Mbunge wa Jimbo la
Kiteto Mkoani Manyara, Edward Ole Lekaita (katikati aliyevaa kofia)
akikagua eneo la chanzo cha maji kwenye Kata ya Dongo.
Mbunge wa Jimbo la
Kiteto, Mkoani Manyara, Edward Ole Lekaita (wapili kushoto) akipanda
mlima umbali wa mita 2,200 usawa wa bahari ili kukagua chanzo cha maji
kwenye Kata ya Dongo.
………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Kiteto
MBUNGE wa Jimbo la
Kiteto Mkoani Manyara, Edward Ole Lekaita amelazimika kupanda mlima
wenye urefu wa mita 2,200 kwa kutembelea kwa miguu umbali wa kilomita
tano ili kukagua chanzo cha maji kwenye Kata ya Dongo ambapo wananchi
wana changamoto ya maji.
Ole Lekaita
ametembelea eneo hilo akiwa kwenye ziara yake ya kutembelea wananchi na
kubaini changamoto na kuona mafanikio chanya ya wapiga kura wa jimbo
lake.
Amesema alilazimika
kupanda kutembelea eneo hilo la chanzo cha maji ambapo kutajengwa bwawa
kubwa la maji litakalohudumia binadamu na mifugo wa kata za Dongo na
Laiseri.
Amesema kero ya maji
imekuwa sugu kwa wananchi wa eneo hilo hivyo amefika ili aweze kuona
namna ya wananchi wataondokana changamoto hiyo.
“Mradi wa bwawa hili
kubwa utakapokamilika utasaidia wananchi wa kata za Dongo na Laiseri
ambazo zipo pembezoni na zina uhitaji makubwa wa maji,” amesema Ole
Lekaita.
Amesema amewasiliana
kwa njia ya simu na meneja wa mamlaka ya maji vijijini (Ruwasa) wa
wilaya ya Kiteto ambaye amemuhakikishia ndani ya wiki moja atatembelea
mradi huo.
“Nitakutana na meneja
wa Ruwasa ili tuweze kuboresha mradi na wananchi watatuliwe kero ya
maji ambayo imekuwa sugu kwa wananchi wa kata ya Dongo,” amesema Ole
Lekaita.
Hata hivyo, mkazi wa
kijiji cha Dongo, Juma Mwadimange amempongeza mbunge huyo kwa jitihada
zake za kufuatilia kero za wananchi hadi kupanda mlima na kufika kwenye
chanzo cha maji.
“Wananchi wa jimbo la
Kiteto hawakufanya makosa kumchagua Ole Lekaita kuwatumikia kwani
ameonyesha imani kubwa hadi kupanda mlima na kutembelea umbali mrefu na
kufika kwenye chanzo cha maji,” amesema Mwadimange.
Akiwa kwenye ziara ya
kata ya Dongo, mbunge huyo pia ametembelea shule ya msingi Dongo, shule
ya msingi Chang’ombe na zahanati ya Dongo na kuzungumza na wananchi wa
eneo hilo.
No comments :
Post a Comment