Mkurugenzi wa elimu na utawala kutoka ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Julius Nestory,akizungumza na wakuu wa shule za Sekondari zilizo chini ya Makanisa ya Kanisa Katoliki na Jumuiya ya Kikristo Tanzania ambayo yanaratibiwa na Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC) iliyofanyika leo Januari 27,2021 jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC) Bw.Peter Maduki,akielezea jinsi wanavyotoa elimu katika shule zao wakati wa wa Mkutano wa wakuu wa shule za Sekondari zilizochini ya Makanisa ya Kanisa Katoliki na Jumuiya ya Kikristo Tanzania ambayo yanaratibiwa na Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC) iliyofanyika leo Januari 27,2021 jijini Dodoma.
Sehemu ya washiriki wakifatilia Hotuba ya Mgeni rasmi wakati wa kikao cha wakuu wa shule za sekondari zilizochini ya Makanisa ya Kanisa Katoliki na Jumuiya ya Kikristo Tanzania ambayo yanaratibiwa na Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC)
…………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Tume ya Kikristo ya huduma za kijamii (CSSC) imepongezwa kwa kuendelea kutoa huduma
bora kwa jamii hasa katika elimu na kuwa mchango mkubwa katika kuleta maendeleo na kuongeza ubora wa elimu hapa nchini.Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa elimu na utawala kutoka ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Julius Nestory wakati akiongea na walimu wakuu wa shule za Sekondari zilizochini ya CSSC waliokutana kwa lengo la kutathmini na kuweka malengo mapya katika shule hizo.
Amesema Shule hizo zimekuwa na mchango mkubwa katika kutoa elimu hapa nchini na huduma nyingine za kijamii hasa katika sekta ya afya katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
“Shule hizi zimekuwa na mchango mkubwa sana hapa nchini hata ukiangalia katika ufaulu shule binafsi zinafanya vizuri sana na zenu zimo sitaki kuzitaja shule hizo lakini wenyewe mnajua, ufaulu huu unatubeba hata sisi serikali” amesema Julius.
Aidha amewataka wakuu wa shule hizo kuendelea kusimamia maadili, miongozo na sera za Serikali ili kufikia malengo zaidi na kuendelea kuipa sifa nzuri huduma hiyo hapa nchini katika kutoa huduma za kijamii.
Aidha amewataka kuheshimu ngazi nyingine za utawala katika maeneo yao ya kazi pindi wanapofika katika ofisi zao kuangalia utawala katika maeneo yao.
” Wengi wenu wakija wakuu wa Wilaya na wengine nje ya Kamishna wa elimu wanasema hawawapi ushirikiano lakini tambueni kuwa Mkuu wa Wilaya akijilidhisha hakuna usalama katika eneo hilo anauwezo wa kufunga shule hiyo kwahiyo mujue Mamlaka kati ya Wizara ya Elimu na TAMISEMI” Amesema.
Aidha amesema wamekubaliana na CSSC kufanya mitihani ya pamoja ya kupima uelewa (moku) kuwa na usawa kwa madarasa yote ya mitihani kama darasa la nne, saba, kidato cha pili na kidato cha nne.
Ameongeza kuwa “Serikali imetoa muongozo wa kukalilisha madarasa mtoto umemfanyia mtihani wa kipimo na amefuvu huyo ni wako, madarasa yanayoruhusiwa kukalilisha madarasa ni darasa la nne na kidato cha pili tu” amesema.
Ametaka walimu wote wanaofanya kazi katika shule hizo kuwa na mikataba ya kazi na mwalimu anapokiuka miiko yake ya kazi aripotiwe kwa mwajiri wake na Serikali ipate taarifa ili inapoajiri walimu ijue tabia ya mwalimu huyo kabla ya kumuajiri.
Ameongeza kuwa ” Pia Wakuu wa shule zingatieni ratiba za kuamka kwa watoto na suala la michezo mtoto lazima acheze kuna baadhi ya watoto hawachezi sio kwamba hawapendi kucheza bali wakuu hamtaki wacheze, ruhusuni watoto wacheze” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa CSSC Peter Maduki amebainisha kuwa kupitia mkutano huo wamepata wasaa wa kubadilishana uzoefu na changamoto zinazowakabili na kushirikishana mbinu za kuzikabili changamoto hizo katika maeneo yao ya kazi kwa sababu walimu wametoka katika maeneo mbalimbali ya nchi hii.
Amebainisha kuwa”kwa kuzingatia kuwa shule hizi zinatoka katika maeneo mbalimbali ya nchi pia imekuwa njia ya kufahamiana kwa walimu hawa, na tumeweka mikakati mbalimbali ya pamoja katika kuziimarisha shule hizo ziweze kufanikiwa zaidi” amesema Maduki.
No comments :
Post a Comment