Friday, December 11, 2020

NBS, OCGS na UNFPA Kushirikiana Kufanya Utafiti Afya ya Uzazi Tanzania

Na Mwandishi Wetu, MAELEZO.

TANZANIA inaungana na Mataifa zaidi ya 43 Duniani kufanya utafiti wa nne wa tathmini ya afya ya uzazi na huduma zitolewazo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa mwaka 2020 ambao unalenga kupata takwimu zitakazosaidia kuimarisha sekta ya afya kwenye mataifa hayo.

Utafiti huo ambao unaratibiwa kwa pamoja kati ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar (OCGS) utasaidia

kukabiliana na changamoto za huduma hizo ambazo kwa sasa zinapatikana kwenye maeneo mengi nchini.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam jana mara baada ya ufunguzi wa Kikao cha Wadau wa Utafiti huo, Mtaalamu wa Programu ya Idadi ya Watu na Maendeleo kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na idadi ya watu Duniani- UNFPA Bw. Samwel Msokwa, amesema utafiti huo utaendelea kufanyika hadi mwaka 2030 utakapofanyiwa mapitio ya kidunia ya kuangalia tathmini zake.

“Utafiti huu ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili, kwa Tanzania huu ni wa nne na unatarajiwa kufanyika tena hadi kipindi cha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu kitakapofikia ukomo mwaka 2030” Alieleza Msokwa.

Mtaalamu huyo kutoka UNFPA aliongeza kuwa baada ya mwaka 2030 mapitio ya kidunia yatafanyika kuangalia ni kwa namna gani utafiti huu uendelee kufanyika kwa kuwa takwimu zinataonesha hali halisi na mwelekeo wa namna huduma hizi za afya zinavyotolewa.

Msokwa alisema kutokana na maendeleo makubwa ya tekinolojia ambayo yameleta mabadiliko makubwa katika sekta ya afya ikiwemo vitendea kazi na na hata namna ya utoaji wa huduma zenyewe, utafiti huu unakuwa na umuhimu sasa kwani takwimu zitakazozalishwa zitasaidia kupanga na kufanyia maamuzi yatakayopelekea kukidhi mahitaji ya sasa ya sekta ya afya.

Mtaalamu huyo kutoka UNFPA alieleza kuwa Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linashirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wadau wa maendeleo kufanya kazi mbalimbali za kuzalisha takwimu ikiwemo Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi, Utafiti wa Afya ya Mama na Mtoto pamoja na Sensa ya Watu na Makazi.

Awali, akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo kwa niaba ya Menejimenti za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar (OCGS), Sabina Raphael Daima kutoka OCGS alieleza kuwa matokeo ya utafiti huo yatasaidia sekta ya afya nchini hususan hali ya upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi nchini.

“Matokeo yataisaidia Serikali, Shirika la UNFPA na Wadau wengine katika programu ya FP2000 ya kupima na kufuatilia matokeo ya hatua zilizochukuliwa katika utoaji wa huduma na dawa za afya ya uzazi” alieleza Sabia.

Sabina ambaye ni Mkurugenzi wa Takwimu za Ajira katika Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar, aliongeza kuwa matokeo ya utafiti huo yatasaidia kuchochea programu za afya na watunga sera kuweka vipaumbele kwa uzazi wa mpango na huduma za afya mama na mtoto.


Utafiti huo ambao unaratibiwa kwa pamoja kati ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar (OCGS) unagharimiwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirika hilo la Umoja wa Mataifa unatarajiwa kuanza mwishoni mwa Disemba, 2020. 

 

No comments :

Post a Comment