Wednesday, January 27, 2021

EWURA YASITISHA BEI MPYA ZA MAJI ZILIZOPASWA KUTOZWA KUANZIA ANKRA ZA JANUARI 2021

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa  Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maj (EWURA), Mhandisi Godfrey Chibulunje,akizngumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Januari 27,2021 jijini Dodoma wakati akitangaza kufuta bei mpya za Maji.

Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa  Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maj (EWURA), Mhandisi Godfrey Chibulunje,wakati akitangaza kufuta bei mpya za Maji leo Januari 27,2021 jijini Dodoma.

……………………………………………………………………………

Na Alex Sonna, Dodoma
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji(EWURA), imetangaza kusitisha bei

mpya za maji zilizopaswa kutozwa kuanzia ankra za Januari, 2021 ili kufanya uchunguzi wa kina kutokana na malalamiko ya wateja.

Uamuzi huu umetangazwa leo Januari 27,2021 Jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Mhandisi Godfrey Chibulunje, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema bei hizo zilizofutwa ni zile ambazo zilikuwa zimeidhinishwa na Mamlaka hiyo kwa mwaka 2020/21 na kwasasa zitaendelea kutozwa zilizokuwapo za mwaka 2018/19.

“Hivi karibuni kumekuwepo na malalamiko makubwa ambapo kati ya malalamiko yote yanayopokelewa na EWURA katika sekta ya umeme, mafuta, gesi asilia, asilimia 60 ni ya maji,kilio kikubwa kutoka kwa wateja wa huduma za maji kipo kwenye ankra za maji ambapo asilimia 75 ya malalamiko yote ni kutokubaliana na ankra zinazotolewa na mamlaka mbalimbali nchini,”amesema.

Ameeleza kuwa malalamiko mengine ambayo ni makubwa na migogoro ya uunganishaji huduma za maji ambapo ni asilimia 13.

“EWURA huidhinisha bei kwa mamlaka za maji kwa miaka mitatu ambapo bei hizo ziliidhinishwa kwa mwaka 2018/19, 2019/20 na 2020/21 na kwa utaratibu wetu kuanzia Januari 2021 mamlaka nyingi zilikuwa zinatarajia kuanza kutumia bei za mwaka 2020/21,”amesema.

Hata hivyo, amesema kutokana na malalamiko hayo imefuta bei zote ambazo zilitakiwa kuanza kutumika mwezi huu na kuelekeza zitumike bei za mwaka 2018/19.
“Hatua hii inachukuliwa ili kuipa uwezo EWURA kufanya uchunguzi wa kina juu ya malalamiko haya ya maji ili kubaini ukweli wa malalamiko hayo ambapo baada ya kumaliza shughuli ya uchunguzi wa kiufundi, EWURA itatoa maelekezo mengine ya matumizi ya bei ambazo zilitakiwa kuanza Januari, 2021,”amesema.

Mkurugenzi huyo amesema bei zilizofutwa Ni kwenye mamlaka za maji za Mikoa, Wilaya, Mji midogo na miradi mikubwa ya kitaifa ambazo ziliomba kuidhinishiwa kupandisha ankra za maji  mwezi huu.

 

No comments :

Post a Comment