********************************
Na Mwandishi wetu, Kiteto
MKUU wa Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph
Makungu amewaasa Madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Kiteto, kuepuka vitendo vya rushwa viliyotafsiriwa kwa vitendo 24.
Makungu
akizungumza na madiwani na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto
amesema vitendo hivyo 24 vipo kwa mujibu wa sheria ya kuzuia na
kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Amesema ni kosa
kwa mtu yeyote au wakala wake kutumia nyaraka kwa lengo la kudanganya na
kujipatia fedha au faida kwenye shughuli za mwajiri wake zikiwa na
maelezo ya uongo, potofu au kasoro yoyote.
“Tumeona katika
kipindi kilichopita baadhi ya madiwani walilazimisha kulipwa posho za
kujikimu, posho za kujikimu msingi wake ni diwani awe amesafiri na
kulala nje ya makazi yake ili kuhudhuria mkutano siku inayofuata kwa
hiyo akibainika hatua zitachukuliwa chini ya kifungu hicho,” amesema
Makungu.
Amesema wapo
baadhi ya wakuu wa idara wanaoandaa vikao hewa, ukumbi hewa, kisha
wanawalipa washiriki hewa wa vikao au mikutano hiyo na wanadai malipo
baada ya kupata stakabadhi na pia wengine wanaandaa miradi hewa ukifika
sehemu husika haipo.
Amesema wapo
baadhi wanaandaa safari hewa kwa kuonyesha kuwa walisafiri na kutaka
malipo ili hali wanatambua kuwa hawakusafiri kwenda popote.
“Madiwani mnayo
majukumu ya kubaini hayo yote na kuyatolea maazimio ya haki kwenye vikao
vyenu kwa manufaa ya wananchi mnaowawakilisha,” amesema Makungu.
Amesema katika
halmashauri kuna manunuzi ya huduma mbalimbali kama mafuta ya magari na
vifaa mbalimbali ambapo bei hukuzwa pengine hata mara mbili ya bei yake
halisi.
“Kwenye pembejeo
za kilimo nyaraka za udanganyifu pia hutumika kwani wapo baadhi ya
maofisa kilimo hutumia majina ya marehemu kupitia mawakala ili wapate
pembejeo na madiwani wapo kwenye kata wanashindwa kubaini hilo,” amesema
Makungu.
Amesema ni kosa
kwa mtu yeyote kutumia madaraka yake huku akivunja sheria katika
kutekeleza au kuacha kutekeleza majukumu yake ya kiofisi kwa lengo la
kujipatia manufaa yasiyo halali yeye mwenyewe au mtu mwingine.
Amesema sheria
inaweka katazo kwa watakaotumia udiwani kujipatia ukandarasi wafahamu
watakumbana na TAKUKURU kama sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2011
inavyoelekeza.
Amesema TAKUKURU
ni kiongozi wa mapambano ya rushwa hata hivyo kila mwananchi anawajibika
katika vita dhidi ya rushwa kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 27 (2).
“Ibara hiyo
inasema watu wote wanatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya Mamlaka ya
nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za ubadhirifu na uharibifu na
kuendesha uchumi wa Taifa kwa makini kama watu ambao ndiyo waamuzi wa
Hali ya baadaye ya Taifa lao,” amesema Makungu.
No comments :
Post a Comment