Friday, January 29, 2021

Kwa nini wadau inapaswa wajue sababu mikutano mikuu ya mwaka sekta ya hifadhi ya jamii ikisitishwa?

Baadhi ya wanachama na wadau wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) wakifuatilia mada mojawapo ya mikutano mikuu kila Mwaka ya taasisi hiyo mwaka 2018 kwenye ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni Zanzibar. (Na Mpigapicha Wetu)

Na Christian Gaya. 

Majira Ijumaa 29 Januari 2021

Wawekezaji wakubwa wa mifuko ya hifadhi ya jamii ni wafanyakazi na waajiri wao, pale wanaojisajili uanachama wa uchangiaji kwa kukatwa asilimia fulani kutoka katika ...

mishahara yao.

Mwajiri na yeye kuchangia kiasi hicho hicho kila mwezi au zaidi kwa ajili ya mfanyakazi wake, kwa makubaliano ya kupata huduma mbalimbali za mafao ya muda mfupi na ya muda mrefu, kutoka katika mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii.

Hata hivyo, wanachama na wadau wengine wa sekta ya hifadhi ya jamii mara nyingi wameonekana kuwa ni kundi ambalo halina mamlaka kabisa ya kusimamia utendaji na uendeshaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii, ikiwemo kufuatilia tabia na utaratibu wa utendaji wa bodi za wadhamini wa mifuko hiyo ya hifadhi ya jamii, hali inayoonesha kutofautiana kwa mitazamo kwa upande mwingine.

Mfano, wadau kutoka sektabinafsi, sektarasmi na sekta zisizorasmi wanapotaka kujua ni sababu zipi zilizofanya mifuko hiyo ya hifadhi ya jamii, mathalani Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), mfuko wa wafanyakazi wa serikalini (PSSSF), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), wasitishe mikutano mikuu ya kila mwaka kwa ajili ya wanachama wao na washirika  wengine, kama sheria inavyoelekeza, hata baada ya kurekebishwa mara ya mwisho mwaka 2017, mpaka leo hii, na hata kama baadhi ya taasisi hizo ziliunganishwa na kuanza kufanya kazi rasmi mwaka 2018.

Na hiyo hata kama Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Zanzibar (ZSSF) ambao wenyewe ilikuwa wanaendelea kuwajibika kufanya mikutano yao mikuu ya kila mwaka kwa wanachama na wadau wao hadi mwaka 2019 isipokuwa mwaka 2020 tu.

Katika hali hiyo mdau mwingine anaweza kujiuliza iwapo kama kuna maana yoyote mifuko hiyo iendeshwi kwa kufuata utaratibu na kanuni wa sheria za hifadhi ya jamii za kikatiba?

Na je tangu mwaka 2018 wanachama na wadau wengine wa hifadhi ya jamii wamekuwa wakisimamiaje utendaji na uendeshaji wa mifuko hiyo?

Zaidi, na je, ni jinsi gani ya kufuatilia tabia, mienendo na taratibu zote za utendaji wa bodi za wadhamini?

Njia mojawapo ya wanachama na wadau wa mifuko ya hifadhi hizo za jamii,  kwa ajili ya kufuatilia na kujua utendaji wa mifuko hiyo inayosimamiwa na bodi za wadhamini, ni kupitia mikutano mikuu ya kila mwaka maarufu “Annual General Meeting” (AGM), ambayo inaelekezwa kisheria kwamba iwe ni hivyo.

Wadau wa mifuko ya hifadhi ya jamii hawana tofauti na wadau au wateja wa taasisi zingine za fedha kama vile benki, na wengi wao hushuhudia benki nyingi nchini hufanya mikutano mikuu ya kila mwaka.

Wadau kama wanachama ambao ndiyo wachangiaji mathalani wafanyakazi na waaajiri wao, mara nyingi ndiyo waliodhaminiwa au wakala wa kuhakikisha ya kwamba kuna ushirikiano na taasisi hizo. 

