Jane Edward, Michuzi TV,Arusha.
Shirika la ndege la Air Tanzania limerejesha safari zake rasmi za kuja mkoani Arusha kupitia kiwanja cha ndege cha Arusha ikiwa na malengo ya kutangaza utalii na kusogeza huduma karibu kwa wateja.
Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea ndege hiyo katika kiwanja cha ndege wa Arusha,Meneja wa shirika la ndege la Air Tanzania Kanda ya kaskazini, Estermary Karumbo alisema kuwa, kwa muda mrefu walisitisha huduma kupitia kiwanja hicho kutokana na changamoto mbalimbali ila kwa sasa wamerudi rasmi.
Alisema kuwa,uwepo wa safari hiyo utasaidia sana kukuza utalii na kuweza kurahisisha huduma ya usafiri kwa wateja wao ,badala ya kwenda kupandia kiwanja cha Kia ambapo wanatumia muda mrefu wataweza kutumia kiwanja hicho kwa muda mchache.
"Tunamshukuru sana Rais Magufuli pamoja na serikali yetu kwa juhudi kubwa walizofanya za kuhakikisha tunarudisha tena huduma katika kiwanja cha ndege Arusha ,ambapo ndege yetu itakuwa inatoka Arusha kupitia Zanzibar kwenda Dar es Salaam ,ambapo ni fursa Sasa kwa wafanyabiashara wetu wa mizigo kuutumia uwanja huu kusafirisha bidhaa badala ya kutumia uwanja wa Kia ili kuokoa muda ."alisema Karumbo.
Naye Meneja wa kiwanja Cha ndege Cha Arusha ,Injinia Elipid Tesha alisema kuwa,wanashukuru Sana kwa shirika hilo kurudisha huduma zake katika uwanja huo kwani inatoa fursa kubwa ya kutangaza utalii sambamba na kuokoa muda kwa watumiaji wake.
Alisema kuwa,wameweza kufanya maboresha mbalimbali ya uwanja huo kwa kipindi Cha mwaka wa fedha 2019/2020 na 2020/2021 katika ukarabati was kiungo Cha kuingilia barabara ya kurukia ndege kwa kiwango cha lami ,ambapo kiungo hicho kinatumika Sana hasa hasa na ndege kubwa Kama ATR 72 na Bomberdier.
Naye Rubani wa ndege kutoka shirika la Air Tanzania , Captain Michael Lengaram alisema kuwa,ni furaha kubwa Sana kwao kutua tena katika kiwanja hicho Cha Arusha baada ya kusitisha muda mrefu na hivyo historia imeweza kuandikwa tena ,hivyo wanawakaribisha sana abiria wao kuweza kukitumia tena kiwanja hicho.
No comments :
Post a Comment