Monday, January 4, 2021

HAKUNA KIWANGO CHA FEDHA KILICHOWEKWA KWA MATRAFIKI KUKIKUSANYA BARABARANI-SIRRO

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro ameweka wazi hakuna kiwango cha fedha ambacho kimewekwa kwa askari polisi wa kikosi cha usalama barabarani bali fedha zitatokana na makosa yaliyofanyika na si vinginevyo.

Akizungumza leo Januari 4,2020 mbele ya waandishi wa habri, IGP Sirro amefafanua kumekuwepo na madai kwamba trafiki wamewekewa malengo ya kukusanya pesa wawapo barabarani, sio kweli,hiyo biashara haipo.

"Ni kwamba fedha zinapatikana kulingana na makosa ambayo yanafanywa barabarani, lakini hakuna kiwango ambacho kimewekwa kwa trafiki kukikusanya ili kuongeza pato la taifa,"amesema Sirro.
Aidha amefafanua kukusanya fedha za barabarani sio kazi yao jeshi la polisi, lakini wao wanachofanya ni kukamata makosa yanayotokana na makosa yanayofanywa na wanaotumia vyombo vya moto, hivyo fedha ni za Serikali na ndizo zinazotumika kununua dawa, kujenga miundombinu ya huduma za kijamii.

Ametumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa watanzania na hasa mabalozi wa usalama barabarani ambao wamekuwa na mchango mkubwa wa kutoa habari zinazosaidia kuchukua hatua huku akieleza maagizo mbalimbali aliyoyatoa kwa kikosi hicho ili kuhakikisha wanaboresha utoaji huduma kwa jamii.

Wakati huo huo, Sirro amesema kuna umuhimu wa askari kuendelea kuhwa na heshima kwa wale wanaowahudumia.Kuhusu changamoto ambazo zinakikabili kikosi cha usalama barabarani, amesema ni uhaba wa vifaa vikiwemo vya kupima ulevi kwa madereva lakini tayari wamejipanga kuondoa changamoto hiyo.

 Alipoulizwa ni mkoa gani trafiki ndio wanalalamikiwa zaidi kwa tuhuma za kujihusisha na rushwa, amejibu hawezi kueleza ni mkoa gani ila anafahamu kuna maeneo machache ndio yanalalamikiwa yakiwemo ya jijini Dar es Salaam, Tanga.


 

No comments :

Post a Comment