Thursday, December 31, 2020

Umoja wa Falme za Kiarabu wavutiwa kuwekeza Zanzibar, Rais Dkt.Mwinyi awakaribisha

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewaomba wawekezaji kutoka nchi za Jumuiya ya Kiarabu (UAE) kuja kuwekeza nchini, hususan katika sekta ya utalii, anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini.
Dkt. Mwinyi ametoa wito huo Ikulu jijini Zanzibar Desemba 30, 2020 wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Falme za Kiarabu nchini Tanzania, Khalifa Abdulrahman Almarzouqi, aliyefika kujitambulisha kwa Rais.

Amesema, katika dhana ya kuimarisha uchumi, Zanzibar inalenga kuimarisha uchumi wake kupitia Uchumi wa Buluu, hivyo inahitaji wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali Duniani, ikiwemo UAE ili kuwekeza kupitia sekta ya utalii yenye vivutio mbalimbali katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalenga kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa eneo muhimu la uwekezaji, hivyo akawataka wawekezaji kutoka nchi hizo kuja kuwekeza katika miradi mbalimbali.

Amesema, sheria za uwekezaji ikihusisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya miradi mbalimbali zinatoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya visiwa.

Aidha, Dkt. Mwinyi ametoa pongezi kwa nchi za jumuiya hiyo kwa uhusiano na ushirikiano mzuri na wa muda mrefu kati yake na Zanzibar, pamoja na misaada mbalimbali inayoendelea kutolewa kupitia nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Amesema, nchi za Jumuiya ya Kiarabu zimekuwa zikiunga mkono juhudi za serikali na hivyo kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Zanzibar, ambapo kwa nyakati tofauti zimesaidia miradimbali, ukiwemo Mfuko wa ‘Khalifa Fund’ unaolenga kuwawezesha kiuchumi Vijana wa Zanzibar.

Vile vile ameziomba taasisi na wadau wa maendeleo kutoka nchi hizo kuunga mkono juhudi za serikali zinazolenga kuuweka katika mazingira bora zaidi Mji Mkongwe wa Zanzibar, (ulio katika Urithi wa Ulimwengu) ili uweze kuwa eneo la kiuchumi.

Nae Balozi wa UAE nchini Tanzania, Khalifa Abdulrahman Almarzouqi amemhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kuwa UAE itaendeleza uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Zanzibar, sambamba na kuendelea kuisaidia nchi hiyo katika nyanja za kiuchumi na kijamii.

Aidha, ameahidi kuwashajiisha wawekezaji wa nchi hizo kuja nchini kuwekeza, akibainisha kuwepo kwa kampuni mbali mbali zinazowekeza katika sekta ya utalii kupitia miradi mbali mbali, ikiwemo ya ujenzi wa Hoteli kubwa za kitalii, michezo ya baharini na miradi mingineyo. 

 

No comments :

Post a Comment