Thursday, January 14, 2021

MBUNGE KUNAMBI AAHIDI KUANZA UJENZI WA KIVUKO KWENYE MTO MNGETA AMBAO UNA MAMBA

……………………………………………………………………………………..

NIPO na nyinyi! Ni kauli ambayo ameitoa Mbunge wa Jimbo la Mlimba mkoani Morogoro, Godwin Kunambi alipofika kujionea changamoto inayowakabili wananchi wake wa Kijiji cha

Kidete Kata ya Mngeta ambao hawana kivuko kinachowawezesha kuvuka Mto Mngeta.

Kunambi amefika katika kijiji hiko ikiwa ni muendelezo wake wa ziara ya kutembelea Jimbo lake kwa ajili ya kuwashukuru kwa kumchagua kwa kura nyingi Rais Dk John Magufuli, yeye kuwa Mbunge na madiwani wanaotokana na CCM lakini pia kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wake kwenye kila kata ambapo jumla ya kata kwenye jimbo hilo ni 16.

Akiwa kijijini hapo Kunambi amejionea changamoto wanayokabiliana nayo wananchi wa eneo hilo katika kuvuka Mto huo wenye Mamba wengi kwa kutumia Mtumbwi mdogo ambao kwa hakika unahatarisha maisha ya wananchi hao.

Akizungumza na wananchi hao baada ya kuvuka Mto huo kwa kutumia Mtumbwi huo kama wananchi wake, Kunambi amewaomba wananchi hao kumpa miezi mitatu hadi ifikapo Mei Mwaka huu ujenzi wa daraja kubwa la kudumu utaanza na kwa sasa anapambana kuhakikisha kinajengwa kivuko cha muda mfupi.

” Ninafahamu changamoto hii inawatesa wanafunzi wetu na hata nyinyi wananchi katika ufanyaji wa shughuli zenu za kilimo, niwaombe mnipe miezi mitatu ya kuanza ujenzi wa daraja kubwa lakini kwa kipindi hiki kifupi hiki nimemwambia Meneja wa Tanroad Wilaya anipe gharama zinazohitajika ili nitafute tujenge daraja la muda hapa, niwahakikishie hadi kufikia Mei tutakua tumeanza ujenzi wa daraja kubwa ili kuondoa kero hii.

Sipo tayari kuona wananchi wangu wa Mngeta mliotuchagua sisi na Rais Dk John Magufuli muendelee kuteseka na kupata changamoto hii ya kuliwa na Mamba, niwahakikishie tutaanza ujenzi wa daraja la muda mfupi wakati huu ambao tunasubiri daraja la kudumu,” Amesema Mbunge Kunambi.

Kwa upande wao wananchi wa kata hiyo wamemshukuru Mbunge huyo kwa kitendo chake cha kufika na kujionea changamoto wanayokumbana nayo huku wakimuomba kutimiza ahadi yake hiyo ndani ya muda mfupi ili waweze kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

” Hatujutii kumchagua Kunambi ameonesha jinsi gani yeye ni Mtoto wa Mlimba, kufika kwake na kujionea kero hii ni hatua ya kwanza lakini tayari ametuahidi kujenga kivuko cha muda mfupi huku akisema ndani ya miezi mitatu daraja la kudumu litajengwa, tunamshukuru sana,” Amesema Joseph Mathias ambaye ni mkazi wa Kijiji hiko.

 

No comments :

Post a Comment