![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2021/01/nte-1-620x308-1.jpg)
………………………………………………………………………………
Na Alex Sonna, DODOMA
SERIKALI imetumia Sh.Bilioni 16.4 kukarabati miundombinu ya shule za ufundi za sekondari zilizopo kwenye mikoa tisa nchini.
Kufuatia uboreshaji
huo, Wakuu wa Mikoa tisa wametakiwa kuhakikisha wanakuwa walezi wa shule
hizo ili zitoe vijana wenye umahiri wa kutosha na wabobezi kwenye vitu
mbalimbali.
Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo,
ametoa agizo hilo leo Januari 22,2021 alipokuwa akizungumza na Wakuu
hao kwa njia ya ‘video conference’, Jijini Dodoma.
Amefafanua kuwa Shule
sekondari ya ufundi ya Bwiru ilipewa Sh.Milioni 825, Chato Sh.Bilioni
3.9, Ifunda Sh.Bilioni 3.6, Iyunga Sh.Bilioni 1.01, Moshi Sh.Bilioni
2.1, Mtwara Sh.Bilioni 1.3, Musoma Sh.Bilioni 1.2, Mwadui Sh.Milioni 226
na Tanga Sh.Bilioni 2.1.
Waziri Jafo amesema
kuwa wakuu hao wa mikoa wenye shule hizo wanapaswa kuzitembelea na
kuzungumza na walimu ikiwa ni pamoja na waajiriwa wapya ili kueleza kwa
mapana mikakati ya serikali ya kuinua ubora wa shule hizo.
Aidha, amesema jumla ya Sh.Milioni 30 zimetengwa
kwa Kila shule kwa ajili ya ununuzi wa mitambo na vifaa vya kufundishia
na kujifunzia katika shule zote hizo za ufundi za sekondari za
serikali.
“Baada ya Rais John
Magufuli kutangaza na kutoa dira ya kuelekea uchumi wa viwanda mwaka
2016, Ofisi ya Rais Tamisemi ilichukua hatua mbalimbali ili kufanya
maandalizi ya wataalamu ambao baadae watatumika katika viwanda
vinavyoendelea kujengwa nchini,”amesema.
Amesema wataalamu
hao watatoka katika shule hizo za sekondari za ufundi ambapo hatua
zimechukuliwa ili kuimarisha utoaji wa elimu ya ufundi na kuifanya
iendane na mahitaji na ushindani katika ulimwengu wa ajira ili kuongeza
pato la mwananchi wa taifa kwa ujumla.
Amesema ili
kuhakikisha ufundishaji na ujifunzaji katika shule hizo Novemba mwaka
2020, Serikali iliajiri walimu 150 wa masomo ya ufundi wa fani
mbalimbali kwa wastani wa walimu 16.
Ametoa wito kwa wakurugenzi watendaji wa Halmshauri wenye shule hizo kuhakikisha miundombinu na vifaa vinatunzwa.
No comments :
Post a Comment