Monday, December 21, 2020

SERIKALI YAJA NA MFUMO SHIRIKISHI KUDHIBITI UVUVI HARAMU

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza katika mkutano wa hadhara na wakazi wa Kijiji cha Mchinga Namba Mbili, kilichopo Wilaya ya Mchinga Mkoani Lindi wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo na kubainisha kuwa wizara itaandaa mfumo shirikishi wa kupambana na uvuvi haramu siku zote badala ya kuwa na operesheni za vipindi maalum.

Mkuu wa Wilaya ya Lindi Bw. Shaibu Ndemanga ambaye amemwakilisha mkuu wa mkoa wa Lindi Bw. Godfrey Zambi katika ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki, akitoa taarifa ya mkoa na namna walivyofanikiwa kutokomeza uvuvi haramu wa kutumia mabomu kwa asilimia mia moja.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (aliyekaa katikati) amepata fursa ya kusikiliza maoni, maswali na kero mbalimbali za wavuvi alipofanya ziara ya kikazi katika Kijiji cha Mchinga namba Mbili kilichopo Wilaya ya Mchinga Mkoani Lindi na kuahidi kero zinazohusu wizara atahakikisha anazifanyia kazi ili wavuvi waweze kufanya shughuli zao bila bughudha na kuwatahadharisha wasijiingize katika uvuvi haramu.

Muonekano wa baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Mchinga Namba Mbili, kilichopo Wilaya ya Mchinga Mkoani Lindi waliohudhuria mkutano wa hadhara wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki aliyefika kijijini hapo katika ziara yake ya kwanza mkoani humo, kwa ajili ya kusikiliza kero mbalimbali zinazowakumba wavuvi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akishika zao la mwani wakati alipotembelea mashamba ya zao hilo yaliyopo kwenye Bahari ya Hindi, katika kijiji cha Mchinga Namba Moja mara baada ya kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mchinga Namba Mbili, vilivyopo Wilaya ya Mchinga Mkoani Lindi na kuwataka wakulima wa zao hilo waliongezee thamani kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwemo sabuni.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa ameshika jongoo bahari ambapo ni moja ya mazao yaliyopo baharini ambayo yana soko kubwa nje ya nchi wakati alipokuwa anatembelea mashamba ya zao la mwani yaliyopo kwenye Bahari ya Hindi, katika kijiji cha Mchinga Namba Moja kiilichopo Wilaya ya Mchinga Mkoani Lindi.

Mbunge wa Jimbo la Mchinga Mama Salma Kikwete akizungumza kwa niaba ya wabunge wa Mkoa wa Lindi wakati wa ugeni wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki katika ofisi za mkoa huo na kubainisha changamoto mbalimbali za wavuvi zikiwemo za vitendea kazi na bei ndogo ya zao la mwani. Waziri Ndaki yuko mkoani Lindi kwa ziara ya Kikazi ya siku mbili.

Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael Madalla akifafanua namna wizara inavyochukua hatua mbalimbali kuhamasisha wananchi kufuga samaki, upatikanaji wa vifaranga bora pamoja na vyakula bora vya samaki, wakati wa kikao cha uongozi wa Mkoa wa Lindi na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki aliyefika mkoani hapo kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.

……………………………………………………………………………………………………………..

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema serikali itaandaa mfumo shirikishi na endelevu wa kudhibiti zaidi uvuvi haramu ambao utafanya mikoa na wilaya zishiriki

kikamilifu katika kutokomeza uvuvi huo badala ya kuwa na operesheni za kutafuta wavuvi haramu.

Waziri Ndaki amebainisha hayo (21.12.2020) alipokuwa katika mkutano wa hadhara na wakazi wa Kijiji cha Mchinga Namba Mbili, kilichopo Wilaya ya Mchinga Mkoani Lindi wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo na kubainisha kuwa mfumo huo utasaidia serikali kuondokana na operesheni za za vipindi maalum na badala yake mfumo uwe unafanya kazi siku zote.

