Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, akijibu hoja mbalimbali mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, zilizoulizwa na Kamati hiyo, jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Suleiman Kakoso, akifafanua jambo kwa viongozi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), pamoja na wajumbe wa kamati yake wakati wa uwasilishwaji wa taarifa mbalimbali za miundo na majukumu yaliyo chini ya Sekta hiyo, jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Mhandisi Japhet Maselle, akiwasilisha taarifa kuhusu muundo na majukumu ya Wakala huo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, jijini Dodoma.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Wakurugenzi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), wakisikiliza uwasilishwaji wa taarifa kuhusu miundo na majukumu ya taasisi mbalimbali zilizo chini ya Sekta hiyo, jijini Dodoma.
PICHA NA WUU
*************************************************
Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) umesema kuwa umeongeza mapato yake ya ndani (Own
Sources) kutoka Shilingi Bilioni 4 kwa mwaka wa fedha 2006/07 hadi kufikia Shilingi Bilioni 54 kwa mwaka wa fedha 2019/20.Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Mhandisi Japhet Maselle, wakati akiwasilisha taarifa kuhusu Muundo na majukumu ya Wakala huo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu jijini Dodoma.
Mhandisi Maselle, amesema kuwa ongezeko hilo limeifanya TEMESA Kupunguza utegemezi wake kwa Serikali katika kujiendesha kwake na kuweza kuchangia Mfuko Mkuu wa Serikali kila mwaka.
“Mfano katika mwaka 2018/19 tulitoa kiasi cha Shilingi 1,130,209,422.50 na mwaka 2019/20 kiasi cha shilingi 1,224,378,108.24 zilitolewa gawio kwa Serikali”, amesema Mhandisi Maselle.
Aidha, amefafanua kuwa ongezeko hilo pia limeiwezesha TEMESA kuongeza idadi ya Vivuko kutoka 13 mwaka 2005 hadi kufikia 33 mwaka 2020 vikiwemo Vivuko viwili vipya vilivyokamilika kujengwa kwa ajili ya kutoa huduma katika Mkoa wa Geita (Chato-Nkome) na Pwani (Mafia-Nyamisati).
Maselle, ameeleza kuwa mbali
na miradi hiyo TEMESA imeshiriki katika miradi mingine ikiwemo kuweka
mifumo ya umeme na usalama katika miradi mbalimbali ya kimkakati kama
vile Mwalimu Julius Nyerere Dam,
Mkulazi Sugar Industry, Mji wa Serikali Mtumba na Ukuta wa Mirerani.
Kuhusu ujenzi wa karakana katika kila wilaya, Mhandisi Maselle, amesema kuwa tayari TEMESA imenunua karakana zinazotembea (mobile workshop), kwa karakana ambazo zipo nje ya miji na kukarabti zile zilizochoka ili kurahisisha huduma kwa wateja wao.
“Tunachokiomba kutoka Serikalini ni kupatiwa fedha kwa wakati ili kuboresha miundombinu ya karakana zetu ili kuwa na ufanisi katika utengenezaji wa magari”, amesisitiza Maselle.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Suleiman Kakoso, amesema kuwa ili wakala huo uweze kusimama na kujiendesha kibiashara Serikali inatakiwa itoe fedha kwa wakala huo.
Ameiagiza Wizara kupitia TEMESA na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuwasilisha mchanganuo wa madeni wanayodai katika taasisi zote za Serikali kwa Kamati hiyo ili kuweza kusaidia kusukuma na kukumbusha Serikali kulipa madeni hayo.
Ameitaka pia Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT), kuendelea kujikita katika utoaji wa elimu kwa ngazi ya chini ili kupata wataalamu kama mafundi sanifu na mafundi mchundo ambapo kwa sasa wataalamu hao wanaonekana kupungua.
TEMESA, TBA, Vikosi vya Ujenzi pamoja na ICoT ni baadhi ya Taasisi zilizo chini ya Sekta ya Ujenzi ambapo leo zimewasilisha taarifa zao kuhusu miundo na majukumu yao kwa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu ambapo pamoja na mambo mengine Taasisi hizo zimetakiwa kufanya kazi kwa ufanisi na weledi ili kuleta tija kwa Taifa.
No comments :
Post a Comment