Wednesday, January 27, 2021

RAIS MAGUFULI ATOA MSIMAMO CHANJO YA CORONA...."SITEGEMEI KUTANGAZA KUJIFUNGIA NDANI"


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa Butengo Chato mkoani Geita kabla ya kuzindua Shamba kubwa la Miti lenye jumla ya ekari elfu 69 mkoani Geita leo tarehe 27 Januari 2021.
**
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli amewatahadhalisha kuhusu chanjo ya COVID 19 inayoendelea katika mataifa mbalimbali na kuwasisitiza kusimama imara huku akisisitiza kuwa hategemei hata siku moja kuwatangazia wananchi wajifungie ndani kwa sababu ya Ugonjwa wa Corona.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Jumatano January 27,2021 wakati azindua shamba la miti la Silayo mkoani Geita.

"Mtatishwa sana ndugu zangu Watanzania lakini simameni imara, najua wapo baadhi ya watanzania hata wameondoka ndani ya nchi na kukimbilia maeneo mengine na kwenda kuchanjwa na walikochanjwa huko wamekuja huku wametuletea corona ambayo ni ya ajabu ajabu simameni imara.”

“Chanjo hazifai kama Wazungu wangekuwa na uwezo wa kuleta chanjo, hata chanjo ya Ukimwi ingekuwa imeshaletwa, chanjo ya kifua kikuu ingekuwa kifua ingeshaondoka, hata chanjo ya malaria ingekuwa ishapatikana hata chanjo ya kansa ingekuwa imeshapatikana, lazima watanzania tuwe waangalifu kwa mambo ya kuletewa letewa,” amesema Rais Magufuli.

“Sisi Watanzania hatujajifungia ndani na hatutegemei kujifungia ndani, na wala sitegemei kutangaza hata siku moja kwamba tunajifungia ndani kwa sababu Mungu wetu yupo hai na ataendelea kutulinda Watanzania. Tutaendelea kuchukua tahadhali nyingine za kiafya ikiwa pamoja na kujifukizia, unajifukizia huku unamuomba Mungu unasali..., sali huku unapiga zoezi la kulima mahindi, viazi ili ule vizuri ushibe. Corona ashindwe kuingia katika mwili wako,” ameongeza Rais Magufuli.

No comments :

Post a Comment