Monday, January 11, 2021

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO AAGIZA UCHUNGUZI GHARAMA ZA UJENZI JENGO LA UTAWALA KIWANDA CHA CHAKI MASWA

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (Mb), akiwa amembeba  Mtoto Lutimba Shoto, aliyepelekwa na ma a yake Bi. Sophia John (hayupo pichani), kupata huduma ya kliniki katika Hospitali Mpya ya Wilaya ya Bariadi iliyopo kijiji cha Dutwa, alipokuwa katika ziara ya kukagua miradi ya kimkakati inayofadhiliwa na Serikali mkoani Simiyu.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis, akisalimiana na Bi. Tano Nyakisaka, aliyemleta mtoto wake kupata huduma ya kliniki katika Hospitali ya Wilaya ya Bariadi iliyopo Kijiji cha Dutwa Mkoani Simiyu, wakati wa ziara ya kukagua miradi ya kimkakati Mkoani humo.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (Mb), akiwaasa wakina mama (hawapo pichani), waliofika katika Hospitali ya Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, kupata huduma ya mama na mtoto, kuhakikisha wanawapeleka Watoto Hospitalini hapo kila inapobidi ili kulinda afya zao, wakati wa ziara ya kukagua miradi ya kimkakati Mkoani humo. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Bw. James John.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Bw. Festo Kiswaga, akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (Mb), kuhusu mipango ya kuboresha miundombinu wezeshi hususani barabara ili wagonjwa waweze kufika katika Hospitali ya Wilaya ya Bariadi kwa urahisi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Bw. James John (kulia), akimuongoza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (Mb), kutembelea mradi wa kimkakati wa Hospitali ya Wilaya ya Bariadi uliopata fedha zaidi ya shilingi bilioni 1.9 kutoka Serikalini, ambao umeanza kutoa huduma kwa wananchi.

Muonekano wa moja ya majengo saba ya Hospitali ya Wilaya ya Bariadi, ambapo takiribani Sh. bilioni 1.9 zilitolewa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, ambapo imeanza kutumika rasmi kuanzia mwezi Aprili Mwaka 2020 ambapo tangu wakati huo zaidi ya wagonjwa 2968 wamepatiwa huduma hospitalini hapo.

Mbunge wa Maswa Mashariki, Mhe. Stansilaus Nyongo, akimuomba Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (Mb), (hayupo pichani), kusaidia upatikanaji wa fedha za kukamilisha ununuzi wa mitambo ya kutengenezea chaki  na vifungashio iliyoagizwa nchini Uturuki. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Frederick Sagamiko.

Msimamizi wa Mradi wa Viwanda vya Chaki na Vifungashio, Mhandisi Simon Salum, akitoa maelezo ya ujenzi wa Ofisi ya Utawala kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (Mb), ambayo imegharimu takribani shilingi milioni 178.4, ikiwa bado haijakamilika, wakati wa ziara ya kukagua miradi ya kimkakati Wilayani Maswa Mkoani Simiyu. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Frederick Sagamiko.

Jengo la utawala  katika mradi wa ujenzi wa Viwanda vya Chaki na vifungashio lililopo Wilayani Maswa Mkoani Simiyu litakalogharimu shilingi 178.4, ambalo Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis, hakuridhika za gharama za ujenzi wake ikilinganishwa na jengo lenyewe lilivyo na kumwagiza Mkuu wa Wialaya ya Maswa Bw. Aswege Kaminyoge, kuchunguza ujenzi huo.

Muonekano wa jengo la kiwanda cha kutengeneza Chaki,  lililoko katika eneo la  mradi wa kimkakati wa ujenzi wa Viwanda vya vifungashio na Chaki Wilayani Maswa ambao hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi bilioni 8.

(Picha na Farida Ramadhani, WFM, Simiyu)

*********************************************

Na. Farida Ramadhani na Peter Haule, Simiyu

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mwanaidi Ali Khamis, amemwagiza Mkuu wa Wilaya

ya Maswa mkoani Simiyu, Bw. Aswege Kaminyoge, kufanya uchunguzi wa gharama zilizotumika kujenga jengo la utawala la miradi ya kimkakati ya Chaki na Vifungashio wilayani humo baada ya kutoridhishwa na gharama zilizotumika ikilinganishwa na jengo hilo lilivyo.

Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis, ametoa agizo hilo Mjini Maswa, baada ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya miradi hiyo inayofadhiliwa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 8.

