Thursday, December 17, 2020

MAKAMU WA PILI ZANZIBAR AAGIZA USIMAMIZI WA MASHINE MAALUMU HOSPITALI YA KASKAZINI A


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akisalimiana na Wananchi waliofika Hospitali ya Wilaya Kaskazini A iliyopo Kivunge kupata huduma za Afya baada ya kufanya ziara ya ghafla.


MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kufuatilia

Makubaliano yaliyopo baina ya Kampuni ya Pyramid iliyoko Dar es salaam na Taasisi ya Hipsi ya Zanzibar juu ya usimamizi wa Mashine Maalum ya uchunguzi wa Maabara iliyowekwa kutoa huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Kaskazini A iliyopo Kivunge.

Agizo hilo la Mheshimiwa Hemed Suleiman alilolitoa wakati wa
ziara ya ghafla katika Hospitali hiyo na kuangalia uwajibikaji wa
Watendaji wa Hospitali hiyo pamoja na huduma za Afya wanazopata
Wananchi, na hilo limekuja kufuatia Mashine hiyo kutofanya kazi kwa tatizo la
kuungua kwa Taa wakati bado iko kwenye dhamana ya Kampuni hiyo.

Amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Hipsi iliyoshirikiana na
Kampuni hiyo ya Pyramid kutoa mrejesho wa taarifa ndani ya masaa Kumi
na Mbili na kupelekewa kwa Mkuu wa Mkoa Kaskazini na baadaye
kuwasilishwa kwake kwa hatua zitazostahiki.

 Hemed alisema licha ya kwamba  Taifa limekuwa likipokea
misaada na baadhi ya michango kutoka kwa Wafadhili na Taasisi za
Kitaifa na Kimataifa kwa ajili ya huduma za Jamii lakini Serikali
haitaridhia kuona Wananchi wake wanaendelea kukosa huduma  za Afya kwa
dharau za Mtendaji mmoja.

Alisema Serikali italazimika kufuatilia mazingira halisi ya huduma za
Maabara za Hospitali hiyo na pale itakapohisi kwamba wale waliopewa
jukumu la kutoa huduma hizo hawako makini haitasita kuachana nao na
badala yake italazimika kununua Mashine nyingine.

Akizungumzia huduma za damu salama, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
aliwataka Watendaji wa Kitengo cha Damu salama kwenye Hospitali hiyo
ya Wilaya  kutobweteka kwa kusubiri Wananchi kuchangia Huduma hiyo
inayohitaji Elimu na uhamasishaji mkubwa.

Mheshimiwa Hemed alisema Watendaji wa Kitengo hicho wanapaswa kutoa
Taarifa kwa Wakuu wa Wilaya na Mkoa kwani wao tayari wana uzoefu
mkubwa katika shughuli za uhamasishaji wa uchangiaji damu wanazokuwa
wakizitekeleza kila Mwaka.

Alisema inasikitisha kuona Kitengo cha Damu salama cha Hospitali hiyo
imekusanya uzito wa Uniti Nne tokea kianze kutoa huduma Mwezi Mmoja
uliopita wakati hata robo ya mahitaji halisi ya matumizi ya huduma
hiyo kwa Wagonjwa haijakidhi.

Akisalimiana na Wananchi waliofika Hospitali hiyo kupata huduma za
Afya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman
aliwahakikishia Wananchi hao kwamba Serikali Kuu imejizatiti katika
kuona huduma za Afya zinawafikia popote walipo.

Mheshimiwa Hemed alisema changamoto zinazowapata Wananchi wakati wa
huduma hizo ikiwemo baadhi ya ukosefu wa Dawa wanazoandikiwa na
Dakatari zitatafutia njia ya kuziondosha kwa Vile Serikali bado
inaendelea na Sera zake za kutoa Matibabu Bure.

Alisema zipo baadhi ya Dawa ambayo matumizi yake kwa Wagonjwa
hufanyika kwa nadra na zina gharama kubwa lakini hicho hakitakuwa
kikwao isipokuwa utaratibu maalum utaandaliwa kupitia Bohari Kuu ya
Dawa Zanzibar ili kuona pale Mgonjwa anapohitaji kupatiwa Dawa hizo
inawezekana.

Mapema Daktari Dhamana wa Hospitali ya Wilaya ya Kaskazini A iliyopo
Kivunge Dr. Tamimu Said Hamad alisema huduma za Afya katika Hospitali
hiyo zimeimarika kiasi kwamba hata malalamiko ya baadhi ya Wagonjwa
yanaendelea kupungua siku hadi siku.

Dr. Tamimu alisema zipo changamoto za kubanduka kwa paa na kupasuka
kwa baadhi ya kuta na Vyumba vya jengo jipya la Hospitali hiyo jambo
lililowatia hofu hasa kwenye vyumba wanavyolazwa wagonjwa wanaopatiwa
huduma za Afya.

Alisema Jengo hilo Jipya lililokabidhiwa Serikalini baada ya kumaliza
Ujenzi wake Mnamo Mwezi Aprili Mwaka huu, limezinduliwa  Rasmi kwa
ajili ya kutoa huduma za  afya Mwezi Oktoba Mwaka huu.

Nao kwa upande wao baadhi ya Wananchi waliofika kupata huduma za Afya
Hosptalini hapo wamemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar jinsi
wanavyoendelea kupata faraja kutokana na huduma wanazopata jambo
linalowatia moyo.

Hata hivyo Wananchi hao waliishauri Serikali kuendelea kufuatilia
huduma za Afya zinazotolewa na baadhi ya Hospitali Nchini ambapo wapo
baadhi ya Watendaji wanaendelea kuwasumbuwa Wagonjwa.

Walisema usumbufu huo mara nyingi hutokea 112 na pale mgonjwa
anapotakiwa kufanya vipimo kutokana na mradhi yanayomsumbua inakuwa
mtihani mkubwa jinsi anavyozunguusha hadi kukata tamaa.

 

No comments :

Post a Comment