Mkuu wa Mkoa wa
Manyara, Joseph Joseph Mkirikiti akizungumza kwenye kikao cha kamati ya
ushauri ya Mkoa huo (RCC) kilichofanyika mjini Babati.
Mbunge wa Jimbo la Kiteto Mkoani Manyara, Wakili msomi Edward Ole Lekaita Kisau akizungumza kwenye kikao cha RCC mjini Babati.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul akizungumza kwenye kikao cha RCC mjini Babati.
****************************************
Na Mwandishi wetu, Manyara
MKUU wa Mkoa wa
Manyara, Joseph Joseph Mkirikiti amewataka wadau wa maendeleo nchini
kuwekeza kwenye Wilaya za Mkoa huo kutokana na kuwepo kwa fursa
mbalimbali za kiuchumi.
Mkirikiti ameyasema
hayo wakati akizungumza mjini Babati kwenye ufunguzi wa kikao cha kamati
ya ushauri cha mkoa huo (RCC) kilichohusisha wakuu wa wilaya, wabunge,
wakurugenzi, wenyeviti wa halmashauri, makatibu tawala na wadau
mbalimbali wa maendeleo.
Amesema mkoa huo una
fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo, mifugo, madini, uvuvi,
utalii na nyingine hivyo ni muda wa kuchangamkia fursa hizo kwenye mkoa
huo wa tatu kwa ukubwa nchini.
“Ni vizuri
tukajadiliana na kila mmoja wetu akajipima ili tukauweka Mkoa wetu kuwa
katika namna bora Zaidi” Alisema Mhe.Mkirikiti.
Hata hivyo, amewataka
watendaji kujenga mahusiano mazuri ya kazi kati yao na wawakilishi wa
wananchi ili kujua matatizo yanayoikabili jamii kwa lengo la kuwaletea
maendeleo katika maeneo mbalimbali.
“Tuache kulalamika
sasa ni muda wa kila mmoja kuja na mbinu za kufanikisha majawabu na
kutotoa changamoto pekee, tutumie kikao hiki tujadiliane kwa uwazi,
bila shaka nina Imani tukiangalia yale yaliyojadiliwa na wenzetu katika
vikao vilivyopita tukaweka na dira yetu bila shaka tutafanikiwa kwa
kupiga hatua zaidi,” amesema Mkirikiti.
Naibu Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Babati
Mjini amesema bado changamoto ya bei ya maji ipo juu kwa wananchi hivyo
Bawasa wahakikishe wanateremsha ankara ili iwiane na maeneo mengine
wanavyolipa.
“Wananchi wa Mji
mdogo wa Kiabakari Mkoani Mara wanalipa ankara ya maji shilingi 300 kwa
kila uniti sisi Babati ndiyo mji pekee tunalipishwa ghali kwani kwa kila
uniti tunatozwa shilingi 1,800 hapana kwa kweli, Bawasa mnapaswa
kutafakari hilo,” amesema Gekul.
Mbunge wa jimbo la
Kiteto, Wakili msomi Edward Ole Lekaita Kisau, amesema baadhi ya sehemu
za eneo hilo kuna changamoto ya mawasiliano ya simu hivyo upatikane
ufumbuzi na pia wananchi bado wanalalamikia kukatika kwa nishati ya
umeme kila mara na hawapatiwi majawabu yanayojitosheleza.
“Wafanyakazi wa
Tanesco wakiulizwa juu ya kukatika mara kwa mara kwa umeme, badala ya
kuja na wajawabu yenye tija wanadai kuwa nishati hiyo imetoka Dodoma,
utadhani Dodoma ni eneo lingine tofauti na nchi hii,” amesema Ole
Lekaita.
Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga amesema migogoro ya
ardhi pia inatakiwa kupatiwa ufumbuzi ili kero hiyo ya wananchi
itatuliwe.
No comments :
Post a Comment