Monday, December 7, 2020

STAMICO YAPATA TUZO YA KUWA MSHIRIKI BORA WA BIASHARA (Best Business Partner of the year 2020)


Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limezidi kuchanja mbuga kimataifa baada ya kupata tuzo ya kuwa mshiriki bora wa kibiashara katika sekta ya madini.

Tuzo hiyo imetolewa na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Prof.Dkt. Ratlan Pardede katika hafla ya kutambua na kuthamini michango ya wafanyabiashara wa Tanzania wanaofanya biashara na nchi ya Indonesia. Sherehe za utowaji wa tuzo hizi zilifanyika katika ofisi za ubalozi wa Indonesia zilizopo jijini Dar es salaam.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hii Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dk. Venance Mwasse ameshukuru ubalozi wa Indonesia kwa kutambua mchango wa shirika katika uwejezaji katika sekta ya madini na kusema kuwa tuzo hiyo ni ishara ya mabadiliko ya STAMICO katika kujiendesha kibiashara na kujitanua kimataifa.

Dk. Mwasse alisema STAMICO imekuwa na ushirikiano wa kimkakati wa muda mrefu na Shirika la Madini la Indonesia lijulikanalo kama PT.Timah. Ushirikiano huo umepelekea kusainiwa hati ya makubaliano katika kuendeleza miradi mbalimbali hususani ya madini ya bati yaliyopo wilayani Kyerwa.

Ushirikiano huo umefungua milango ya wataalamu wa madini kutoka Shirika hilo la madini kuja nchini kujionea maeneo mbalimbali ya uwekezaji.

Katika kuendeleza ushirikiano huo Balozi wa Indonesia Prof. Dkt. Ratlan Pardede ameishukuru STAMICO kwa hatua ya kusaini hati ya makubaliano na kutoa ushirikiano mkubwa wa kitaalamu kwa wawekezaji waliokuja nchini kwa kuwapeleka katika maeneo mbalimbali ya miradi.

Aidha, ameipongeza STAMICO kwa jitihada zake za dhati za kuendeleza mawasiliano na taasisi ya PT.Timah licha ya kuwepo kwa changamoto ya ugonjwa wa Covid19 ambao ulitikisa dunia.
Alisema hii ni dhamira ya dhati inayodhihirisha nia ya Shirika hilo katika kuwavutia wawekezaji wa nje kwenye sekta ya madini.

Tuzo hii litaongeza nguvu zaidi kwa Shirika kuendelea kuwasaidia wachimbaji wadogo, kwa kuwaunganisha na wawekezaji ili waweze kuboresha shughuli na kuinua kipato chao alisema.

Mheshimiwa Balozi aliahidi kuendelea kufanya kazi na STAMICO ili kuendelea kuboresha sekta ya madini nchini na alitoa mwaliko kwa wataalamu wa STAMICO kutembelea nchini indonesia ili kupata uzoefu utakaoleta chachu ya mabadiliko katika sekta hiyo.

Mkurugezi wa STAMICO alimweleza Mheshimiwa Balozi juu ya mradi wa madini ya bati inayolega kuboresha soko la madini hayo ili kuchochea ukuwaji wa uchimbaji wa madini ya bati hasa tukilenga wachimbaji wadogo,” alisema.

Aidha, Alisema Shirika limeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Dk. John Magufuli za kuboresha na kuendeleza sekta ya madini tukilenga wachimbaji wadogo wa Tanzania.

 

No comments :

Post a Comment