Wednesday, January 13, 2021

KUWE NA UTARATIBU MAALUM WA KUGAWA UMETA KWA WANANCHI

Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Mhe. Hashimu Mgandilwa aliyekaa mbele akiwa katika kikao na ujumbe wa REA ulioongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo wa pili kushoto akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga walipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini katika Wilaya ya Ruangwa

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo, akizungumza wakati wa kikao cha pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Mhe.Hashimu Mgandilwa walipomtembelea Ofisini kwake tarehe 11/12/2021ƒ

Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga akielezea utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini katika kikao cha pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hashimu Mgandilwa walipomtembelea ofisini kwake tarehe 11/01/2021

…………………………………………….

Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mh. Hashimu Mgandilwa ameshauri Wakala wa Nishati Vijijini

(REA) na TANESCO kuweka utaratibu wa wazi wa kusambaza vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) ambavyo vinatumika kama mbadala wa mfumo wa kutandaza nyaya katika nyumba ili wananchi wengi waweze kuunganishiwa umeme.

Mgandilwa alitoa ushauri huo tarehe 11/01/2021 ofisini kwake Ruangwa wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) kukagua utekelezaji wa miradi ya kusambaza nishati vijijini katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

“Upatikanaji wa UMETA hauko wazi mwitikio ni mkubwa, mlolongo ni mrefu tupunguze urasimu wananchi walio katika wigo wa mradi wapewe ili waweze kuunganishiwa umeme,” alisema Mgandilwa.

Aidha aliipongeza Bodi kwa kazi nzuri ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini na kuahidi kutoa ushirikiano katika usimamizi wa miradi hiyo. Alisema katika Wilaya yake vimebaki vijiji 25 ambavyo havina umeme.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo alimshukuru Mkuu huyo wa Wilaya kwa ushirikiano wake hasa katika kuhamasisha uunganishaji wa wateja ambao umewezesha Wilaya yake kufikia zaidi ya asilimia 100 ya wateja wa awali ambao walipangwa kuunganishiwa umeme.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga alimwagiza Mkandarasi anayetekeleza Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza kampuni ya State Grid Electrical and Technical Works LTD kugawa UMETA 250 za bure kwa wananchi ndani ya miezi miwili.

Mhandisi Maganga alimweleza Mkuu wa Wilaya kuwa vijiji 25 vilivyobaki bila umeme vitapatiwa umeme katika Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ambao unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Akijibu malalamiko yanayopelekwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na wananchi ambao vitongoji vyao havina umeme, Mhandisi Maganga alisema Serikali imeanza kusanifu mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji vyote ambao utaanza mwezi Julai 2021.

 

No comments :

Post a Comment