Tuesday, January 26, 2021

SERIKALI YAWAONYA MAWAKALA WAKUBWA WA MAFUTA WANAOPANDISHA BEI KIHOLELA


 Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma leo.

 Charles James, Michuzi TV
SERIKALI imewaonya mawakala wakubwa wa mafuta watakaopandisha bei ya mafuta kinyume na bei ambayo ni ya kiwanda na watakaobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo

kufutiwa leseni zao za biashara.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe alipokua akizungumza na wandishi wa habari juu ya mfumuko wa bei ya mafuta ambao umekua mkubwa kwa siku za  hivi karibuni.

Waziri Mwambe pia ametoa maelekezo kwa Tume ya Ushindani kuhakikisha wanafuafitilia mwenendo wa mafuta nchini huku akiwataka kumuandalia ripoti ya hali ya bidhaa hiyo nchini.

Amesema kwa sasa changamoto ya mafuta nchini haipo kwani yapo ya kutosha baada ya kuwasili kwa meli mbili ndani ya kipindi cha mwezi mmoja ambazo zimeshusha mafuta takribani Tani 48,000 na uhitaji ukiwa ni mafuta Tank 30,000 kwa mwezi huki akisema changamoto itakayoendelea kwa muda mfupi ni ongezeko la bei kwani mafuta yanayowasili tayari waagizaji walishaagiza kwa bei hii ambayo imepanda duniani kote.

" Kwa sasa changamoto itakayokuepo ni ya bei na tayari tumeshawapunguzia waagizaji baadhi ya gharama za kushusha mafuta pale bandarini lakini pia niwahakikishie watanzania uhaba wa mafuta hauwezi kuwepo kwani Februari 17 kuna meli ya mafuta itawasili na nimeagiza isichukue muda mrefu kushusha pale bandarini hadi Februari 20 meli hiyo iwe imeshashusha mafuta.

Niwaombe watanzania na hasa vijana kuona hii kama fursa ya kujipatia kipato, haiwezekani tuwe na uhaba wa mafuta ilihali Nchi yetu ina ardhi ambayo inakubali kilimo cha mazao ya mafuta, wajiunge kwenye vikundi vidogo vidogo wapatiwe mikopo ile ya kwenye Halmashauri na wajikite kwenye kilimo hiko," Amesema Waziri Mwambe.

Pia ametoa wito kwa Wakuu wa Mikoa ambao mikoa yao inakubali kilimo cha michikichi, alizeti na karanga na mazao mengine ya mafuta kuhamasisha Wananchi wao kujikita kwenye kilimo hicho ili kuweza kujikwamua kiuchumi wao wenyewe lakini pia kuzalisha mbegu ambazo zitatumika na viwanda vya ndani na kupunguza gharama za uagizaji mafuta nje ya Nchi.

No comments :

Post a Comment