Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itaendelea kufanya kazi kwa karibu na uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) katika kuhakikisha amana zote za wananchama zinasimamiwa ipasavyo, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali
Mwinyi akikata utepe kulifungua jengo jipya la Ofisi za ZSSF Tibirizi
“Hifadhi Building” Chakechake Pemba na (kulia kwa Rais) Makamu wa Kwanza
wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Maalim Seif Sharif Hamad, ikiwa ni
shamrashamra za kusherehekea miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar.(Picha na
Ikulu/ Diramakini).
Rais
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Januari 5, 2021 katika hotuba yake ya
ufunguzi wa jengo jipya la “Hifadhi Building” la (ZSSF) lililopo
Tibirinzi, Wilaya ya Chake Chake , Mkoa wa Kusini Pemba, ikiwa ni
miongoni mwa shamrashamra za sherehe za miaka 57 ya Mapinduzi matukufu
ya Zanzibar ya mwaka 1964 ambapo pia, Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim
Seif Sharif Hamad alihudhuria.
Katika
hotuba hiyo Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, ni jukumu la Serikali
kuhakikisha inachukua hatua zionazofaa na kwa wakati katika kuhakikisha
mfuko huo unaendelea kuimarika, unaongozwa na kusimamiwa na viongozi
walio makini na wanaojiepusha na vitendo vya ubadhirifu, rushwa na wizi.
Amesisitiza
kwamba, Serikali itahakikisha wanachama wa mfuko huo wanaishi bila kuwa
na wasiwasi wa hatma ya amana wanayowekeza ambayo mara nyingi huwa
nitegemeo kubwa katika maisha ya wafanyakazi baada ya kustaafu.
Amesema
kuwa, ni lazima viongozi wa ZSSF wahakikishe kwamba utekelezaji wa
dhamira njema ya kutumia amana ya wanachama wa mfuko wanayokusanya
iambatane na mipango imara ya kusimamia uwekezaji huo.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk. Hussein Ali
Mwinyi akiondoka katika viwanja vya Jengo Jipya la Ofisi za ZSSF la
Hifadhi Building, baada ya kulifungua ikiwa ni shamrashamra za sherehe
za miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar na kulia kwa Rais ni Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad na kushoto kwa
Rais ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe.
Jamal Kassim Ali.(Picha na Ikulu/Diramakini).
Aidha,
Rais Dkt. Mwinyi amewataka viongozi kuhakikisha kwamba fedha
inayowekezwa inazalisha na shughuli zote za uendeshaji wa taasisi hiyo
zinafanywa kwa weledi, umahiri na umakini mkubwa.
Rais
Dkt. Mwinyi amesisitiza kwamba uongozi ni lazima kila wakati uhakikishe
kwamba idadi ya fedha zinazohitajika kulipa stahiki za wanachama
wanaostaafu na mafao mbalimbali zinakuwepo kila wakati bila ya nenda
rudi na usambufu wa aina yoyote ile.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali
Mwinyi akimsikiliza Mjenzi wa Jengo la Ofisi za ZSSF Hifadhi Building
lililopo katika eneo la Tibirinzi Chakechake Pemba Mkurugenzi wa Kampuni
ya Quality Building Contractor, Ndg. Khamis Haji akitoa maelezo ya
ujenzi huo wakati wa ufunguzi uliofanyika Januari 5, 2021 na kulia kwa
Rais ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Maalim Seif Sharif
Hamad na kushoto kwa Rais ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na
Mipango Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali.(Picha na Ikulu/ Diramakini).
Amesema kuwa, kuwepo kwa majengo ya ofisi za kisasa ni hatua muhimu katika juhudi hizo za kuvutia wawekezaji kisiwani Pemba.
Rais
Dkt. Mwinyi amesema kuwa, kazi kubwa imefanywa na Serikali ya Awamu ya
Saba ya kuimarisha mazingira ya kufanya kazi kisiwani Pemba ambapo
majengo mengi ya serikali yamejengwa na mengine yamefanyiwa matengenezo
makubwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Katika
hotuba yake hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amewahimiza viongozi wa ZSSF
kuhakikisha taratibu za ukodishaji wa maduka yaliyomo katika maduka
mapya ya Michenzani Mall na jengo la Thabit Kombo kwani ni kipindi
kirefu tangu majengo hayo yalipozinduliwa rasmi.
Sambamba
na hayo, Rais Dkt. Mwinyi alitoa pongezi kwa wakandarasi wa ujenzi wa
jengo hilo Kampuni ya kizalendo ya Quality Building Contractor pamoja na
kampuni ya Arqes Africa kwa kazi kubwa waliyoifanya.
Rais
Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kutoa pongezi za dhati kwa uongozi wa
Wizara ya Fedha, uongozi wa ZSSF pamoja na Kamati ya Sherehe na
Maadhimisho ya Kitaifa kwa maandalizi mazuri ya shughuli hiyo na kwa
kumualika kuwa mgeni rasmi.
Amesisitiza
kwamba ni jukumu la kila mwananchi wa Zanzibar kuendelea na kudumisha
fikra njema za waasisi wa nchi wakiongozwa na Marehemu Mzee Abeid Amani
Karume.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali
Mwinyi na kushoto kwa Rais Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
Mhe.Maalim Seif Sharif Hamad wakimsikiliza Meneja Mipango Uwekezaji na
Utafiti wa ZSSF, Ndg. Abdulazizi Ibrahim Iddi akitoa maelezo wakati wa
kutembelea moja ya nyumba iliyopo katika jengo la Ofisi za ZSSF “Hifadhi
Building “ baada ya kulifunga leo Januari 5, 2021 ikiwa ni shamrashamra
za kusherehekea miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar.(Picha na Ikulu/
Diramakini).
