Katika sehemu ya kwanza Ijumaa iliyopita, Meneja Uhusiano na Itifaki Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Zalia Mbeo, alisema kuwa dhamana za serikali za muda mrefu huuzwa kwenye soko la awali kwa utaratibu wa ushindani kupitia minada, na kwamba baada ya hapo uuzaji wa dhamana hizo hufanywa kwenye soko la upili.
Majira Ijumaa 11 Desemba 2020
Wiki iliyopita tulizungumzia juu dhamana za serikali za muda mrefu na umuhimu wa wastaafu kuzinunua kama fursa muhimu kwao, mbali ya wawekezaji wengine. Wiki hii tutagusia hata jinsi kukokotoa hatifungani hizi za muda mrefu kwa kutumia baadhi ya mifano halisi, kama anavyoendelea kuelezea MWANDISHI WETU CHRISTIAN GAYA.
DHAMANA za muda mrefu ni hati ya madeni. Ikiwa na maana ya kwamba hati hiyo inaonesha mkopaji ambaye ndiye aliyetoa dhamana hiyo na mkopeshaji ambaye anakuwa ndiye aliyenunua dhamana na huyu ndiye anayeitwa mwekezaji.
Wakati serikali au mashirika
makubwa yanapohitaji kupata pesa kwa ajili ya kujiendesha, wanakopa pesa kutoka
kwa wawekezaji na wakishazipokea pesa hizo ndipo wanatoa hati ya dhamana ya
madeni kwa wawekezaji kuonesha kwamba pesa walizozipokea ni madeni.
Hati hizo za madeni zinaonesha muda usiobadilika ambao deni hilo litalipwa na huwa zina ukomo
wa zaidi ya mwaka mmoja. Kwa Tanzania hapa kuna hatifungani za miaka 2, 5, 7,
10, 15 na 20.
Hati hizo za madeni zinazotolewa na wakopaji zinakuwa na ahadi ya kiwango cha malipo ya riba kwa kipindi fulani. Koponi ya hati yako yaweza kusema kutakuwa na riba ya 10% ambayo italipwa kila mwaka mpaka ukomo wa deni utapofika, malipo ya riba yaweza kuwa mara moja, mbili, tatu na nne kwa mwaka kutegemeana na koponi ya hati inavyosema.
Kwa hapa Tanzania koponi za hatifungani zinasema malipo lazima yafanyika mara mbili kwa mwaka, mfano riba yako unayotakiwa kulipwa kwa mwaka mzima ni jumla ya milioni 4 hivyo kila baada ya tarehe fulani ya mwezi wa sita utakuwa unalipwa milioni mbili na itakapofika tarehe hiyo hiyo ya mwisho wa mwaka mwezi wa kumi na mbili utakuwa unalipwa milioni mbili na hivyo kufanya kulipwa jumla ya riba ya milioni 4 kwa mwaka.
Ahadi ya kurudishiwa kianzio ulichowekeza wakati deni linapofika ukomo. Hii ina maana kama ulitoa milioni 100 kwa mfano kununua bond, ikishafika ukomo utarudishiwa ile milioni 100 yako ambayo uliitoa.
Baadhi ya faida za kuwekeza
katika dhamana za serikali ni kwamba umiliki wake unahamishika, maana yake ni
kwamba unaweza kurithisha familia yako na kwa upande mwingine ni wa shilingi unaweza
kuziuza pale inapotekea ukawa na uhitaji wa pesa.
Pia dhamana za serikali zaweza kutumika kama dhamana za kuombea mikopo katika
taasisi kama vile za fedha zinazotoa mikopo.
Riba inayotolewa kutokana na
kuwekeza katika dhamana za serikali ni kwamba gawio ni kubwa na lenye kuaminika
zaidi kuliko riba zinazopatikana kwenye taasisi za fedha kama vile mabenki.
Kwa upande mwingine ni kwamba uwekezaji wake wa kwenye dhamana za serikali
unakuwa hauna hali hatarishi yoyote kubwa kwa mwekezaji na hivyo kuwa ni
uwekezaji wa uhakika na wa kipekee kwa sababu ya dhamana hizo kutolewa na
serikali.