Na kazi mojawapo ya waajiri ni kusimamia ukataji na kupeleka michango kwenye mifuko ya hifadhi hiyo, pamoja na kuhakikisha kwamba wanatunza kumbukumbu za wafanyakazi wao baada ya kutekeleza hilo.

Kwa kawaida kuhudhuria mkutano mkuu wa mwaka  huwa ni nafasi kipekee na muhimu sana kwa wadau kama wanachama wa mifuko hii ya hifadhi ya jamii, kwa ajili ya kuchambua na kuzungumzia mambo muhimu yanayogusa afya na ustawi wa mifuko kwa kutumia  taarifa mbalimbali.

Baadhi ya sababu za muhimu huo ni fursa za kupata uchambuzi wa taarifa za bodi ya wadhamini kuhusu taasisi hizo, ili kujua nafasi na uwezo wa mifuko kifedha.

Nyingine ni kujua utendaji na za utekelezaji,  ikiwemo kufuatilia malalamiko ya wadau na jinsi yanavyotatuliwa kwa kutumia taratibu husika, ikiwemo hata zinazotumia za kisasa kama vile za kidigitali maarufu “teknolojia ya habari na mawasiliano” (TEHAMA).

Mbali ya hayo, wadau pia wana haki kufahamu na kuelewa kuhusu maamuzi muhimu yaliyoamuliwa na kutekelezwa baada ya mikutano mikuu ya kila mwaka, kusisitishwa kufanyika, yaani ikiwemo mambo muhimu ambayo yalipewa vipaumbele pamoja na yaliyoambatana.

Hivyo, siku zote wadau wa mifuko ya hifadhi ya jamii huona umuhimu kupata nafasi hiyo ya mikutano mikuu ya kila mwaka, kama wachangiaji, waitumie ipasavyo kuendelea kujipanga, haswa kwa ajili ya kustaafu.

Katika mkutano mkuu wa kila mwaka wanachama wa mfuko na wadau mbalimbali wa sekta ya hifadhi ya jamii nchini wanahudhuria ikiwemo wenyeviti na wajumbe wa bodi, maofisa watendaji wakuu, maofisa wanaoshughulika na raslimaliwatu na utawala, maofisa sheria, uhasibu, maofisa fedha, maofisa teknolojia na mawasiliano na maofisa bima, kutoka serikalikuu na taasisi za serikali.

 

Pia hata mashirika ya umma, makampuni binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi kutoka sehemu za kazi, vyama vya waajiri.

 

Hata wananchi wengine wanaotakiwa kushiriki kwa lengo la kutaka kujua na kupata elimu ya masuala ya hifadhi ya jamii, pia huruhusiwa kushiriki.

 

Mkutano mkuu wa mwaka huwa huwa na madhumuni mbalimbali yanayogusa sekta hiyo ya hifadhi ya jamii, mfano kutathmini na kujadili maendeleo pamoja na maboresho ya sekta nzima ya hifadhi ya jamii, mchango wake katika kuongeza ajira, na kuwezesha ujasiriamali.

 

Madhumuni mengine huweza hata kuwa kwa ajili kupanua wigo wa hifadhi ya jamii ili kuwafikia hata wadau ambao wako kwenye sekta zilizorasmi na zisizorasmi.

 

Pia mikutano hiyo huwa ni fursa na nafasi kipekee kwa mfuko kuonesha ufanisi wa kazi zao pamoja na mafanikio yao kwa  wanachama na wadau wengine wa hifadhi ya jamii,  kuhusiana na  ukusanyaji wa michango yao, kupunguza matumizi ya uendeshwaji wa shughuli zao, na pia hata kwa upande wa uwekezaji wao kwenye vitegauchumi mbalimbali.

Wakati kama huo wa mikutano hiyo ya kila mwaka huwa ni fursa ya kuwataarifu mambo yanayohusiana na idadi ya jumla ya wanachama na waajiri wapya walioandikishwa kwa mwaka huo, pamoja na thamani za rasilimali zote za mfuko husika.  