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Jamal Kassim Ali alisema kuwa,
kukamilika kwa ujenzi huo ni mafanikio makubwa kwani itaongeza ufanisi
na mapato.
Amesema
kuwa, kukamilika kwa jeno hilo kunatokana na ushirikiano wa Mfuko wa
ZSSF, Wizara na Bodi ya Mfuko huo sambamba na ushauri mkubwa uliokuwa
ukitolewa na Rais juu ya Mfuko huo huku akieleza haja kwa taasisi za
Serikali kuwa makini katika kutekeleza miradi kama hiyo ikiwa ni pamoja
na kufanya tathmini ya miradi kabla ya ujenzi wake.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe.Jamal Kassim Ali
akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi kuzungumza na wananchi
wa Pemba wakati wa hafla ua ufunguzi wa Ofisi za ZSSF Tibirinzi
Pemba.(Picha na Ikulu/ Diramakini).
Ameeleza
kwamba, fedha zliozotumika ni michago ya wanachama wa ZSSF hivyo, ni
vyema zikarudi na kupata tija kwa wanachama wa mfuko huo huku akiwataka
wale wote watakao kodi jengo hilo wanapaswa kulipa fedha zinazotakiwa.
Nae
Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Khamis Mussa
Omar alisema kuwa, kwa bahati mbaya ZSSF Tawi la Pemba awali ilikuwa
ikitoa huduma zake katika maeneo ya kukodi katika majengo ya watu
binafsi, ofisi za kudumu zilianzishwa mwaka 2004 katika jengo lake la
Kituo cha Mikutano (Pemba Conference Centre) ambalo pia, linatoa huduma
za malazi afisi ambayo ilikuwa ndogo sana.
Hivyo,
ZSSF iliamua kujenga jengo hilo jipya la kisasa linaloendana na
mahitaji ya sasa na hapo baadae ambapo mkataba wa ujenzi ulitiwa saini
tarehe 4 Julai 2019 baina ya ZSSF na Kampuni ya Kizalendo ya Quality
Building Contractors baada ya Kampuni hiyo kuwa mshindi wa zabuni.
Kufuatia
kusainiwa kwa mkataba huo, ujenzi ulianza rasmi tarehe 1 Agosti 2019
ambao ni mradi uliokuwawa miezi 12 na ulitarajiwa kukamilika tarehe 31
Julai,2020 lakini kutokana na changamoto zilizobainika wakati wa ujenzi
na athari ya maradhi ya COVID 19 lakini hata hivyo, ujenzi ulikamilika
rasmi Oktoba 2020.
Mapema
Rais Dkt. Mwinyi mara baada ya kulifungua jengo hilo alipata fursa ya
kulitembelea na kupata maelezo kutoka kwa uongozi wa ZSSF pamoja na
maelezo kutoka kwa Mkandarasi wa jengo hilo Khamis Ali kutoka Kampuni ya
Quality Building Contractor Limited.
Kwa
maelezo ya uongozi wa ZSSF jengo hilo la ghorofa tatu limegharimu jumla
ya sh. Bilioni 7.9 zimetarajiwa kutumika katika ujenzi wa jengo hilo
ambapo hadi sasa jumla ya sh.Bilioni 5.3 ameshalipwa mjenzi huku mjenzi
huyo mzalendo akitoa shukurani kwa Rais kwa Dkt. Mwinyi kuwapa
kipaumbele wajenzi wazalendo.
Wakati
huo huo, Rais Dk. Mwinyi ametembelea ujenzi wa barabara unaoelekea
katika maeneo huru ya vitega uchumi Micheweni na kufika eneo la
Maziwangombe na kuwaeleza wananchi wa Micheweni kwamba fursa za ajira
zitakapoanza wao watapewa kipambele.
Amewataka
wakuu wa mikoa na wilaya kwa kila wilaya kutafuta maeneo ya uwekezaji
huku akisisitiza kwamba kuna haja ya eneo hilo la Micheweni kuweka
viwanda vinavyohusiana na uchumi wa buluu zaidi kutokana na mazingira
yake.
Rais
Dkt. Mwinyi ameeleza haja ya kusogezwa kwa huduma nyingine muhimu
zikiwemo maji na umeme ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kurahisisha
uwekezaji katika eneo hilo na kuwataka wizara husika kupanga na kuweka
fedha kwa ajili ya mchakato huo.
Amesema,
miezi minane kwa barabara ya kilomita 2.8 iliyoelezwa na wajenzi wa
barabara hiyo kutoka uongozi wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi ni
mingi sana na kuutaka wapunguze ili shughuli ziweze kuendelea.
Amesisitiza
kwamba ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni zitafanyiwa kazi huku
akieleza haja ya kujengwa barabara yote badala ya kujengwa eneo hiyo ya
ambayo ujenzi wake unaendelea hivi sasa.
Ameeleza
azma ya Serikali ya kuweka viwanda katika eneo hilo kwa ajili ya kupata
ajira zikiwemo zile ajira 300,000 zilizoelezwa katika Ilani ya uchaguzi
ya CCM ya 2020-2025 ili nyingine zitoke katika eneo hilo huku
akiwapongeza wananchi wa Micheweni kwa kuupokea mradi huo.
Mapema
Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Maendeleo ya Uwekezaji (ZIPA), Shariff Ali
Shariff amemueleza Rais, Dkt. Mwinyi mipango na mikakati iliyowekwa na
ZIPA juu ya eneo hilo la uwekezaji.
Nae
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib kwa niaba ya
wananchi wa Micheweni ametoa shukurani kwa Rais Dkt. Mwinyi kwa uamuzi
wake wa kuijenga barabara hiyo na kusema kwamba wananchi wamefarijika.
No comments :
Post a Comment