Monday, January 18, 2021

Dkt Manongi awataka Watumishi wa NCAA kuweka Malengo ya Utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya chama tawala 2020 – 2025

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Dkt. Freddy Manongi akiongea na Watumishi wa NCAA leo tarehe 18 Februari,2021wakati wa kikao maalum cha mwanzo wa mwaka ikiwa ni sehemu ya utaratibu aliojiwekea wa kukutana na Watumishi mara kwa mara kujadili masala mbalimbali kuhusu utendaji kazi.

Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA (Huduma za Shirika) Bw. Audax Bahweitima akizungumza na Watumishi wa NCAA katika kikao kazi kati ya Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Dkt Freddy Manongi na Watumishi wa Mamlaka hiyo.

Kamishna wa Uhifadhi wa wa NCAA Dkt. Freddy Manongi (Kulia) akimtambulisha kwa Watumishi wa Mamlaka hiyo Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayesimamia Utalii, Uhifadhi na Maendeleo ya Jamii Dkt. Christopher Timbuka ambaye amehamia NCAA hivi karibuni.

Sehemu ya Watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wakimsikiliza Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Dkt. Freddy Manongi (hayupo pichani)akiyekutana na watumishi hao kujadili masuala mbalimbali ya utendaji kazi.

***********************************************

Na Kassim Nyaki-NCAA

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Dkt Freddy Manongi amewataka watumishi wa Mamlaka hiyo kuhakikisha kuwa wanaweka malengo ya

Utekelezaji wa Ilani ya Chama tawala hasa katika eneo la kuongeza watalii na Mapato ya Serikali.

Akizungumza na watumishi wa Mamlaka hiyo katika kikao maalum cha mwanzo wa mwaka cha kujadili utekelezaji wa majukumu; Kamishna Dkt. Manongi ameeleza kuwa ni wajibu wa kila mtumishi kusoma ilani ya CCM na kujiwekea malengo ya kutekeleza ilani hiyo ili kuhakikisha kuwa NCAA inatekeleza lengo la Serikali la kuongeza idadi ya watalii kufikia wageni Milioni tano ifikapo mwaka 2025 na kuchangia ongezeko la pato la Serikali hasa katika Sekta ya Utalii. 

Dkt. Manongi amewaeleza watumishi wa hao kuwa Wizara imeipa Mamlaka hiyo lengo la kuongeza watalii wanaotembelea eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kufikia watalii million mbili kwa mwaka.

“Waziri wetu wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro alishaelekeza kila mtumishi kuisoma ilani na kuielewa ili kila mtu aitafsiri kwa vitendo na kuweka malengo ya utekelezaji wa majukumu na kuhakikisha kuwa tunaongeza idadi ya watalii na Mapato ya Serikali kila mwaka” alisisitiza Dkt. Manongi.

Dkt Manongi amefafanua kuwa ili kufikia malengo hayo lazima kila mtumishi afanye kazi kwa bidii na kujituma muda wote na ofisi yake itahakikisha inaweka malengo na kuwapima watumishi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

Ameongeza kuwa NCAA kama moja ya Taasisi zinazofuata mfumo wa Jeshi la  Uhifadhi lazima watumishi waendelee kuwa na nidhamu, ukakamavu na kuhakikisha wanafuata Sheria, taratibu na kanuni za Utumishi wa Umma katika Utekelezaji wa majukumu yao.

Halikadhalika Dkt. Manongi ameeleza kuwa katika kuimarisha utendaji kazi, NCAA inaendelea na uboreshaji wa General Management Plan na kupitia upya mpango mkakati wa Shirika (Corporate Strategic Plan) sambamba na Mpango wa matumizi Mseto ya Ardhi ili kuhakikisha kunakuwa na utaratibu mzuri wa kufikia Malengo makuu matatu ya Mamlaka hiyo ambayo ni; Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii.

Ameeleza Kuwa NCAA inaendelea na ujenzi na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali kadri inavyopata pesa kutoka Serikalini ili kuhakikisha kunaendelea kuwa na mazingira rafiki na ya kuvutia kwa wageni mbalimbali wanaotembelea Hifadhi ya Ngorongoro.

Katika kikao hicho na watumishi wa NCAA Dkt.Manongi ametumia fursa hiyo kuwatambulisha Manaibu Kamishna wawili waliohamishiwa NCAA hivi karibuni ambao ni Dkt. Christopher Timbuka  anayesimamia Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii na Bw. Audax Bahweitama ambaye ni naibu Kamishna wa NCAA anayesimamia Huduma za Shirika. 

Dkt. Manongi amewatakia watumishi hao heri ya mwaka mpya na utekelezaji mwema wa majukumu wenye mafanikio.

 

No comments :

Post a Comment