“Tuwe na mfumo endelevu wa kumaliza kabisa tatizo la uvuvi haramu kwa hiyo tutafanya hivyo badala ya kuwa na operesheni au zimamoto ya kutafuta wavuvi haramu tuwe na mfumo unaofanya kazi siku zote huku mikoani, wilayani na mahali pengine popote.” Amesema Mhe. Ndaki

Waziri Ndaki amewataka pia watu wanaojihusisha na wanaofikiria kujiingiza katika uvuvi haramu kwamba watatafutwa popote watakapokuwa na watapata adhabu kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za nchi huku akipongeza wananchi wanaoishi Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi, kwa kudhibiti uvuvi haramu hususan unaotumia mabomu ambao kwa mujibu wa taarifa ya Mkoa wa Lindi, uvuvi huo umedhibitiwa kwa asilimia mia moja, huku akiahidi kuyafanyia kazi mapungufu yaliyopo ndani ya wizara katika kudhibiti uvuvi haramu.  

Aidha, kuhusu zao la mwani Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wakazi hao wa Kijiji cha Mchinga Namba Mbili ameyataka makampuni yanayonunua zao hilo kutumia mizani zilizo sahihi na kuacha mara moja kuwadhulumu wakulima hao na kuwataka pia wakulima kuangalia uwezekano wa kuliongezea thamani zao hilo ili kuuza kwa bei nzuri tofauti na bei ya sasa ya kilo moja kwa Shilingi Elfu Moja ambayo wakulima hao wanasema haitoshelezi.  

Pia, amesema wizara itaangalia utaratibu kwa kushirikiana na halmashauri kuwawezesha wakulima wa mwani kupitia vikundi vyao katika kutengeneza bidhaa zitokanazo na mwani badala ya kuuza kama malighafi ili waweze kunufaika zaidi kibiashara kwa kujiongezea mapato.

Awali akiwa katika Ofisi za Mkoa wa Lindi, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesomewa taarifa ya mkoa huo na Mkuu wa Wilaya ya Lindi Bw. Shaibu Ndemanga ambaye amemwakilisha mkuu wa mkoa huo Bw. Godfrey Zambi ambapo taarifa hiyo imebainisha mkoa kwa kushirikina na wizara umedhibiti uvuvi haramu kwa asilimia mia moja na kubainisha kuwa mkoa utaendelea kuhakikisha unadhibiti kabisa vitendo hivyo.

“Mheshimiwa Waziri katika eneo hili tumefanya vizuri sana miaka mitano iliyopita tusingeweza kusafiri kutoka pale Mnazi mmoja hadi hapa mkoani bila kusikia bomu tuna zaidi ya miaka mitatu hadi minne hatujasikia bomu kwa hili tumedhibiti kwa asilimia mia moja.” Amesema Bw. Ndemanga

Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa Mkoa wa Lindi, Mbunge wa Jimbo la Mchinga Mama Salma Kikwete amemwambia Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki wavuvi wa mkoa huo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya vifaa vya uvuvi kwa kuwa wanatumia zana duni badala ya kutumia boti za kisasa na kuwepo kwa soko la kisasa la kuuzia mazao ya samaki, huku akitaka pia akinamama wawezeshwe katika kilimo cha mwani hususan suala la bei.

“Lindi tuna changamoto za vitendea kazi tunakuomba mheshimiwa waziri ulichukue suala la changamoto uende nalo ukalifanyie kazi ninaamini na ninajua baada ya muda mfupi tutapata majibu ambayo ni chanya hususan katika upatikanaji wa boti ya kisasa ya uvuvi na suala la bei ya zao la mwani.” Amefafanua Mama Kikwete.

Mapema akiwa njiani kuelekea Mkoani Lindi kuanza ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo, ikiwa ya kwanza kikazi nje ya Mkoa wa Dodoma tangu kuapishwa kushika wadhifa huo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amefika katika ofisi za taasisi na wakala zilizo chini ya wizara hiyo zilizopo Kata ya Naliendele, Manispaa ya Mtwara Mikindani na kuwataka watumishi hususan wa Kituo cha Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (FRP) kufuata sheria, taratibu na kanuni zilizopo katika kudhibiti uvuvi haramu na kutowaonea watu kwa kuwabambikizia kesi.

Amewataka watumishi hao kuwa waaminifu kwa kuhakikisha faini zinazolipwa ziwe halali za kieletroniki badala ya kuwaandikia faini kwa risiti za mkono na kutowaonea wavuvi kwa namna yoyote.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki yuko katika ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Lindi ambapo anatarajia pia kukutana na wakulima na wafugaji katika kuhakikisha serikali inaondoa kero za kutoelewana kati ya watu wanaojishulisha katika sekta hizo mbili.

 

No comments :

Post a Comment