Thursday, January 14, 2021

BILIONEA LAIZER AJENGA SHULE NA KUIKABIDHI SERIKALI

***************************************************

Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MFANYABIASHARA maarufu wa madini ya Tanzanite, Saniniu Laizer ameikabidhi Serikali shule mpya ya msingi aliyoijenga kwa gharama ya shilingi milioni 466.8 kwenye Kitongoji cha Namelock, Kijiji cha Naepo, Kata ya Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Akisoma risala wakati wa kukabidhi shule hiyo mwanafamilia wa Laizer, Simon Siria alisema shule hiyo itakayowanufaisha wanafunzi wa jamii ya wakulima na wafugaji ina madarasa saba.
Siria alisema shule hiyo ilianza kujengwa darasa moja na wananchi wa kitongoji cha Namelock na kijiji cha Naepo mwaka 2017 ndipo bilionea Laizer akaimaliza mwaka huu.
Alisema jamii iliona waanze kujenga shule kwani wakati wa mvua wanafunzi huwa wanashindwa kuvuka korongo kwenda shule ya msingi Naepo iliyopo kilomita 1.5 kutoka katika eneo hilo.
“Shule hii itakuwa mkombozi kwa wanafunzi wa eneo hili kwani wengine ni wadogo na iliwalazimu kutembea kilomita 2.5 kwenda shule ya msingi Naisinyai na wengine kwenda Naepo,” alisema Siria.
Bilionea Laizer akizungumza wakati akikabidhi shule hiyo kwa Serikali alisema  imemgharimu jumla ya shilingi milioni 466.8 na hadi hivi sasa kuna wanafunzi 30 wanaosoma hapo.
Bilionea Laizer alisema shule hiyo ina madarasa saba, matundu 10 ya vyoo na nyumba mbili za walimu watakaoweza kuishi familia nne.
“Tunaomba serikali itupatie walimu na pia tunaomba shule hii iwe ya mchepuo wa kiingereza ili wanafunzi watakaosoma hapo wawe bora kwenye taaluma yao,” alisema Bilionea Laizer.
Katibu Tawala wa wilaya ya Simanjiro, Zuwena Omary alisema Serikali ipo pamoja na wachimbaji madini wenye kusaidia jamii kwa kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo.
“Kila mwanafunzi atakayesoma hapa na kufanikiwa kwenye maisha yake hawezi kukusahau na pia utapata thawabu kutokana na tukio hili,” alisema.
Alisema hivi sasa wanafunzi hao waliokuwa wanaotembea umbali mrefu kufuata masomo katika shule za mbali watakuwa wanasoma karibu kwenye shule hiyo ya msingi Saniniu Laizer.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka alisema wachimbaji wengine wa madini ya Tanzanite wanapaswa kuiga mfano wa bilionea Laizer kwa kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo ya jamii ikiwemo shule.
Ole Sendeka alisema atamuunga mkono bilionea Laizer popote penye kuhitaji mkono wa mbunge kwani amekuwa akisaidia jamii kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo shule na nyumba za ibada.

 

No comments :

Post a Comment