Rais wa Ethiopia Bi. Sahle-Work Zewde.
**
Mheshimiwa
Sahle-Work Zewde, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la
Ethiopia anatarajia kufanya ziara ya kikazi ya siku moja nchini Tanzania
Jumatatu ya tarehe 25 Januari, 2021 kwa mwaliko wa mwenyeji wake,
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Mheshimiwa
Sahle-Work Zewde anatarajiwa kuwasili katika uwanja wa ndege wa Chato
majira ya saa 4:00 asubuhi na kupokelewa na mwenyeji wake Mhe. Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli. Baada ya mapokezi hayo ya Kitaifa, Mheshimiwa
Zewde ataendelea na ratiba nyingine zitakazokuwa zimepangwa ikiwemo
kufanya mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake.
Lengo
la ziara hiyo ni kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizi
mbili pamoja na kubadilishana mawazo juu ya masuala mbalimbali ya
kikanda na kimataifa yenye maslahi kwa nchi zote mbili.
Profesa
Palamagamba John Kabudi (Mb) Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki akizungumza na waandishi wa habari Chato, Mkoani Geita
ameeleza kuwa, Tanzania na Ethiopia zimeendelea kuwa na uhusiano na
ushirikiano mzuri wa muda mrefu. Uhusiano huo unatokana na msingi mzuri
uliowekwa na Waasisi wa nchi hizi, Hayati Mwalimu Julius Nyerere wa
Tanzania na Hayati Haile Sellasie wa Ethiopia ambao walishirikiana
katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika na uanzishwaji wa Jumuiya
ya Umoja wa Afrika (Organization of African Unity -OAU) mwaka 1963.
Profesa
Kabudi aliendelea kueleza kuwa Tanzania na Ethiopia zimeendelea
kushirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo kukuza lugha ya
Kishwahili,uwekezaji, biashara, utalii, ulinzi na usalama, na usafiri wa
anga. "Mwaka 2017, nchi hizi zilisaini Hati ya Makubaliano ya
Ushirikiano (MoU) ya kuanzisha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (Joint
Permanent Commission of Cooperation-JPCC), Azimio la Pamoja la Mkakati
wa Ushirikiano kati ya Tanzania na Ethiopia (Joint Declaration on
Strategic Partnership between Tanzania and Ethiopia); na Mkataba wa
Ushirikiano katika Sekta ya Utalii (Cooperation in Tourism) ambayo
utekelezaji wake unaendelea vizuri". alieleza Profesa Kabudi.
Mashirikiano
mengine baina ya Nchi hizi mbili ni pamoja na sekta ya
Utalii,uchukuzi,ulinzi na Usalama, utamaduni pamoja na viwanda.
Takwimu
za biashara kati ya Tanzania na Ethiopia zinaonesha ongezeko la kiwango
cha biashara (Trade Volume) kati ya nchi hizi mbili. Mathalan kiwango
cha biashara kiliongezeka kutoka Bilioni 1.5 mwaka 2012 hadi Bilioni 9.3
mwaka 2014 na kufikia Bilioni 13.5 mwaka 2019. Urari wa Biashara
(Balance of Trade) uliongezeka kutoka Milioni 946.8 mwaka 2012 hadi
Bilioni 12 mwaka 2019.
Aidha,
taarifa ya Profesa Kabudi kwa waandishi wa habari imeeleza kuwa Kituo
cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi 13 yenye thamani ya Dola
za Marekani Milioni 14. 57 kutoka nchini Ethiopia katika kipindi cha
kuanzia mwaka 1990 hadi mwaka 2020. Miradi hiyo imezalisha ajira 677 kwa
Watanzania na ipo katika sekta za viwanda (manufacturing), ujenzi,
uchukuzi na Utalii.
Tanzania
ilifungua Ubalozi wake nchini Ethiopia tangu mwaka 1963, Ubalozi huo
pia unaiwakilisha Tanzania katika Umoja wa Afrika. Kwa kutambua umuhimu
wa uhusiano wetu, Ethiopia nayo ilifungua Ubalozi wake hapa nchini mwezi
Mei, 2018.
No comments :
Post a Comment