Nyingine ni mdau kujua hata taarifa zinazohusiana na jumla ya idadi ya ukusanyaji wa michango ya wanachama, idadi ya wastaafu waliopata pensheni kwa mwaka uliopita,  na jumla ya wastaafu waliopo mpaka wakati wa mkutano mkuu wa mwaka unapofanyika.

Na hata pia kuzungumzia juu ya kima cha juu na kima cha chini cha pensheni kinachotolewa na mfuko husika kwa wastaafu wake.

Vile vile ni mdau hata pia kupata nafasi kuzungumzia kuhusu kima cha juu na kima cha chini cha pensheni kinachotolewa na mfuko husika kwa wastaafu wake.

Pia huwa ni fursa muhimu kwa wanachama na wadau wengine kujua hata upandishwaji wa viwango vya pensheni unaofanywa na mfuko husika, kulingana na mabadiliko ya kiuchumi.

Baadhi ya wadau na wanachama wengine huenda wangependa kujua uhai wa mfuko husika na kama umefanyiwa tathmini ya kitaalamu hivi karibuni, na kama takwimu zinathibitisha ya kuwa mfuko uko imara na kama una uwezo wa kujiendesha na kulipa mafao ya wanachama wake  kwa miaka  kadhaa bila kuteteleka au bila kukusanya michango, ili kuwaondolea hofu kuhusu maendeleo ya mfuko wao.

Na nyingine ni kujua kuhusu lengo husika iwapo kuna uthaminishaji wake, ikiwa ni kuwezesha pensheni kuendana na ukuaji wa gharama za maisha kwa wastaafu wake.

Kadhalika, wadau na wanachama wengine hupenda kujua changamoto mbalimbali zinazokabili mfuko husika, mfano zinazohusiana na baadhi ya wanachama kukimbilia kuchukua michango yao.

Changamoto nyingine ambayo wanachama na wadau huhitaji kujua ni kuhusiana na waajiri kutolipa michango ya wafanyakazi wao kwa wakati, uelewa mdogo wa hifadhi ya jamii kwa watanzania wote kwa ujumla, pamoja  na uandikishaji wa sekta isiyo rasmi ikiwemo wakulima na wavuvi.

Huenda kundi lingine la wadau wangependa kujua mikakati kambambe ya mfuko husika kuhusiana na siku zijazo, mfano njia mbalimbali za kukabiliana na changamoto mbalimbali za mfuko.

Kwa maana hiyo, kisheria mkutano mkuu wa mwaka unatakiwa ufanywe kila mwaka, na   isipofanyika hivyo mtu mwingine anaweza kusema, basi “uwezo wa nguvu wa mamlaka ya kisheria iliyoelekezwa hauna nguvu yoyote kwa wanachama, waajiri na hata kwa wadau wengine”.

 

Ni wajibu wa bodi ya wadhamini za mifuko husika kuhakikisha ya kuwa mikutano mikuu ya mwaka inafanyika na taarifa zake zinawafikia wadau wote  wa mfuko husika kwa muda na siyo vinginevyo, vinginevyo uwekezaji kwenye taasisi hizo utakosa imani.  

 

Pia, bodi hizo wahakikishe kuwa taarifa zinazotolewa na mfuko husika zinakuwa na ubora wa hali ya juu, na kwamba lazima ziwafikie wanachama na wadau wanaohusika waliotawanyika karibu nchi nzima, kwa muda unaotakiwa, yaani kwa kila mwaka, ili wawakilishi wao waweze kuhudhuria na kuweza kuchambua utekelezwaji na utendaji wa mfuko yao kwa mujibu wa sheria za hifadhi ya jamii.  

 

Christian Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni, mshauri na mtaalamu wa masuala ya pensheni na kustaafu. Kwa maelezo zaidi: gayagmc@yahoo.com +255 655 13 13 41, unaweza kutembelea www.hakipensheni.blogspot.com, info@hakipensheni.co.tz

No comments :

Post a Comment