Alisema kuwa jingo hilo lililokamilika kwa asilimia 93 ni la kawaida sana na haliwezi kugharimu shilingi milioni 178 fedha ambazo amesema ni nyingi ikilinganishwa na thamaniya jengo hilo ambalo mpaka sasa limejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 110 kwa kutumia mfumo wa force account.

 “Tathmini ifanyike haraka na ripoti yake nipatiwe, lakini pia mkae muangalie namna ya kupunguza gharama, jengo lile haliwezi kutumia kiasi chote cha fedha hizo, lengo la Serikali ni kuzisaidia Halmashauri kujitegemea lakini sio kwa namna hii”, alisisitiza Mhe. Mwanaidi Ali Khamis.

Aidha alimuagiza Mkandarasi wa SUMA JKT anayesimamia ujenzi wa Kiwanda cha Chaki na vifungashio kuhakikisha ujenzi wa majengo ya mradi huo yanakamilika kwa wakati ifikapo tarehe 15 mwezi Januari, 2021 kama alivyoelekeza Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo ili kazi ya kufunga mitambo ya kiwanda hicho ifanyike na  kuanza uzalishaji.

 “Tena tarehe 15 naona mbali, mimi naagiza tarehe 14, yaani kuanzia leo ufanyekazi usiku na mchana ili mradi huu ukamilike kwa wakati na vifaa viletwe kwa ajili ya kuanza kufanya kazi ili kutoa ajira kwa vijana pamoja na kuboresha mapato ya Halmashauri ambalo ndilo lengo la Serikali kuziwezesha Halmashauri zijitegemee na kuacha utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali Kuu”, alisema Mhe. Mwanaidi Ali Khamis.

Naye Mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki, Mhe. Staslaus Nyongo aliiomba Wizara ya Fedha na Mipango kutoa fedha kwa ajili ya kulipia mitambo ya kuchakata chaki iliyoko nchini Uturuki ili ifungwe kiwandani hapo na kuanza uzalishaji ili kuiwezesha Halmashauri ya Wialaya Maswa kuongeza mapato na kuwapunguzia wananchi mzigo wa michango ya miradi ya maendeleo ikiwemo elimu.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa Bw. Aswege Kaminyoge alimhakikishia Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis kwamba atatekeleza maagizo hayo na kusimamia kwa karibu zaidi utekelezaji wa miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati na kuishukuru Serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa miradi hiyo ya Kimkakati.

Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Dkt. Fredirick Sagamiko alisema kuwa mwanzoni miradi hiyo miwili ya kiwanda cha kutengeneza chaki na kiwanda cha kutengeneza vifungashio ilitengewa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 8.2 lakini baada ya kufanya uchambuzi wa miradi hiyo, gharama imeongezeka hadi kufikia zaidi ya shilingi bilioni 29.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Bw. Festo Kiswaga kuhakikisha anajenga mindombinu ya barabara za hospitali mpya ya wilaya hiyo ili kuwawezesha wananchi kufika kwa urahisi na hudumiwa.

Alisema miundombinu iliyopo ya barabara za kuelekea hospitalini hapo zinaweza kusababisha madhara kwa wananchi hususani wagonjwa wanaohudumiwa katika hospitali hiyo hasa kipindi hiki cha mvua wakiwemo akina mama wajawazito na watoto.

Akizungumza na baadhi ya wagonjwa hospitalini hapo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango aliwataka wananchi kutumia kikamilifu huduma za hospitali hiyo iliyojengwa na Serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 1.9 na kusisitiza kuwa huduma za watoto waliochini ya umri wa miaka mitano zinatolewa bure.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa Hospitali hiyo iliyoko katika kijiji cha Dutwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Bw. James John alisema hospitali hiyo imekamilika na imeanza kutoa huduma za afya kwa wananchi wakiwemo wagonjwa wa nje, wanaolazwa, huduma ya mama, baba na mtoto, tiba na matunzo ya wagonjwa wa kifua kikuu na ukoma.

Aliiomba Serikali isaidie upatikanaji wa watumishi wa kada mbalimbali, vifaa tiba ikiwemo vifaa vya upasuaji, vitanda vya kujifungulia, mashine za kutolea dawa ya usingizi, ultrasound, samani pamoja na gari la kubebea wagonjwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Bw. Festo Kiswaga, alimweleza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis kwamba miundombinu ya barabara itawekwa kuunganisha majengo ya hospitali ili kuondoa adha ya wagonjwa kutembea kwenye tope hasa wakati wa mvua.

 

No comments :

Post a Comment