Hapa ieleweke wazi ya kwamba kwa Tanzania dhamana za serikali zinatolewa na serikali ya Tanzania tu kupitia kwa Benki Kuu ya Tanzania lakini kwa nchi nyingine zilizoendelea sana kama vile Amerika, mashirika makubwa pia yanatoa dhamana za hatifungani za muda mfupi na za muda mrefu kwa wawekezaji.
Soko la awali yaani primary market hapa ni pale Benki Kuu ya Tanzania inapotoa kwa mara ya kwanza dhamana za serikali yaani treasury bonds kwa wawekezaji kwa niaba ya serikali.
Na soko la pili yaani
secondary market ni pale hii inapohusisha kuuza na kununua hatifungani za muda
mfupi yaani treasury bills na hii kitendo hiki huwa kinafanyika pale Dar Es
Salaam Stock Exchange yaani DSE. Hapa ndipo mahali ambapo mtu mwekezaji anapotaka
kuuza dhamana za serikali yaani treasury bond anayoimiliki anaweza kwenda
kuuza.
Kianzio cha kuwa mwekezaji wa moja kwa moja kwenye dhamana za muda mrefu kwa
Tanzania ni shilingi 1,000,000. Hii ina maana ya kwamba ukiwa na mtaji wa
kuanzia milioni moja basi unaruhusiwa moja kwa moja kushiriki kwenye mnada wa dhamana
za serikali.
Unawezaje kupata pesa na faida kupitia dhamana za serikali za muda mrefu. Chukulia mfano huu ambao ulifanyika kwenye zabuni ya tarehe 22-Jul-2015 na Benki Kuu ya Tanzania.
Fikiria ya kuwa dhamana za serikali zilitolewa punguzo ya shilingi za kitanzania 75.88133/100. Kwa maana hiyo ni kwamba koponi moja yenye thamani ya shilingi 100,000.00 iliuzwa kwa shilingi 75,813.3.
Kwa upande mwingine ni kwamba ili kuvutia wawekezaji hivyo shilingi moja yaani 100 iliuzwa kwa Shilingi 75.813.3 ambayo ni sawa na koponi ya riba ya asilimia 9.18
Hivyo taarifa muhimu katika majibu
ya mnada huo ni ifuatavyo: Kiwango cha koponi ni asilimia 9.18. Muda wa malipo
ya koponi ya kila nusu mwaka ni
23 Julai na 21 Januari. Na tarehe ya ukomo wake ni 23-Jul-2020.Thamani ya
koponi moja ni shilingi laki moja.
Dhamana zilitolewa kwa punguzo ya Shilingi 75.8133/100 hii inamaanisha ya kuwa koponi moja yenye thamani ya shilingi 100,000 iliuzwa kwa shilingi 75,813.3
Chukulia kwa mfano kama ulinunua koponi 1000 zenye thamani ya Shilingi laki moja (TZS 100,000) ambazo umezipata kwa punguzo hiyo ya Shilingi 75,813.3 kwa kila koponi moja, ina maana utakuwa na uwekezaji wa koponi 1000x Shilingi laki 100,000 (1000x Shilingi 100,000) ambayo ni sawa na Shilingi milioni 100,000,000 za Kitanzania (TZS 100,000,000).
Lakini kumbuka ya kuwa umepata punguzo la Shilingi 75,813.3, kwa hiyo ulichokitoa mfukoni ni koponi elfu moja x Shilingi 75,813.3 yaani (1000xTZS 75,813.3), ambayo ni sawa na jumla ya Shilingi milioni 75,813,300 za Kitanzania.
Hivyo unaweza kuona umetoa Shilingi milioni 75,813,300 na hatimaye kwa maamuzi yako ya kuwekeza ukapata mali yenye thamani ya shilingi milioni 100,000,000.
Kwa mahesabu ya haraka ina maana kuna faida kama ya Shilingi milioni 24,186,700 za Kitanzania ambayo itakuwa imejificha kwenye uwekezaji wako. Kwa kufanya maamuzi hayo ya uwekezaji ina maana mpaka sasa umeshatengeneza kama shilingi milioni 24.
Kwa kutumia taarifa za kwenye mfano wetu hapo juu unaweza kuona ni kiasi gani utakuwa unapata kama pato la riba kwa kipindi chote cha uwekezaji, ambacho ni kipindi cha miaka mitano utokanao na uwekezaji wako. Inaendelea wiki ijayo
No comments :
Post a Comment