo) na wachuuzi wa madini hayo wamempongeza Waziri wa madini Dotto Biteko kwa kutoa ruhusa ya kuuza madini ya Tanzanite bila kuwa na leseni.
Hatua hiyo imetokea kwenye machimbo ya Tanzanite baada ya Waziri Biteko kutoa ruhusa hiyo Januari 13 kwenye mkutano wake na madalali wa madini ya Tanzanite, wachuuzi na WanaApolo katika eneo la Dodoma kitalu B (Opec).
Waziri huyo amesema kwenye eneo la madini ya Tanzanite hakuuzwi karanga hivyo mtu yeyote akiwa na madini hayo hapaswi kuulizwa ameyatoa wapi ila akitaka kutoka nayo nje ya ukuta unaozunguka madini hayo anapaswa kupata kibali baada ya kufanyiwa tathimini.
Amesema wachuuzi na WanaApolo wana haki ya kuuza madini waliyopata bila kuulizwa leseni kwa saba hawana leseni na imekuwa changamoto kwao.
Hata hivyo, amesema utaratibu wa kila Tanzanite inayopatikana kufungiwa lakiri (seal) utabadilishwa na kupata kibali kinachoonyesha kiwango cha madini kilichopo hadi sokoni na ili mradi wadau hao wahakikishe wanaachana na utoroshaji na wanalipa kodi na Serikali inapata mapato yake.
Pia, amewataka wadau wa madini ya Tanzanite kuwa wazalendo kwa kuhakikisha wanashiriki kupiga vita utoroshwaji wa madini hayo kwa kutoa taarifa ili uhalifu hiyo umalizike.
“Pamoja na hayo nampongeza dada yangu Rachel Njau Katibu wa Marema Tawi la Mirerani kwa kuwapatia WanaApolo elimu ya ulipaji kodi na kutotorosha madini,” amesema Waziri Biteko.
Hata hivyo, Waziri Biteko akizungumza juu ya kufungwa kwa madini hayo na lakiri (seal) ambayo imelalamikiwa na wadau hao wa madini amesema haitatumika badala yake watahitaji kupata kibali kinachoonesha kiwango cha madini kinapotoka hadi kwenye soko halisi. 
“Ofisa madini mkazi (RMO) anafuata sheria na sisi kama Serikali tumekuwa tukidhibiti utoroshwaji wa madini kupitia taasisi zetu lengo likiwa kuifanya sekta hii iwanufaishe wadau walio katika mnyororo wa thamani huku serikali ikipata mapato yake,” amesema Waziri Biteko.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amemuomba Waziri Biteko kuhakikisha mchakato wa ujenzi wa jengo kubwa zaidi la ukaguzi lijengwe ili wadau wa madini wapekuliwe kwa urahisi na pia wapate sehemu ya kupumzika wakisubiri kufanyiwa upekuzi. 
“Pamoja na hayo bado kuna changamoto ya madini kufungwa lakini (seal) hili ni tatizo lingine kwani linachelewesha mchakato wa uuzaji na ununuzi kwa kila jiwe kutakuwa kufungwa kwa lakiri,” amesema Ole Sendeka.
Mdau wa madini Ambrose Ndege amesema suala la wanaApolo kupekuliwa na mameneja na wamiliki wa madini linapaswa kupigwa vita kwani hawalipwi mshahara.
“Mmiliki na meneja huwa wanadhibiti madini yao pindi uzalishaji ukishatoka ndipo wanaApolo huachiwa kupiga ukware na kupekuapulekua ili wapate sasa hiki kitendo cha mameneja na wamiliki kuwasachi siyo sahihi kwani siyo kila mtu kwenye madini anapata, mimi nilikuja miaka 15 iliyopita sasa hivi nina mvi na sijapata,” amesema Ndege.
Mdau mwingine John Ndossy amesema Serikali iweke mashine ya kuwapekua kwani utaratibu wa sasa wa kupekua unadhalilisha utu wao.
“Tanzanite ni baraka kwetu sasa isiwe laana kwa sisi kudhalilishwa na kuporwa utu wetu kwani Tanzanite haina thamani ya utu wetu Serikali iweke mashine ya kuwapekua kwani utaratibu wa sasa siyo rafiki,” amesema.

 

No comments :

Post a Comment