* Asema ni dhambi kubwa
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
KITENDO
cha wanafunzi wengi wa Shule ya Msingi Barango iliyopo wilayani Ubungo
katika Mkoa wa Dar es Salaam kukaa chini kutokana uhaba wa madawati
kimemkasirisha na kusababisha Rais Dk.John Magufuli kutoa maagizo na
maelekezo kwa viongozi wa mkoa huo.
Dk.Magufuli
amesema haiwezekani katika Mkoa wa wenye viongozi wa ngazi mbalimbali
akiwemo Mbunge wa Ubungo Profesa Kitila Mkumbo ambaye ni mwalimu lakini
wanafunzi wanakaa chini.
Akizungumza
leo wakati akizindua Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Ihungo iliyopo
mkoani Kagera, Rais Magufuli ametumia nafasi hiyo kuizungumzia shule ya
Barango ambayo ina wanafunzi wengi ambao wanakaa chini kwa kukosa
madawati lakini pia kuna madarasa mengine yamebomoka.
"Madarasa
mengine yamebomoka, madawati mengine yamevunjika yameachwa bure, Mkuu
wa Wilaya yupo, Mkuu wa Mkoa yupo, Mkurugenzi wa Ubungo yupo na bado
anakusanya kodi, na Mbunge wa Ubungo yupo tena yuko hapa na ni Profesa
tena wa elimu.'' Amesema JPM.
"Simama
Profesa (Kitila) wakuone kwenye Jimbo lako, simama hapo mbele wakuone
kabisa na ni Profesa wa elimu, anafundisha elimu, mimi napenda kusema
ukweli, kaa sasa wameshakuona lakini hiyo shule ya Barangu wanafunzi
wanakaa chini.
"Ninamshukuru
huyo muandishi ambaye ameitoa kwenye mitandao, viongozi wa kule
wakasema ni masuala ya kisiasa, hayo sio masuala ya kisiasa, bali ndio
mambo ninayopenda kuyajua, ninazungumza nikiwa Kagera lakini nikienda
Dar es Salaam niyakute yamekamilika na wanafunzi hawakai chini.
"Nitaenda
kuitembelea mimi hiyo shule, kwa hiyo kama wananisikia wa Dar es salaam
meseji sent and delivary. Haiwezekani ndugu zangu wana Kagera, uwe
umechaguliwa na wananchi unaitwa Rais halafu ukawapa watu madaraka,
ukawapa uwaziri, ukawapa ukuu wa mkoa , ukawapa ukurugenzi na
wanakusanya kodi na bajeti zipo, na wanazunguka kwenye maeneo hayo
wanakuta wanafunzi wanakaa chini"Amesema Rais Magufuli.
Amesisitiza
hiyo ni dhambi kwake na kwamba alikosea kuchagua baadhi ya
viongozi."Ndio maana nilipofika hapa nilizungukia madarasa, sikusubiri
madarasa niliyoandaliwa, nikawa navamia madarasa nikakuta madawati yapo
nikafurahi sana nikasema Haleluya...hongereni sana ninyi lakini ile
shule iliyopo Ubungo maneno haya wakayasikie na mawaziri mko hapa".
Amesema.
Aidha
amesema ana uhakika kuna maeneo watu wanafanya kazi vizuri sana lakini
kuna maeneo mengine bado wamelala."Na ndio maana Mkurugenzi wa Geita
niliamua nimfukuze kazi, yeye ananunua gari la Sh.milioni 400 huku
wananchi wanachangishwa kwa ajili ya kununua madawati, zinatolewa fedha
na mgodi wa wa GGM kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya wananchi yeye
anakwenda kununua magari.''
"Anakwenda
kununulia mpaka mabasi ya kusafirisha wafayakazi, yupo Geita Mjini,
utakuwa unasafirisha walimu kwenda kwenye shule kufundisha. Kwa hiyo
nitoe mwito kwa viongozi wenzangu, tuzitumie fedha hizi vizuri ili
zilete matokeo kwa wananchi,"amesema.
Ameongeza,
"Na hizi Sh.bilioni bilioni sita zilizotolewa na Serikali ya Uingereza
na Sh.bilioni tano zilizotolewa na Serikali ya Tanzania zisingetumika
vizuri leo tusingeona mfano huu(Shule), nilipokuja hapa Kagera walitaka
fedha hizi nizigawe nikanunue ndizi, nikanunue mahindi.
"Nikasema
sitoi kitu, najua nilioekana wa ovyo kwa baadhi ya wanasiasa, huwezi
ukawagawia watu wote wa Kagera chakula, nilitaka niwaambie ukweli na
ukweli unakuweka huru." Amesema JPM.
No comments :
Post a Comment